Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Morogoro Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia hoja ambayo iko mbele yetu. Nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa matamanio yake makubwa ya kutaka kuifanya Tanzania iendelee kung’ara na kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mafanikio makubwa kwenye SGR, tumeona mafanikio makubwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo limo katika Wizara hii ambayo nataka kuizungumzia, na pia tumeona mafanikio makubwa kwenye Daraja la Kigongo Busisi, kwenye afya, shule na mambo kadha wa kadha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais, japokuwa kuna wenzetu wengine wanasema kwa nini tunampongeza Rais? Wabunge tunajua jitihada ambazo amezifanya Mama huyu kwa Watanzania katika majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii vilevile kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, lakini msaidizi wake Advocate Kapinga na watendaji wote wa Wizara na taasisi zilizokuwa chini ya Wizara. Kiuhalisia, hakika wanamsaidia Mama katika suala la umeme na mambo mengine yanayohusu Wizara hii, tuna kila sababu ya kuwapongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawapongeza Mameneja wa Mikoa wa TANESCO, na vilevile Meneja wangu wa Mkoa wa Morogoro, Engineer Fadhili, pamoja na Meneja wangu wa Wilaya ya Morogoro vijijini, ndugu yangu Oswald kwa kazi kubwa ambayo anaifanya katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi, nami niende kwenye suala la kuchangia. Nianze na kuchangia kwenye suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tuna kila sababu ya kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa. Mama wakati anachukua Madaraka, bwawa hili lilikuwa kwenye 14% au 15% hadi 16%, lakini leo tunaambiwa limekamilika, na bwawa hili liko kwenye Jimbo la Morogoro Kusini na Jimbo la Rufiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni uhalisia kwamba limekamilika mashine zote tisa zinafanya kazi na umeme umeingia kwenye gridi ya Taifa. Kwa kuingia kwenye gridi ya Taifa, maana yake nini? Tumeongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika Taifa letu, lakini vilevile kuna ongezeko la umeme kwenye gridi ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kukupongeza Mheshimiwa Dkt. Dotto Biteko kwa kazi kubwa ambayo umemsaidia mama, kiuhalisia umefanya mambo makubwa na Taifa litakukumbuka katika kipindi ambacho umeongoza Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio kwenye hili suala la Bwawa la Mwalimu Nyerere, sisi Wanamorogoro na Wanapwani, nitaendelea kusema sitaweza kuliacha hili mpaka Serikali itupe majibu. Bwawa limekamilika, kuna suala la CSR ambayo CSR hiyo mimi toka naingia Bungeni naisema kila siku, lakini Serikali mnatuambia tutakaa Wanamorogoro, Wanapwani na tutatoka na majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kaka yangu, mdogo wangu wakati anapokuja kutoa majibu ya hoja ambazo zimewasilishwa na Wabunge, hebu naomba utupe majibu Wanamorogoro na Wanapwani, lini haki yetu hii ya CSR tutaipata? Sisi Wabunge tunakwenda kwenye uchaguzi, wananchi wetu watatuuliza maswali kuhusu suala hili, tunaomba utusaidie, utupatie majibu tukawaambie wananchi wetu (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani, na naachilia, naogopa kushika shilingi yake na kuheshimu sana, lakini napenda nishike shilingi ili kusudi nipate majibu yaliyokuwa sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kuna suala tuliambiwa Wanamorogoro na Wanapwani tungepewa shilingi bilioni kumi kumi, sisi kwenye Halmashauri yetu tulizipangia mpaka matumizi, lakini tunapozungumza mpaka leo hakuna fedha hiyo. Nini hatma ya fedha hiyo walau itangulie wananchi wetu waweze kupata matokeo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza jambo hilo, nizungumzie kwenye suala la REA. Tuna kila sababu ya kumpongeza Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini kumpongeza yeye mwenyewe binafsi Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na wasaidizi wake. Pia kipekee sana, nampongeza Mtendaji Mkuu wa REA Eng. Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika kuhakikisha nchi nzima inawaka umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu Morogoro Kusini nina kata 17, katika kata 17 nina vijiji 85, vitongoji 437. Leo tunapozungumza, kata 17 zote zinawaka umeme katika vijiji 85. Wakati tunaingia kwenye Bunge hili na kwa awamu yangu ya pili, vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa ni 36 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo vijiji 85 vyote vinawaka umeme na kiuhalisia kazi kubwa iliyofanywa na REA, kazi kubwa iliyofanywa na Wizara na kazi kubwa ya kutoa fedha aliyotoa Mama, Jimbo langu katika kata 17, kata tisa ziko milimani na huko milimani kutoka makao makuu ya barabara kuu kwenda kwenye makao makuu ya kata ndiyo kuna barabara, lakini kwingine kote ni milimani; mfano Rongwe, Ukwama, Kumba, Mgata, Bwakila Juu, Kigajila kote, Nyamila yenyewe ni milimani, lakini umeme unawaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kumpongeza Mama, lakini tunampongeza Mheshimiwa Waziri kama msaidizi wake Mama kwenye sekta ya nishati, lakini na Mtendaji Mkuu wa REA na watumishi wote wa REA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu bado katika vitongoji 437, vitongoji vyenye umeme ni 191. Pia kuna vitongoji 15 vya jimbo tulivyopewa kwa Wabunge wote, bado havijafanyiwa kazi, lakini nashukuru na ninapongeza katika mgao ambao umetoka tayari nimepata vitongoji vingine 90 ambavyo vitaenda kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, vitongoji 121 vilivyobakia vifanyiwe kazi na wananchi hawa wapate umeme kwa sababu wana uhitaji sana wa umeme kwa maslahi mapana na matumizi kwa faida ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mafanikio hayo, kuna suala la Shule ya Sekondari ya Kolelo. Tulizungumza kwamba umeme ufike kwenye taasisi na umeme kwenye Sekondari ya Kolelo, haujafika. Nilizungumza na Eng. Cecila ambaye ni Mhandisi wa REA Mkoa wa Morogoro, amekwenda kuangalia na ameleta mahitaji kwenye REA Makao Makuu. Ombi langu, tuwapelekee umeme watu hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa ni ombi kuzungumzia suala la substation. Umeme katika Halmashauri ya Morogoro Vijijini unakatikakatika, unatoka kwa kupitia Chalinze unatoka kwa kupitia Morogoro na hii ni kwa sababu hatuna substation ya kupoza umeme matokeo yote yanayojitokeza Halmashauri nzima inakwenda kuwa giza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, tunakoenda tuangalie jinsi gani tunaweza kufanya ili kusudi tupate substation kwenye eneo la Lukurunge kwa sababu watu wa TANESCO walikuwa wanasema wameshafanya feasibility study zao mara mbili lakini wanasubiri pesa, na pesa ikipatikana tutafanya jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niipongeze Serikali kwa kukamilika kwa kituo cha kupoza umeme cha Msamvu ambacho kinalisha karibu Morogoro yote. Tulikuwa na changamoto kubwa sana katika kipindi kilichokwisha lakini sasa hivi katika katika ya umeme kwa Morogoro tumekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi katika hili suala la kuhitaji substation kwa Morogoro, Morogoro vijijini sasa hivi hasa kwenye Kata ya Bwakila Chini, kwenye Kata ya Rundi kuna viwanda vikubwa vya uchenjuaji wa madini ya graphite. Sasa kama tutapata substation, tutashawishi wawekezaji wengine wengi wakajitokeza na wananchi wetu wakaendelea kupata maendeleo makubwa na uchumi kwa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, naendelea kuipongeza TANESCO, katika bajeti ya mwaka 2024 nilizungumzia suala la Mkoa wa Morogoro kwamba ni mkoa wa kimkakati; una vyanzo vitatu vya maji: kuna Kihansi, Kidatu na hili Bwawa la Mwalimu Nyerere. Mkoa wa Mororgoro ni mkubwa, nilizungumzia suala la magari na ninashukuru Meneja wangu wa TANESCO wa Wilaya amepata gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nilizungumzia suala la Ofisi ya Meneja wa TANESCO katika Halmashauri yetu ya Morogoro Vijijini ambayo mpaka sasa bado. Meneja yule anakaa kwenye kontena. Mheshimiwa Waziri hebu angalia kupitia TANESCO tumjengee nyumba yule ili aweze kufanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ambayo iko mbele yetu. Nashukuru sana. (Makofi)