Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kwa hizi dakika sita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mungu pia kwa kutujalia afya njema ili tuendelee kutekeleza majukumu yetu ya Kibunge, lakini ni kwa neema zake siyo kwamba sisi tunastahili sana, ni Mungu ametujalia nimshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nia yake njema ya kutaka kila Mtanzania afikiwe na umeme, ndiyo maana tunaona kwamba Bwawa la Mwalimu Nyerere sasa liko mbioni kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais. Yeye pamoja na Naibu Waziri mdogo wetu, Mheshimiwa Judith kwa kazi ambayo wamekuwa wakiwafanyia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nia njema ya Mheshimiwa Rais inaonekana katika bajeti hii. Hii ni bajeti ambayo 95% ya bajeti wanayopewa inakwenda kwenye maendeleo, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. Ni asilimia tano tu inaenda kwenye OC na mishahara na mambo mengine, lakini 95% ya 1.8 billion ambayo hii wanatekeleza inaenda 1.5 billion kwenye maendeleo. Ni nia njema kabisa ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nia njema ya Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu imeonekana katika bajeti hii, wameongeza tena shilingi bilioni 50 nyingine. Kwa hiyo, bajeti inaenda shilingi trilioni 2.2. zote. Ukiangalia, zaidi ya 90% inakwenda kutatua mahitaji ya Watanzania ya umeme. Nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, na Mheshimiwa Rais, wetu Mama Samia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaamini vitongoji hivyo 32,000 ambavyo vimesalia na hivi ambavyo wanaendelea navyo vitongoji zaidi ya 900 kupitia increment hii, bajeti ya 50 billion plus itakwenda kugusa vitongoji vingi, na Watanzania watafikiwa kwa umeme. Kwa hiyo, hii bajeti ni ya kuungwa mkono, ni bajeti ambayo inaenda kugusa maisha ya Watanzania, kwa sababu umeme umekuwa ni uhitaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, ameliona hili na ndiyo maana bajeti yao imepanda, imeenda zaidi ya shilingi trilioni mbili. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, kwa usikivu ule ule na busara zile zile kwako pamoja na Mheshimiwa Rais wetu, mwangalie gharama hizi za kuunganisha umeme. Tunawaomba, lengo ni jema kabisa, mnapambana, lakini kwenye vijiji mtu ambaye hazidi mita 30 anaunganishiwa kwa shilingi 27,000; ambaye anazidi mita 70 toka miundombinu ya umeme ulikofikia, anaunganishiwa kwa shilingi 515,000, lakini mita 120 ni shilingi 696,000.666.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sisi wale wa mijini, kama mimi natokea Jimbo la Mjini, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, anaunganishiwa kwa takribani shilingi 320,000. Nawaomba m-synchronise, mwangalie hizi gharama za kuunganisha kwa sababu, miji midogo kama Babati, kama Mbulu, kaka yangu Mheshimiwa Issaay amesema na maeneo mengine, ile miji haitofautiani na vijiji na hata huko kwenye vijiji, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Waziri wetu, Doto Biteko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaona kwamba, gharama hizi zimetofautiana, lengo ni jema. Mmeongeza bajeti, basi tunaomba Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri waangalie jicho la kiruzuku katika maeneo hayo, ili gharama za kuunganisha zisilalamikiwe, ili uweze kugusa watu wengi, kwa sababu, Mtanzania wa kawaida aliyeko kitongojini akilipa hizi shilingi laki sita, tayari anakuwa ameishiwa nguvu. Nia yenu ni njema kabisa, nia ya Serikali ni njema, kwenye gharama za kuunganisha mtusaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala zima la miradi ya ujazilizi. Naipongeza Serikali, jambo hili linaenda vizuri. Kwa sisi ambao tunaongoza majimbo ya mijini, wakiona nguzo imevuka imeenda kijijini halafu yeye anaomba pale nguzo moja, nguzo mbili, tatu, anakata tamaa na tumekuwa tukiwatia moyo. Nampongeza Meneja wetu wa Mkoa wa Manyara, amekuwa akitupa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu atuongezee fedha kwa ajili ya umeme jazilizi. Mimi nakaa pale mjini, utakuta mtu anakaa Oysterbay, au Ngarenaro, nguzo mbili, tatu, hawezi kuzipata, anaomba, anatembea mpaka anakata tamaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wamefanya wiring tangu mwaka 2019. Nimekuwa nikiwasiliana na ofisi ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, nimekuwa nikipewa sana ushirikiano, tangu 2019 mtu kafanya wiring, anaomba pale TANESCO, TANESCO wanakwambia bado hatujapata fedha. Naiomba Wizara ya Fedha waweze kufanya disbursement ya hizi bilioni, bajeti yao ilikuwa ni 1.5 trillion, lakini imetolewa one trillion kwenye bajeti ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ile 59% ambayo imetolewa, it is okay, zile zilizobaki waweze kutoa sasa Wizara ya Fedha. Kwa sababu, disbursement yao imekuwa ni 59%. Namwomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, ikimpendeza, basi bajeti yake hii iweze kutolewa kwa asilimia zote. Naamini na kwenye umeme jazilizi watakuwa wamefikiwa baada ya 59%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye vitongoji hivi 15 katika kila Jimbo, napongeza sana, kazi inafanyika na Mameneja wa TANESCO na Ma-engineer wa REA wako site. Kwetu Babati wamefika, wameanza kazi, nawapongeze sana. Ombi langu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, kwa vile vitongoji ambavyo vipo mbali na miundombinu ya umeme, kama ambavyo TANESCO wametuelekeza, sasa wasogeze umeme pale, ili yule mtu wa REA asiache vile vitongoji 15 kwa kila jimbo kwa sababu, tulishawatangazia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ila sasa line kubwa ya umeme ikiwa iko mbali, basi tunaomba Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, wenzetu wa TANESCO waweze kusogeza hizo line, ili hivyo vitongoji 15 ambavyo kazi ilikuwa inatakiwa ianze, viendelee na kazi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu la tatu, kwenye taasisi, nimeona hapa ni kipaumbele katika bajeti, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu ikiwapendeza wenzetu wa mamlaka za maji waangalie gharama zao zile ambazo wanalipa kwa TANESCO, kwa sababu, nitolee mfano Mji wangu wa Babati; visima vyote vimezunguka Ziwa Babati na ule mji umekaa kama bakuli. Maji tunatoa huku bondeni tunayapandisha kwa umeme.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba pia, mawasiliano ya karibu ya TANESCO kupitia bili za maji na units ambazo mamlaka za maji nchini wanatakiwa kulipa, ili waweze kutoa hizo huduma, itasaidia kupunguza bili za maji kwa wananchi. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa malizia...
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nilitamani kusema ni hii mitungi ya gesi, ambayo tumepatiwa. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, Mkoa wetu wa Manyara bado tunaomba tupatiwe ile mitungi ya gesi ya ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kazi ambayo anafanya. Vinginevyo, nawatakia kila heri na hii bajeti tunaiunga mkono ili kazi iendelee. Ahsante sana. (Makofi)