Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi dakika sita za nyongeza ili niweze kuchangia. Naamini kwa mambo makubwa mawili tu, ambayo nilitaka kuyasema zitanitosha kufikisha ujumbe kwa niaba ya wananchi wa Tanzania na hasa wananchi wa Mkalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaongelea vitu viwili tu. Nitaongelea suala la access na connection, access ya umeme vijijini na connection kwa wananchi, na pia nitaongelea suala la tariff ya D1 na T1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la access, nchi yetu imetumia fedha nyingi sana bila kujali inapeleka wapi umeme? Kwa mfano, Serikali imepeleka umeme kijiji cha zaidi ya kilomita labda 100 bila kujali kwenye kijiji kile inakopeleka umeme kuna nyumba ngapi na watu wangapi watapa umeme? Suala lake lilikuwa tu ni kufikisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa fedha hizi nyingi ambazo zimetumika, lile lengo hasa la kutaka wananchi wapate umeme linahusiana na suala la connection. Serikali imefanya jambo hili zito la kufikisha umeme vijiji takribani 12,000 vya nchi hii, umeme umeshafika kijijini au kwenye mji, lakini wananchi wanautazama kwa macho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu kubwa inayochangia ni suala zima la bei za ku-connect umeme. Iko miji midogo midogo, mfano katika Jimbo langu, pale Iguguno na miji mingine ya Nduguti, umeme anaambiwa achangie shilingi 352,000 ili aweze kuvuta umeme wakati Serikali imetumia fedha nyingi sana kuufikisha ule umeme pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba, yako mambo mawili makubwa ambayo yanaweza yakafanyika katika kuhakikisha kwamba, hii access ambayo tumeifanya kubwa katika nchi hii ya kufikisha umeme kwenye vijiji, basi iendane na connections kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu ni bingwa wa ruzuku na ninaamini mwezi wa Kumi wananchi wa Tanzania wanakwenda kupigia kura hizi ruzuku kubwa kubwa. Kuna ruzuku kwenye mbolea, mabilioni; kuna ruzuku kwenye viuatilifu vya dawa na mimea, mabilioni; na sasa ruzuku mpaka kwenye gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata jana tumefungua Coop Bank, Rais ametoa fedha pale kuhakikisha kwamba, hii benki ya ushirika inaenda. Kwa hiyo, namwomba Rais huyu bingwa, mpenda watu wake, aangalie tena suala la ruzuku katika hili suala la connection, ili wananchi waweze kupata umeme kwa bei ya shilingi 27,000 nchi nzima bila kujali mjini, vijijini au miji midogo kwa sababu, fedha aliyotumia kufikisha umeme vijijini ni kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ruzuku ikitizamwa pia kwenye connection itakuwa ni jambo jema kabisa ili wananchi wapate umeme. Hiyo ni kwa upande wa Rais, lakini na Shirika lenyewe la TANESCO, linayo namna ya kuwafanya wananchi wafanye connection. Shirika linakopesheka, linaweza kutafuta fedha mahali popote wakapeleka connection kwa wananchi wote wa Tanzania ambao wanataka umeme. Halafu inapoanza matumizi, kwenye zile tariff, wakamwekea mwananchi kiwango kidogo kidogo akawa analipa kila mwezi kwa kulipa ile shilingi 352,000 kama wanayoitafuta, wala hata-feel. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo TANESCO wanafanya kazi ya kukusanya ushuru wa property tax, tena wanawakusanyia tu watu wengine, siyo zao. Sembuse wakiwafanyia wananchi, wakawa-connect na umeme, halafu matumizi wakawawekea pesa kidogo kidogo wakawa wanarudisha ile fedha ya connection! Watashindwaje kukusanya pesa yao kama leo wanamkusanyia mtu mwingine pesa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Shirika la TANESCO, kwa sababu ruzuku zimezidi, kama itashindikana kwenye ruzuku, basi Shirika lifanye utaratibu wa kuwa-connect watu kwa umeme then anapoanza matumizi, kwa mfano wale wa D1 ni shilingi elfu tisa sijui na mia ngapi? Akiongezewa pale labda shilingi 5,000 au shilingi 6,000 kila anaponunua umeme mpaka atakapomaliza deni lake, wala hatakuli-feel hawezi. Kwa hiyo, naomba sana hii access ya umeme iliyokwenda vijijini iungane na connection. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme sasa ni jambo la nne katika mambo muhimu ya anayohitaji mwananchi. Mwananchi anahitaji chakula, mavazi, malazi, lakini sasa la nne ni umeme. Zamani umeme ilikuwa ni anasa. Ukiona kwa mwenzako unawake, unaona kawaida, hao ni matajiri bwana, lakini sasa hivi umeme ni suala la msingi, ni basic ya nne kwa maisha ya Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana mama, naiomba sana TANESCO; Mheshimiwa Waziri ni mtu wa Mungu, ni mchapakazi, ni mtu rahimu, akisimama tu kuongea, watu wanajua sasa yanashuka madini. Hili la kuisimamia TANESCO iunge umeme kwa watu, halafu iwa-charge kwenye matumizi, linawezekana, liko ndani ya uwezo wake, naomba sana aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nilisema nitaongelea suala la tariff D1 na T2. Sheria inasema mwananchi wa kijijini akiunganishiwa umeme direct, ataunganishwa kwenye D1 na mwananchi wa mjini direct ataunganishwa kwenye T1, lakini ikaja Sheria ya Amendment ya GN ya Mwaka 2016, ikafanyiwa amendment Mwaka 2020, ikaongezwa kipengele kwamba, kila mwananchi ambaye anatumia umeme usiozidi kilowatts 75 achajiwe kwa D1. Kwa hiyo, bila kujali ni wa mjini au ni wa vijijini, ila kama atatumia kilowatts zisizozidi 75 per month achajiwe kwa tariff ya D1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa taratibu wananchi wa mjini wanaondolewa kwenye hii D1. Ukipiga simu TANESCO ukiuliza wanakwambia hii inawahusu wananchi wa vijijini, lakini hii Sheria ya Amendment wanaisahau. Kwa hiyo, naomba sana kama mwananchi anaweza kujibana akatumia tariff siyo chini ya kilowatts 75 kwa mwezi basi achajiwe kwa D1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii dhana kwamba, wananchi wa mjini ni matajiri tuiondoe. Mjini ndiyo kuna watu wana shida kweli kweli. Wapo wajasiriamali wamepanga kwenye chumba kimoja kimoja na bili ya umeme wanajilipia, siyo kwamba, analipa landlord. Kwa hiyo, wanaweza kujibana wakatumia umeme chini ya kilowatts 75 kwa mwezi, wasiondolewe kwenye hiki kitu ili waweze kuufaidi huu umeme ambao nchi yetu imeutafuta, ili wananchi waweze kuutumia. Naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda wako, lakini haya mambo mawili naamini yamefika na yamesikilizwa, na Wabunge ndiyo wamesema mengi sana. Ahsante sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja nikiamini kwamba, hili linakwenda kuwagusa Watanzania na litafanyiwa kazi. (Makofi)