Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru kwa nafasi uliyonipatia kuchangia katika bajeti yetu hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza kabisa, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo imefanyika ndani ya kipindi hiki ambacho sisi sote ni mashahidi tunaona kuongezeka kwa kuweka miundombinu ya umeme katika maeneo yetu na ni ushuhuda tosha kwamba katika vijiji vyote 12,318 umeme umeweza kufika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumeona ongezeko la uzalishaji wa umeme katika nchi yetu kufikia Megawatts 4,031. Kwa kweli ni mapinduzi makubwa ya kinishati ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi kwa Mheshimiwa Rais ambaye ni mbeba maono wa nchi yetu, niendelee kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, kaka yetu Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko kwa kuliongoza jahazi hili la Wizara ya Nishati kwa ufanisi mkubwa na tunaona mabadiliko makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko anao wasaidizi wake; tunamwona Mheshimiwa Judith Kapinga ambaye amekuwa msaidizi wake mahiri sana. Pia, Watendaji Wakuu wa Wizara hii akitangulia Katibu Mkuu, kaka yetu Felchesmi Mramba; tunawaona Naibu Makatibu wakuu wote: Dkt. Mataragio na Dkt. Khatibu Kazungu, pia, watendaji wakuu wa taasisi zote ambazo zinasimamia maeneo haya tukianza na kiongozi wa TANESCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, tutoe pole kwa kuondokewa na DG na tumpongeze DG wa REA ndugu yetu Eng. Hassan ambaye naye amekuwa akifanya kazi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi hawa wanafanya kazi na viongozi wetu wa mikoa. Tunao Mameneja wa TANESCO mikoa yote wakiongozwa na Meneja wa Mkoa wa Kagera na Mameneja wetu wa wilaya. Mimi mahususi nampongeza Meneja wangu wa Wilaya Bwana Peter Masanja kwa kazi kubwa pamoja na watumishi wote ndani ya Wizara ya Nishati, Taasisi zetu za REA, na TANESCO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika maeneo manne. Kwanza, pongezi ambayo imekamilika, lakini pia nitoe shukrani kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Missenyi. Pia, nitakuwa na changamoto ambazo zinawakabili wananchi wa Missenyi na mwisho nitakuwa na maombi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la shukrani, kama ambavyo tumeendelea kuona nchini, katika vijiji vyote 77 ndani ya Wilaya ya Missenyi kwa sasa hivi vyote vina umeme. Ni pongezi na shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Rais na kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye kwa kweli amekuwa ni (pioneer) rubani mzuri katika Wizara yetu hii ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona Wilaya ya Missenyi ina vitongoji 356. Katika maeneo hayo yote, vitongoji 184 sasa hivi vina umeme na kwa sasa hivi kazi inaendelea kwa kasi kubwa katika vitongoji 26. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Wilaya ya Missenyi kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na kiongozi wetu katika Wizara hii ambaye ameaminiwa na Mheshimiwa Rais kushika usukani wa Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaendelea kushukuru kwa umeme sasa hivi katika vitongoji 15 unaendelea kufungwa. Nguzo zimeshaletwa kupitia kampuni ya CCC na tunaona kazi inaendelea. Kwa hiyo, tunaipongeza Serikali yetu na imekuwa ni historia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo ambayo umeme ulipita juu ya vitongoji hivi kwenda maeneo mengine kwa miaka takribani 10, lakini vitongoji hivyo vilikuwa havina umeme. Chini ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan sasa tukiangalia vitongoji vya Nyungwe, Kakoni na maeneo mengine na vyenyewe viko katika orodha ya kufungiwa umeme. Nguzo zimeshashushwa katika maeneo hayo na wananchi wana matarajio makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo letu kwa kweli tunaendelea kuipongeza