Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lulindi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nikushukuru wewe kwa nafasi. Vilevile, ninaomba pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kunipa uhai na kuendelea pale nilipoishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitakuwa mbali sana na wachangiaji waliopita, hususani katika kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na timu yake, pamoja na Mheshimiwa Rais. Kwa kweli tunayo mengi ya kuzungumza kuhusiana na masuala, acha tu umeme au nishati, lakini na mambo mengine ya kimaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukosoa ni kichocheo cha tija ya maendeleo na ni kichocheo cha tija ya kufanya au utekelezaji. Tunapokosoa hatumaanishi kwamba hii Serikali labda ya Awamu ya Sita haijafanya mambo mema mazuri, hapana. Ukiangalia ni Serikali ambayo imefanya vizuri sana katika mambo mengi kama nilivyosema hapo, ukiacha nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa kazi zilizofanyika katika awamu hii kwenye Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na timu yake ya nishati, tunayo ya kuzungumzia, kwa maana ya kukosoa kwa nia ile ile ya kuongeza chachu ya kuhamasisha kufanya jambo liwe jema zaidi; kwamba maendeleo yawe makubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninataka nizungumzie dhana hii ya kupeleka umeme katika vijiji vyote vya nchi hii. Ninakubaliana na hilo na sina shaka kwa hilo; lakini katika mazingira yangu niko tofauti. Ninaomba nitofautiane kidogo kwa lengo lile la kutia chachu kusudi tuweze kufikia lile lengo la kukamilisha vijiji. Mazingira niliyokuwa nayo mimi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na vitongoji vingi vikubwa ambavyo vyenye hadhi sawa kabisa na vijiji, lakini vitongoji hivi viko katika umbali mrefu kutoka kwenye makao makuu ya kijiji mpaka kuvifikia. Sasa unakuta umeme umeishia kwenye makao makuu ya kijiji peke yake, lakini wakati huo kule kitongojini umeme haujafika; na kama nilivyosema kwamba kuna idadi ya watu wengi, kuna vitongoji vingine kuna zaidi ya watu 600. Maana yake ni kwamba watu walioko pale wana hadhi ya kuwa kijiji. Kwa hiyo kuwa-treat kama ni kitongoji kwa kweli ninafikiri inakuwa siyo sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kwamba, hivi vitongoji vyote vyenye umbali mrefu kutoka kwenye makao makuu, vingine ni umbali wa kilometa tano, halafu vyenyewe havipewi umeme kwa kipaumbele; kwa minajili ya kuwa ni vitongoji vitakuja kupewa baadaye; kwa kweli ningeomba jambo hili lisiwe katika jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nitolee mfano. Vitongoji hivyo hivyo unakuta ni vitongoji ambavyo vina kazi au vina taasisi muhimu sana kama vile shule na zahanati ziko pale, lakini sasa unakuta havijapewa umeme kwa sababu tu ni vitongoji. Sasa hali hii inafanya hata zile taasisi zisifanye vizuri. Nikitolea mfano kwenye Kata ya Mkululu kuna Kitongoji cha Lusonje ambacho kina watu 700; na kuna shule pale. Halikadhalika Mkonde kuna takribani watu 600, na kuna msikiti hapo; Nanjota kuna Kitongoji cha Mnazi Mmoja kuna watu zaidi ya 700 na kuna ujenzi wa zahanati kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kijiji cha Mchauru kuna Kitongoji cha Mkowo kina watu zaidi ya 500, lakini kuna kisima pale. Vilevile kuna vitongoji vingine vya Nanganga na Rivango. Kitongoji cha Nanganga kina wananchi zaidi ya 500 na Rivango zaidi ya 500 na kuna shule ya msingi pamoja na zahanati. Hata hivyo, vitu hivi vinakosa kupata umeme na kufanya sasa utekelezaji wa mapinduzi ya kimaendeleo kuwa ni ya chini na ya kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mdavila katika Kitongoji cha Nalyongolo kuna watu zaidi ya 600, kuna ujenzi wa shule shikizi hapa. Halikadhalika kuna Kitongoji cha Mtolya kuna watu zaidi ya 400; Lipumbulu kuna Kitongoji cha Nnandembo kuna watu zaidi ya 500, Chikowedi kina zaidi ya watu 500, Umati, Lupaso watu zaidi ya 800 na kuna shule ya msingi pia. Mbuyuni pia kuna Kitongoji cha Chipindimbi kuna watu zaidi ya 400. Hawa wote ni watu ambao wamekosa umeme kwa kigezo cha kusema kwamba ni kitongoji. Kwa kweli jambo hili nafikiri tungeliangalia kwa umakini hususani katika jimbo langu. Ninaomba sasa hivi vichukuliwe kama ni vijiji, vifanywe kama kipaumbele na vipewe umeme mapema tena kabla ya kupeleka umeme katika maeneo ambayo tayari umeme upo kwa kisingizio hicho cha kitongoji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo ningetaka kulizungumzia hapa ambalo ni la msingi sana, ni jambo la Mradi wa LNG. Ningetaka kufahamu ni nini ambacho kimetokea kwenye mradi huu. Kiuhalisia mradi huu ni mradi muhimu sana hususani kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi au Mikoa ya Kusini kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia, mradi huu muhimu sana hususan katika mikoa ya Mtwara na Lindi au mikoa ya kusini kwa ujumla. Kumekuwa na hisia mara nyingi sana, watu wa mikoa ya kusini kujihisi kana kwamba mipango inayowahusu hususan inayohusiana na maendeleo imekwenda kwa kusuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na mifano mingi sana. Mfano ni huu mradi wa gesi, tangu mwanzo kipindi cha Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mradi wa gesi ulikuja ukaanza kuonekana kwamba ni mradi mkubwa ambao utakomboa mikoa ya kusini, lakini from nowhere huu mradi ulikwenda ukawa stagnant, umekaa kimya, haueleweki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Hassan, wananchi wamepata hamasa kubwa sana, wakati waliposikia kwamba miradi yao ya gesi inaanza, hususan katika mradi huu wa Likong’o wa LNG, mradi wenye thamani kubwa sana wa Dola za Kimarekani bilioni 30 ni mradi mkubwa sana, lakini sasa kumekuwa na ukimya mkubwa, lakini hatuambiwi tatizo liko wapi? Nataka tuulize Serikali, kuna jambo gani limejitokeza kwenye mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuambizane ukweli kama kuna jambo baya limetokea kwenye mradi huu, siyo vibaya tukaambiwa kwa sababu gani? Wananchi wamekuwa wakiwekeza kidogo kidogo katika eneo hili kwa pesa zao mfukoni, lakini na pesa pia kutoka benki. Pesa hizi zinapotea bure, lakini kama wangefahamu bila shaka wasingefanya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ingekuwa ni vizuri kuambiwa, kusudi tujue kwamba ni kitu gani kinatakiwa kuwaambia wananchi wanapotuuliza. Kuna wakati wanatuuliza tunakosa majibu sahihi. Sina ubaya wowote wa kusema kwamba kuna ubaya unafanyika katika hili, hapana, lakini nafikiri inatamani sana mradi uwe umetekelezwa ambapo watu wengi wa kusini wana utegemea mradi huu uwe ni chachu ya maendeleo na kuwakomboa katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu nakutegemea sana, sina shaka na wewe, utendaji wako ni wa hali ya juu, umefanya mambo makubwa sana ambayo nimeyaona kwa macho yangu, umetuletea turbine katika mkoa wa kusini ambako kulikuwa na changamoto kubwa sana ya umeme wa kukatikakatika, lakini hali kadhalika umeidhinisha mradi mkubwa sana ambao utajengwa kutoka Tunduru kuelekea Masasi, sina shaka na hilo na sasa hivi watu wanalipwa fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka mradi huu wa Likong’o Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu awekee nguvu zote watu wa mikoa ya kusini wanufaike na mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)