Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii muhimu mchana huu katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuungana na Wabunge wenzangu wote kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake kwa nchi yetu, na sisi Watanzania wote, yote hayo ni kwa mipango yake, nchi ni salama, tuna amani, upendo na mshikamano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa nchi nzima pia kwa Jimbo la Mbulu Mjini. Kwa kweli pamoja na Serikali nzima ya Awamu ya Sita, tunampongeza, tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Rais na Serikali nzima, pia wananchi wa Mbulu tunaahidi kumlipa kwa fadhila na utendaji uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwanza, ni msikivu, pia kila unachomweleza kinaenda kutekelezwa na ikishindikana anakupa mrejesho kwamba hii imekuwa na wakati mgumu tuitafutie wakati ujao kwenye mipango yetu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Mjini kwa niaba yao pia nitoe pole nyingi kwa msiba wa Mtendaji Mkuu wa TANESCO pia na Watanzania wote waliotangulia mbele za haki, Mwenyezi Mungu awapokee kwenye ufalme wake wa milele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee hali halisi ya sura ya Jimbo la Mbulu Mjini. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, unisikilize rafiki yangu, kwa kweli Mbulu Mjini ina jiografia ya aina yake. Mimi natoka Jimbo la Mbulu Mjini, lakini napakana na Halmashauri nne. Napaka na Karatu, Mbulu Vijijini, Babati Vijijini, pamoja na sehemu kidogo ya Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, eneo langu nusu au karibu 80% ni sura ya vijiji. Katika mitaa 58 ukitafuta mji wenye uhalisia, inaweza kuwa pengine kama 20% tu ya katikati ya mji lakini hutashangaa ukitoka kilomita moja tu kutoka Mjini unakuta nyumba nyingi hazina umeme. Hii ni kwamba, jitihada kubwa zilichukuliwa, vijiji vyote sasa hivi vimeunganishwa na umeme, lakini sehemu iliyoguswa na umeme kwa maana ya wanufaika ni kidogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maombi yangu kwa eneo hili? Kwanza, ni kama alivyoniahidi Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwamba, atarudia kuona upya na wataalam kuangalia sura ya Mji wa Mbulu na mitaa yake, basi timu yake iendelee kufanya ile kazi tuliyokubaliana, ili walau eneo kubwa la Mbulu Mjini lirudishwe kwenye gharama ya shilingi 27,000/= na pia sura ya Vijiji kwa nchi nzima kwa sababu unaweza kukuta umeme umefika pengine kwa miaka kumi, miaka nane, miaka saba katika eneo la Kijiji, lakini wanufaika ni kaya 20 ama 30. Hali hii inafanya wanufaika wanakuwa wachache na Serikali imetumia gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama nchi na kama Wizara, tunawaomba tuangalie namna ya motisha ama mpango kabambe wa uingizaji wa umeme katika maeneo yote ambayo yanahitaji ujazilishi kama ilivyo Jimbo la Mbulu Mjini. Nakushukuru kwa sababu maeneo mengi toka tulivyozungumza kwenye bajeti ile ya mwaka 2024, tumepata vitongoji 15 vimesambazwa umeme, japokuwa baadhi ya maeneo, kaya ziko chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba tu kusema kwamba, safari ya kupeleka umeme kwenye vitongoji na vijiji isingefanikiwa bila mpango mkubwa wa Kitaifa wa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa lazima tutambue jitihada za waasisi wa nchi yetu walioanzisha wazo hili la ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, pia sasa na ambaye ametekeleza maono haya, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na sasa umeme unapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia eneo lingine ambalo ni muhimu kama nchi. Eneo hili ni la utafiti wa kuongeza vyanzo vya umeme. Tukitegemea asilimia kubwa ya vyanzo vya umeme wa maji, huwezi kujua tabianchi inaweza ikatubadilishia hali kiasi gani baadaye kwa maana ya ukosefu wa mvua na mabwawa yakashindwa kuzalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunapozungumza umeme kila kitongoji, umeme kila kaya, umeme kwenye viwanda, hali hii baada ya miaka kumi wataalam watazame ikoje? Je, mahitaji ya wakati huo yatakuwaje kwa jinsi ambavyo umeme tulionao tutautumia na utakidhi haja ya matumizi ya nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nizungumze eneo lingine la miradi hii ya REA. Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ni msikivu sana. Kwenye eneo hili la REA miradi hii haina uwazi sana kwa wananchi. Kijiji kinapelekewa mradi kwa mfano nchi nzima kama ilivyo vijiji vyetu, Mbunge hawezi kujua mradi huu ni wa muda gani? Utakuwa una walengwa wangapi kwenye matarajio? Thamani ya mradi na mwajiri ni nani? Pia mtekelezaji ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaweza kwenda ofisi ya DC, wakaenda pengine site tu wakafanya kazi zao, lakini wananchi wanauliza maswali mengi. Ndiyo hali inayopelekea katika kijiji ambako umeme umepelekwa unakuta waliounganishiwa umeme pengine ni wananchi kumi ama 20, kumbe mradi ule ungeweza ku-cover wananchi pengine 40 ama 50. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii inaifanya miradi kutokuwa na tija. Pia wale wapokea mradi kama wazawa hawatafahamu mradi wao, kwa sababu ni kodi ya Watanzania na fedha za Watanzania, mfumo huu ubadilishwe. Waheshimiwa Wabunge, wafahamu mradi uliopo kwenye eneo lake, ni wa gharama gani? Unalenga walengwa wangapi? Wa thamani gani? Kwa sababu fedha bado ni za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kwamba, mara nyingi wakandarasi wanalalamika, kwa mfano, Mbulu Mjini tuna vijiji 34 vyote vimeunganishwa umeme na vyote vimewashwa pengine nyumba tano, kumi lakini unakuta upelekaji ule wa kuingiza umeme kwa shilingi 27,000 unasuasua. Yawezekana wakandarasi hawakulipwa ama pengine usimamizi siyo mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama inawezekana, tufanye tathmini ya wale tuliowapa kazi mradi huu wa kupeleka umeme kwenye vijiji, kupeleka umeme kwenye vitongoji, kupeleka umeme wa ujazilishaji umeleta tija kwa kiasi gani katika mafanikio yaliyotarajiwa? Hii itasaidia walau wale wote wanaotarajia kupata umeme na wale ambao wamepewa hiyo miradi watekeleze miradi kwa wakati, lakini kwa manufaa ambayo yametarajiwa kwa lengo kuu la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutake tusitake, taasisi nyingi bado zinahitaji umeme. Shule za sekondari, shule za msingi, tuseme sekta ya elimu kwa maana ya taasisi za elimu, makanisa na maeneo mengine ya huduma katika maeneo mbalimbali watu wanaotegemea visima vya maji, kwa maana ya visima vilivyochimbwa, zahanati pamoja na maeneo mengine ambayo kwa namna moja au nyingine wananchi wanapokea huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, tathmini ikifanyika, yale yasiingizwe kwenye vitongoji; yaingizwe kama mradi kabambe wa kuingiza taasisi hizo kupata umeme na kwenye mradi wa uhakika, kwa sababu taasisi hizo zinaweza kuwa za mashine za kusaga, uzalishaji ni mkubwa, unaweza kuleta tija kwenye mapato pia na unaweza kuwa ni huduma nzuri kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwamba, mara nyingi wale wakandarasi wakija wanakuta vitongoji tulivyoomba tayari vimeguswa na umeme, nasi tulishapendekeza. Sasa nashauri kwamba kama inawezekana, maombi ya Wabunge na maoni ya Wabunge yasikilizwe. Je, kwa kuwa kitongoji chako hiki tayari kina umeme, mradi wake ni wa ujazilizi, huu mradi ambao ni wa kufikisha umeme kwenye kitongoji, tunaomba maoni yako ili walau kitongoji gani sasa kwa maoni yako kina tija na sisi tukienda tutatambua ili kuona majengo yaliyo pamoja na maeneo ambayo yana tija kama nchi, hii itasaidia sana katika kuleta tija na manufaa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la mwisho ni kwamba, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu najua amebanwa sana, ana kazi nyingi. Aliahidi kwenda Mbulu, lakini haikuwezekana, yote heri kwa Mwenyezi Mungu. Pia kuja kwake kunahitaji nini? Kunahitaji sana sana kusaidia yale maeneo ambayo kwa sasa yaahitaji umeme kwenye vijiji kama Aicho, Gidamba, Hasama, Boboa na Gedamar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kaya zilizofungwa umeme ni kaya nane, Mheshimiwa Waziri awaelekeze watendaji wa TANESCO kupitia REA waende kwa wananchi, waseme tunahitaji kaya 40 na kaya tunazohitaji ni hizi hapa. Kwa jiografia ya nguzo zetu ili ninyi mfanye wiring na tuweze kuwaunganisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangaliana tu, muda wa mradi unakwisha, umeme umepelekwa kwenye kaya kumi, ishirini badala ya arobaini, tija ile ya kusema kilomita moja kutoka center ya kijiji tunaikosa. Nadhani kazi kubwa imefanyika, tunawapongeza sana na pia bado mahitaji ni makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni umeme ule usio wa waya. Zamani mlikuja na UMETA, sasa hivi sijui mmebatiza jina gani? Najua kuna nyumba ambazo hatutaweza kufikia, kwa sababu unaweza kukuta nyumba ya mwananchi pengine ni nguzo kumi zinahitajika kwenda kwenye nyumba moja, kumbe yule anahitaji umeme wa taa, anahitaji umeme wa kuchaji simu, anahitaji umeme wa matumizi madogo madogo, lakini yule tukifunga hicho chombo ambacho akihitaji waya atatumia kwa muda, akalipia kama bili ya mwezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana kupunguza baadhi ya maeneo na baadhi ya kelele, lakini kwa namna ambavyo yeye tunajua hataweza kufikiwa, kwa sababu hizo nguzo kumi mjini inaweza kuwa nguzo arobaini katika eneo hilo. Hizo nguzo arobaini katika eneo hilo kwa namna ya pekee ingeweza ku-cover hizo nyumba na wakazalisha haraka kuliko tukaenda kwa mwananchi mmoja ambaye atahitaji nguzo kumi na yeye yuko mmoja na matumizi yake ni madogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango wangu huu niendelee kuipongeza Serikali, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)