Serikali. Historia imeandikwa, sasa hivi watu maeneo mengi wanapata mwanga kupitia umeme wetu na wanautumia katika shughuli za kiuchumi ikiwemo katika uzalishaji na maeneo mengine ya viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo letu pamoja na mazuri haya yote ambayo yamefanyika, lakini bado tunazo changamoto moja mbili tatu ambazo ninaamini ziko ndani ya uwezo wa Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuzitatua na zikaleta afueni kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza Mheshimiwa Waziri wetu wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu ni fidia ya wananchi wa Mradi wa Kakono. Tunajua kwamba Serikali imefanya kazi kubwa kuendelea kuzalisha umeme na mojawapo ya watu ambao waliathirika na eneo hili ni wananchi wa Wilaya ya Missenyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wananchi wote ambao wako katika mkondo wa Mradi wa Kakono waweze kupewa fidia. Mwaka 2024 nilisimama hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kuomba wananchi waweze kulipwa na Mheshimiwa Waziri wa Nishati alijibu kwamba Serikali imeshaainisha mahitaji ya wananchi hao na wanadai takribani shilingi bilioni 1.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa ruhusa yako naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, wakati anahitimisha angalau wananchi wa Missenyi waweze kusikia hii fidia ya 1.6 billion kwa wananchi ambao wako katika fidia ya Mradi wa Kakono italipwa lini kwa sababu mwaka 2024 tulisema mwezi wa Saba wangelipwa, lakini mpaka sasa hivi wanasubiria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sababu wana imani na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ninaamini tutakuja kupata majibu mazuri ili wananchi hawa waweze kupewa fidia hiyo na waendelee na shughuli nyingine za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Wabunge wengine ambao wamesema maeneo mengine umeme unakatika. Hata hivyo, naamini kwa Wilaya ya Missenyi inawezekana umeme unakatika kuliko maeneo mengine yote, na ni kwa sababu Wilaya ya Missenyi na Mkoa wa Kagera kwa ujumla tumebarikiwa kuwa na mvua nyingi. Sasa hizo mvua zisiwe zinaleta athari kubwa, tuone jinsi gani ambavyo Serikali imejipanga. Pamoja na kupata mvua nyingi, isiwe ni sababu ya wananchi hao kupata adha ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia sana eneo hili. Ukifuatilia kwa wataalamu, wanasema ni vegetation kwamba miti inakua sana na migomba inakua chini ya waya, lakini ninaamini ule urefu wa mgomba hauwezi kufika hata nusu ya ule urefu ambao nyaya zetu zinakuwa zimefungwa. Pia, wanasema sababu ni vidhibiti radi; naomba kupitia Wizara hii ambayo iko makini chini ya Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko iweze kuja na suluhisho kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera na mahususi Wilaya ya Missenyi ambako umeme kwa kweli unakatika mara kwa mara na hasa kwa sababu tuna mvua nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona umeme unaendelea kukatika kila mvua ikitaka kunyesha, wataalamu wanakata umeme mapema ili kunusuru uharibifu wa miundombinu zaidi. Sasa tuwe na suluhisho la kudumu ili sasa wananchi hawa ambao wanaendelea kupata baraka ya mvua basi na umeme waendelee kuupata katika kipindi chote, hata kama mvua inanyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana katika eneo hili ambalo limekuwa ni changamoto, umeme upo katika maeneo ambayo umeshafika, lakini sasa wananchi waweze kusaidiwa na changamoto hii ya kukatika kwa umeme kuondoa uharibifu wa mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niendelee kuomba, pamoja na kazi kubwa ambayo inafanyika Serikalini ambayo imeendelea kusambaza umeme na mtandao, umeendelea kuongezeka, lazima kuwe na uhitaji wa rasilimaliwatu na vitendeakazi. Hili inawezekana likawa ni hitaji la nchi nzima. Naomba uangalie kwamba rasilimali za wataalamu katika maeneo yetu ni muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Missenyi sasa hivi ina takribani wataalamu 10, lakini tunaona mtandao umeendelea kuongezeka. Kwa hiyo, tunaomba sasa mambo mazuri ya kuendeleza mtandao wa umeme kuongezeka, basi iende sambamba na kuongeza wataalamu ili kazi mahususi iweze kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba, tuna mahitaji ya gari katika Wilaya ya Missenyi ambayo ina gari tatu zilizochakaa ili iweze kuwasaidia wataalamu wetu waweze kufanya kazi kwa weledi na kuwafikia wananchi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la nne ni suala la bajeti. Wilaya ya Missenyi kuna baadhi ya maeneo yanapata umeme katika line inayotoka wilaya nyingine. Kwa mfano, katika kata zetu za Kashenye na Kanyigo, zinapata umeme kutoka wilaya nyingine ambayo Wilaya ya Bukoba, lakini usimamizi wa technical support yote inafanyika ndani ya Wilaya ya Missenyi. Wakati mwingine kuna mkanganyiko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua maendeleo ni hatua, lakini naomba itoshe kusema kwamba Wizara iangalie ni namna gani ya kuweza kutupatia bajeti ya kujenga line ya umeme ambayo itatoka Kyaka pale ambapo kuna substation ndani ya Wilaya yetu ili na usimamizi uwe ni mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba tena, tunacho Kiwanda cha Kagera Sugar, kinafanya kazi nzuri. Tunaomba kipate dedicated line yake kama kiwanda ili sasa ule umeme ambao unaenda kwenye kiwanda na unatumika kwa wananchi, basi kiwanda kiweze kuwa na line yake mahususi kuendelea kutekeleza kazi yake ambayo inafanyika vizuri. Pia, na wananchi waweze kuwa na line yao ili kuondoa ile kunapokuwa na hitilafu kiwandani na wananchi wanaathirika au kunapokuwa na hitilafu kwa wananchi na kiwanda kinaathirika. Hii itasaidia sana kuwasaidia wananchi wetu wa Wilaya ya Missenyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lingine ni vitongoji 172 vilivyobaki. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati katika eneo letu la Missenyi analifahamu. Katika huu mradi wa vitongoji 30,000 vilivyobaki, basi naomba Wilaya ya Missenyi ipewe kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hivi vitongoji 172 vilivyobaki viweze kufikiwa na hao wananchi waendelee kufaidi matunda mazuri ya Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na hii inaenda sambamba na majazilizo katika vitongoji ambavyo vingine vimeshapata umeme, lakini umeme huo umeenda katika nyumba chache. Kwa hiyo, naomba sana tuweze kuyafikia maeneo yote ili wananchi hao waweze kufaidi nishati ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu lingine ni gharama za kuunganisha umeme. Wilaya ya Missenyi katika maeneo ya vijiji vyote 77 bado ina taswira ya vijiji na ndiyo usajili wake kwa mujibu wa sheria. Tukiangalia Sheria ya 282 ya Serikali za Mitaa bado vimesajiliwa kama vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba ule utaratibu uliotumika kuainisha maeneo yaliyochangamka kidogo yamepita maduka saba au 10 yamechangamka na wakati mwingine lami imepita ikaonekana kwamba haya maeneo wananchi hawa wanaweza wakaunganisha umeme kwa shilingi 352,000/=. Naomba tufanye marejeo kwa sababu wananchi wa Missenyi bado wote wako katika vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii shilingi 27,000 ndiyo itumike katika maeneo yetu ambayo wananchi wanaweza kumudu kuliko maeneo mengine ambayo kidogo unaona umeme umepita pale na barabara ya lami imepita halafu wanasema kwamba eneo hili sasa ni eneo ambalo linalipa shilingi 352,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nakushukuru kwa nafasi, lakini naomba changamoto ambazo zimefanyika katika REA Na.1 na Na. 2 ndani ya Jimbo letu ziweze kusahihishwa katika mradi unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nashukuru kwa nafasi, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)