Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busokelo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia kwenye Wizara yetu hii ya Nishati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aliyetujalia uzima na kufika katika Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waswahili wanasema moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema yote. Nianze kwa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na kubwa iliyotukuka anayotufanyia Watanzania. Kila Mtanzania anaelewa na ameona kazi anazofanya Mheshimiwa Rais, ndiyo maana katika sekta hii ya nishati amefanya vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Kaka yangu, rafiki yangu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa kazi nzuri ambayo anaifanya katika Wizara hii ya Nishati. Pamoja na hilo, nampongeza pia Naibu Waziri, mdogo wangu Judith Kapinga, Katibu Mkuu, Naibu Makatibu Wakuu wote, Wakuu wa Taasisi na wote ambao wapo katika Wizara hii ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kuchangia mchango wangu pasipo kuwasahau Engineer Habibu ambaye ni Meneja wa Wilaya wa TANESCO, Wilaya ya Rungwe, anafanya kazi nzuri sana pamoja na Eng. Sabaya ambaye ni Meneja wa Mkoa wa TANESCO, anafanya kazi nzuri sana kule Mkoani Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niingie katika mchango wangu kwa ajili ya kuishauri Wizara. Jambo la kwanza, wenzangu wengi Waheshimiwa Wabunge pia naungana na Kamati kushauri juu ya kuimarisha zaidi gridi imara pamoja na miundombinu ya kusambazia umeme, kwa sababu hivi sasa tuna umeme wa ziada zaidi ya megawati 4,000, lakini namna ya kuwafikia watumiaji ndiyo changamoto. Kwa hiyo, Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi naiomba iendelee kuongeza kasi katika kusambaza umeme na kuiboresha miundombinu hii ya umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano rahisi, ukienda kule Jimboni kwangu Busokelo, kule tunapata mvua mwaka mzima, takribani miezi 10 mpaka 11. Kwa miezi miwili tu ndiyo tunakuwa hatuna mvua. Sasa ukipeleka nguzo za kawaida ambazo ni za mbao, tafsiri yake ni kwamba, zinaoza haraka. Kwa hiyo, tunatamani sana maeneo haya na maeneo mengine yote oevu katika nchi hii ya Tanzania wasambaze miundombinu ya nguzo za zege. Najua TANESCO wameshaanza kufanya kazi hii, lakini waongeze kasi iwe kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kushauri huu mradi wa Rumakali ambao utazalisha megawati 222 wenye thamani ya trilioni 1,058. Mradi huu ni wa muda mrefu, lakini mradi huu utakuwa na manufaa makubwa sana kwa nchi yetu, na ni mradi ambao unapatikana katika Mikoa miwili ya Mbeya na Njombe, hususan katika Wilaya ya Makete na Halmashauri ya Busokelo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu kule waliambiwa kulipwa fidia tangu miaka ya 2018/2019 takribani shilingi bilioni 264 kwamba, wasiendeleze maeneo yao kwa sababu itapita gridi kubwa ya umeme. Naiomba Serikali yangu kwamba, wananchi hawa wameendelea kusubiri fidia hizi katika Kata za Lufilyo, Itete, Lwangwa, Isange, Mpombo, Kandete. Fidia hii wangelipwa mapema ingesaidia sana ili waanze maisha mapya maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ni Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Najua mnafanya kazi nzuri sana, lakini kwa bahati mbaya sana katika vile vitongoji 15 kwa Mikoa miwili ya Mbeya na Tanga wakandarasi wale hawakupatikana kwa wakati. Hivi ninavyosema, nimeambiwa kwamba, wiki iliyopita ndiyo amesaini vile vitongoji 15.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba REA wasimamie vizuri hawa wakandarasi ili waanze kazi hii kwa sababu wananchi tulishawaaminisha muda mrefu, na vitongoji hivi 15 na vilikuwa budgeted miaka miwili mfululizo. Kwa hiyo, naomba sana wenzetu wa REA jambo hili walisimamie kwa ukaribu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kushauri kwamba, hivi sasa mfumo ama sera ya Serikali upande wa kusambaza umeme inahitaji ulipie kwanza ndipo upate huduma. Naungana na Kamati kwamba, laiti kama tungekuwa na sera mpya ya kwamba Serikali ipeleke umeme kwanza kwa wananchi, halafu mwananchi yule ataendelea kulipa kidogo kidogo ili gharama zile ziweze kufidiwa wakati wa matumizi atakapokuwa ameunganishiwa umeme kwa maana tunaita postpaid. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika Serikali itakusanya fedha nyingi, pia huduma hii itakwenda kwa wananchi wengi. Huu ni ushauri wangu kwa Serikali na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri; ni msikivu sana, naamini hili atalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba, kuna umeme huu wa joto ardhi ama jadidifu. Kule Jimboni kwangu Busokelo ni miongoni mwa maeneo ambayo Mungu ametubariki kuwa na umeme wa jotoardhi (geothermal), tayari wenzetu kupitia kampuni tanzu ya TANESCO wameshachoronga visima kule na vinatoa maji yenye kasi kubwa sana. Sasa ombi langu kwa Wizara ni kwamba Wizara itenge fedha ili umeme huu uanze sasa kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka ni mwaka 2024 kulikuwa na kongamano kubwa sana la Afrika kwa masuala ya jotoardhi hapa nchini. Sisi tunajivunia kwamba tayari maeneo haya, visima hivi vimeshachorongwa, basi umeme uanze kusambazwa kwa maana ya umeme jadidifu hususan katika mradi huu Mbaka, Kyejo, na Mbambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho siyo kwa umuhimu, kuna hili jambo la vituo vya mafuta. Kumekuwa kuna vituo vingi sana vya mafuta ambavyo kila baada ya hatua kadhaa kuna kituo cha mafuta. Naomba Serikali yetu ione umuhimu wa kuweka usalama muhimu katika maeneo haya, kwa sababu hata ikitokea ajali unaweza kukuta jambo hili linakuwa hatari kwa wananchi wanaokaa maeneo hayo, zaidi pia na usalama wa wafanyakazi katika vituo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja ya bajeti ya Serikali kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)