Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi leo ya kuweza kuchangia kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia afya hata leo nimeweza kusimama hapa kuchangia kwenye hotuba hii ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu kipenzi Mama Jemedari, Mama wa Shoka, Mwanamke Chuma, kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya ya kutuletea maendeleo kwenye nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu ya mema aliyotutendea Wanamsalala. Mimi kama mwakilishi wa wananchi wa Jimbo la Msalala, ndiye shahidi namba moja ambaye ninatoa ushahidi na ushuhuda wa mambo mazuri ambayo ameyafanya kwenye Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Nishati kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuwa shahidi wakati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anamteua Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko aliteuliwa wakati wa msukosuko mkubwa sana ndani ya Shirika la TANESCO, umeme ukiwa unakatikakatika, na kulikuwa kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuteuliwa kama alivyosema kaka yangu Olelekaita hapa KNK (Kusema na Kutenda), alikaa chini na kufikiria ni namna gani anaweza akatatua tatizo la upatikanaji wa mafuta kwa bei nafuu ambayo itamsaidia Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa tunavyozungumza habari ya mafuta imekuwa ni historia. Sasa upatikanaji wa mafuta kwenye nchi yetu uko salama na jambo limetulia kabisa na hakuna changamoto yoyote ile kwenye suala zima la mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo, kwenye suala zima la umeme na penyewe ameweza kuona ni namna gani anaweza kutatua changamoto ya kukatikakatika kwa umeme akielekeza nguvu kazi kubwa sana katika kuhakikisha ya kwamba kuna uzalishaji, usambazaji na uuzaji umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo la Msalala tulikuwa na upungufu wa umeme takribani vijiji 64, lakini leo hii tunavyozungumza, kwenye Jimbo la Msalala lenye kata 18 na vijiji 92 upatikanaji wa umeme kwenye vijiji vyote, tayari umefika na wananchi sasa wanatumia huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mkurugenzi Mkuu wa REA, kaka yangu Hassan; nampongeza pia Katibu Mkuu kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kuifanya. Kazi kubwa mliyoifanya REA kwenye Jimbo langu la Msalala, wananchi wamenituma niwaletee shukrani zao za dhati kabisa, wanawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, kwani Wanakahama tulipompelekea ombi la namna gani tunapata changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma, aliridhia ombi letu la kuhakikisha kwamba anaifanya Wilaya ya Kahama kuwa Mkoa wa Ki-TANESCO, na hivyo sasa kupelekea halmashauri zetu ikiwemo Halmashauri ya Msalala kuwa ni wilaya za Ki-TANESCO kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na nina imani ananisikiliza vizuri sana. Mheshimiwa tunakupongeza sana, tayari Meneja wa Wilaya wa TANESCO kwenye Halmashauri ya Msalala amesharipoti kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba, changamoto iliyopo kwa sasa, kwa sababu tayari tumepata wilaya, na kama unavyofahamu, na ninampongeza sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, kwani aliweza kutenga eneo la kujenga Ofisi ya Wilaya ya Ki-TANESCO kwenye Jimbo la Msalala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwamba, tayari mimi kama Mbunge niko tayari kuchangia tofali na niliahidi tofali 5,000 tuweke hapo site na eneo lipo. Sasa naomba atakapohitimisha hapa kwa moyo wake ule ule ambao alitusaidia kupata Mkoa wa Ki-TANESCO na Wilaya za Ki-TANESCO aende sasa kutusaidia tupate fungu kidogo ili tuanze ujenzi wa ofisi ya Meneja huyu wa TANESCO ili aweze kupata ofisi ya kufanya shughuli zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Meneja huyu ameripoti, lakini hana usafiri. Naomba sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, chonde chonde kwa udharura wake, naomba tupatiwe gari ambalo Meneja huyu litamrahisishia kutembea kwenye vijiji vyetu na kwenye maeneo hayo ya Jimbo la Msalala. Naomba sana, kilio chetu kwa sasa ni gari la kumwezesha Meneja kutembelea maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nishauri jambo kwenye suala zima la usambazaji umeme. REA wanafanya kazi nzuri sana ya kupeleka na kuunganisha umeme, lakini mtandao ambao wanaunganisha ni mdogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia sasa watu wa TANESCO kwenda kuhakikisha ya kwamba wanatoa elimu kwa wananchi namna ya kuvuta umeme kwenye nyumba zao ili wananchi sasa waweze kutumia haki yao ya msingi ya kuvuta umeme kwenye nyumba zao, kwani kwenye maeneo mengi REA wanapokamilisha mradi wanaondoka, kunakuwa hakuna mtu mwingine kwa ajili ya mwendelezo wa kwenda kutoa elimu ili wananchi hao waweze kuvutiwa umeme kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuweze kuboresha sasa huduma bora itakayotolewa na watu wa TANESCO itakayoenda vijijini kutoa elimu namna ya kuweza kulipia. Kama unavyofahamu Mheshimiwa Naibu Waziri nawapongeza sana, wameanzisha huduma ya NIKONEKT kwenye mtandao, lakini sasa kwenye maeneo yetu kama unavyofahamu Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, asilimia kubwa ya maeneo yetu wananchi hawawezi kutumia hizi simu za kiganjani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanahitaji sana kupata elimu na wanahitaji watu wa TANESCO waweze kutenga muda kuwafikia wananchi kwenye maeneo hayo ili waweze kuwasaidia kujaza fomu na kuwasaidia kuwapa namna ya kuwaonesha wananchi waweze kutumia haki yao ya kuvuta umeme kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, kazi aliyoifanya kwenye Jimbo la Msalala kwenye umeme ni kubwa mno. Nafahamu tayari tumeshapitisha bajeti ya kwenda kupeleka umeme kwenye vitongoji na baadhi ya vitongoji bado umeme haujafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini na ni matumaini yangu makubwa juu ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu katika kuhakikisha kwamba baada ya bajeti hii (na niseme tu ninaunga mkono bajeti hii kwa asilimia mia moja), sasa kazi ya kwenda kuwapelekea wananchi umeme kwenye vitongoji vyetu iweze kufanyika kwa umahiri mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri ikimpendeza, siyo mbaya akatoa maelekezo wakaanzia kwenye Jimbo la Msalala ili waweze kusambaza umeme kwenye vitongoji hivyo kwa sababu kama unavyofahamu sisi ni wazalishaji wa madini na ni wakulima kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji umeme ili tuweze kutumia umeme huu kwenye shughuli zetu za uzalishaji madini. Tunahitaji huduma ya umeme ili tuweze kutumia kwenye umwagiliaji na kwenye kuchakata mazao kwenye maeneo yetu haya ya Msalala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na ninampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kazi kubwa. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, endelea kupambana, tuna imani kubwa na wewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)