Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Regina Ndege Qwaray

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Nishati. Kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwani amekuwa mfano wa kuigwa, ni mama jasiri ambaye amewatumikia Watanzania bila kuchoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, msaidizi wake, Naibu Waziri, Mheshimiwa Judith Kapinga pamoja na Watumishi wote wa Wizara ya Nishati kwa namna wanavyomsaidia Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba, hii Sekta ya Nishati inakwenda kusonga mbele. Niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa dhamira yake ya dhati kabisa kuhakikisha Watanzania wanakwenda kuondokana na matumizi ya nishati chafu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuwa kinara katika Afrika kuhakikisha kwamba, Watanzania wanatoka kwenye matumizi ya nishati chafu na kwenda kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia. Kwa kufanya hivyo, amekwenda kuokoa maisha ya Watanzania walio wengi, hasa wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu kwamba, wanawake wengi maeneo ya vijijini wamekuwa wakitumia kuni katika kupikia, lakini wanawake wa mijini wamekuwa wakitumia mkaa. Haya yote yanasababisha uharibifu sana wa mazingira, lakini siyo hilo tu pia, wanawake wengi wamekuwa waathirika wakubwa katika afya kwa sababu ya matumizi ya nishati chafu ya kupikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumshukuru sana na sisi, kama wanawake na Watanzania wote, tukamuunge Mheshimiwa Rais kuhakikisha ajenda yake ya Nishati Safi ya Kupikia inakwenda kutimia kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wameanza kuelewa matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia na tayari imeanza kufika mpaka maeneo ya vijijini. Sisi Wabunge, kama wawakilishi wa wananchi tumekwenda kugawa nishati kwa wananchi, hasa katika makundi maalum, lakini bado kuna changamoto, tunaomba Serikali iende kuongeza kasi katika kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana katika mazingira ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wananchi ambao wana mwitikio na wameelewa matumizi ya nishati safi ya kupikia, lakini changamoto ni upatikanaji. Mtu ananunua mtungi wa gesi kituo cha kubadilishia mtungi wa gesi, anatumia gharama kubwa kuliko gharama ya kwenda kubadilisha gesi. Kwa hiyo, naomba sana mawakala wetu wasogeze huduma karibu na wananchi, ili wananchi waweze kupata huduma ya kubadilisha gesi kwa wepesi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Serikali kwa kuongeza kasi kuhakikisha kwamba, vijiji vyote vimekwenda kupata umeme na sasa hivi Serikali ina mpango wa kuelekea kwenye vitongoji na tayari kazi imeanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kuna vijiji vyenye sura ya miji, bado gharama ya kuunganisha umeme imekuwa kubwa. Mfano, Mkoa wangu wa Manyara tuna Kijiji cha Magugu, kuna Kijiji cha Matui, bado gharama iko juu sana, badala ya shilingi 27,000 leo wananchi wanaunganishiwa umeme kwa shilingi 320,000. Ukiona hivyo, ujue kasi ya kuunganisha umeme kwa wananchi imekuwa ndogo ni kwa sababu, wananchi wanashindwa kufikia gharama zile za kuunganisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa, dhamira ya Rais ni kuhakikisha kila Mtanzania anakwenda kupata umeme, naomba sasa Serikali iweke mkakati kuhakikisha vile vijiji vyenye sura ya miji umeme upungue gharama ili wananchi wote waweze kuunganishiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi ambao wana utayari wa kujiunga na umeme wa three phase, lakini wanashindwa kulingana na gharama. Naomba sasa, Serikali iweke mkakati wananchi hawa wapewe mikopo wanapokwenda kuunganisha umeme ili wakipewa mikopo hii watakuwa wanalipa taratibu, kadiri anavyonunua units za Luku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama amenunua units za shilingi laki moja, yule mwananchi apewe nusu, ili nusu ilipie deni la TANESCO. Hii itasaidia wananchi wengi kuendelea na umeme, kujiunga na hiyo nishati safi ya umeme, lakini pia, itasaidia kwenda kuibua viwanda vyetu kuzalisha kwa wingi. Hii ni kwa sababu, gharama itapungua, lakini wananchi wengi watajiunga kwa gharama ambayo akijiunga kwa bei ya mkopo, gharama ya ulipaji haitakuwa na maumivu makali kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi, kama Babati, tuna kituo kile cha kupozea umeme, substation. Kituo hiki toka kimeanza kutumika mpaka leo matumizi yake yako chini ya 50%. Hii ni hasara kwa Shirika. