Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Wizara hii ambayo iko kwenye Kamati ambayo nipo. Katika Kamati ukurasa wa 15 tumetoa mapendekezo na maoni kwa Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, kabla sijaendelea, naomba nitoe pole kwa Naibu Waziri Mkuu kwa kifo cha Ndugu yetu Eng. Nyamhanga, ni kiongozi aliyekuwa makini, lakini Mungu amempenda zaidi, sisi tuliobaki kazi yetu kuiga pale alipotuachia tufanye kazi kwa uaminifu kama alivyokuwepo marehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naishukuru pia Serikali, kwa mara ya kwanza kufanikisha Mradi wa Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, suala la umeme sasa siyo tatizo tena, kilichobaki ni kuhakikisha miundombinu inatengenezwa na wananchi sasa mambo ya kukatika umeme yasiwepo tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vitongoji takribani 32,000 katika nchi nzima lakini mpaka sasa ni vitongoji 927 ambavyo vimepata umeme. Kamati pamoja nami, tunaishauri Serikali kuongeza speed. Tunatambua wameongeza muda wa kuunganisha vitongoji kwa umeme mpaka 2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba speed ya kuongeza vitongoji kupata umeme, maana huko chini ndiko kwenye wananchi. Tunaomba sana speed iongezwe sawasawa na tulivyowashauri katika ukurasa wetu wa 15. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna mikoa ambayo haijaingia kwenye gridi ya Taifa, tunashukuru Kigoma imeingia sasa katika list, kulikuwa kuna Kigoma, Katavi, Rukwa pamoja na Lindi na Mtwara. Tunaomba vilevile speed iongezeke kwa mikoa iliyobaki waweze kupata umeme, na uweze kuingizwa kwenye gridi ya Taifa kwa sababu kwa kuingiza umeme huko, basi hakutakuwa na matatizo katika mikoa hiyo tajwa nao watapata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shida kubwa sana katika Wizara. Upande wa kibajeti sisi tunategemea fedha nyingine kutoka kwa wafadhili. Kuna ndugu zetu wa IMF, waliahidi kutoa zaidi ya shilingi bilioni 52, lakini imekuwa ikionekana kwenye bajeti halafu hatujaipata. Tuombe ndugu zetu waweze kuifuatilia kwa sababu OC mpaka sasa ina 16% peke yake. Ili uweze kuwa na maendeleo, ni lazima fedha za miradi au fedha za kazi ziwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi tunaomba usimamizi wa upatikanaji wa fedha na tuombe Wizara kwa sababu kazi ya Bunge imesimama kuisemea Serikali, kuiambia, basi Wizara ya Fedha ihakikishe tunapata fedha kwa wakati kwa sababu Bunge likipitisha fedha, ni kazi ya Wizara kutoa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo ya kupata fedha nusu, 50% mnazuia watendaji wasiweze kutimiza wajibu ambao wamepewa na Serikali, kwa sababu Bunge ni chombo ambacho kina mamlaka ya kupitisha bajeti, sasa bajeti zetu tunakaa hapa miezi miwili au mitatu, tunapitisha bajeti, halafu fedha hazitoki. Hii inakuwa siyo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Shirika letu la TANOIL. Hili Shirika kiukweli lina umuhimu kwa sababu Serikali isipokuwa na chombo cha kusimamia mafuta na kuhifadhi chenyewe inakuwa siyo sawa na kuwa na makampuni binafsi kunaweza kukatokea hujuma mbalimbali, lakini shirika hili limekuwa lina deni kubwa sana zaidi ya shilingi bilioni 21. Ukusanyaji wa madeni kutoka TANOIL unaenda kwa kusuasua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namfahamu Mheshimiwa Waziri, weledi wa kazi alionao, fanya utaratibu mahususi kabisa wa kuhakikisha fedha zetu zaidi ya shilingi bilioni 21 ziko nje ya mfuko wa Serikali, zirudishwe haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ripoti inasema ni asilimai ndogo sana kama 6.8 ambayo tumekusanya ambayo ni shilingi bilioni 1.43. Hiyo ni hela ndogo sana. Tunaomba ufanyike utaratibu wa makusudi kuhakikisha Shirika hili linakusanya shilingi bilioni 21 ambazo ni pesa nyingi zinazohitajika kwenye Bajeti ya Mfuko wa Serikali na kwenye Wizara husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana suala la gharama za umeme. Tunajua kuna umeme wa REA ambao vijijini wanajiandikisha kwa shilingi 27,000, lakini umeme huo huo kuna sehemu nyingine zinasema, ikiwa ni mita 30, hiyo shilingi 27,000; ikiwa mita 70 ni shilingi 515,000, hiyo different ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tutoe matabaka kati ya vijijini pamoja na mijini. Tunafahamu kwamba wakati mwingine ni pesa za miradi makusudi kusaidia wananchi wa vijijini kupata umeme, lakini ambaye anapita kwa mita 120 analipa shilingi 696,000. Wananchi kule chini wanaona kama ni tabaka kubwa sana. Basi tuna kazi kubwa sana, kama tunakuwa tunataka ibaki kama ilivyo, tuweke elimu kubwa sana ya wananchi waweze kuelewa, kwa nini huyu analipa shilingi 27,000, na huyu analipa shilingi 320,000 na mwingine analipa kiasi kingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba tutoe elimu kitengo kinachohusika, basi kitoe elimu kuliko kutokusema inaleta lawama kwa wananchi. Pia kama Kamati, tunafikiri tukiweka angalau tukapandisha hiyo shilingi 27,000 na tushushe ile ya shilingi 500,000 na angalau hapo katikati tuweze kuona wananchi wetu wote wako katika tabaka moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kabisa matumizi ya nishati safi. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais ameweza kusimamia hili na tumeona jinsi ambavyo wananchi wameanza kuelewa matumizi ya nishati safi. Tunafahamu kabisa majiko ya gesi ambayo mengine tuligawa, kama sisi wasimamizi wa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wametoa majiko ya gesi ya ruzuku ambayo yamemsaidia mwananchi wa kijijini kutokununua hiyo gesi kwa shilingi 48,000 kwenda kununua kwa shilingi 20,000 na maeneo mengine imeshuka hadi shilingi 18,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mahitaji ni makubwa, tayari tumeshafanya elimu kwa wananchi, na wako tayari kutumia nishati safi, lakini bado tunahitaji kuongeza idadi ya majiko haya ili yaweze kufika kijijini kwa watu wote. Nafahamu katika Wilaya ya Rungwe tulipata tu kiasi cha majiko 3,000. Kwa hiyo, yanakuwa siyo mengi. Kama siyo 300,000, sorry.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana tuongezewe majiko na yapelekwe kwa kutumia Wizara na kwa kusimamiwa na Wakuu wa Wilaya ili watu wetu waweze kuendeleza pale walipoishia, lakini mwisho wa siku bado elimu inahitajika, zile gesi zikiisha wengine wanatupa yale mitungi na watu wabaya wasioitakia mema nchi yetu, wanauza kama vyuma chakavu. Kuna haja ya kuweka ukali zaidi na ulinzi kuhakikisha tunalinda rasilimali hizi za Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kasi ya kuongeza umeme vitongojini, nimeshasema, lakini mwisho wa siku tunahitaji kusaidia maeneo ambayo ni ya kimsingi. Kwa mfano, vijijini wanahitaji mashine za kusaga kwa ajili ya pampu za maji, basi tuwekeze maeneo yale kama speed hiyo ni ndogo, lakini pale tunaita center za vijiji tuhakikishe tunaweka umeme angalau kusaidia jamii kwa ujumla wake kwa sababu kukiwa kuna mashine ya kusaga, kukawa kuna pampu ya maji au shuleni na vitu kama hivyo, tunaomba tuongezewe nguvu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naamini kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati wanayo kazi kubwa sana na wamefanya kazi kubwa sana, basi hapa ambapo wameishia kwenye bajeti hii tunaomba wasimamie haya ambayo tumeyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, naunga mkono hoja bajeti hii kwa sababu kule kijijini wanahitaji umeme na tunahitaji kuwapitishia fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nashukuru sana. (Makofi)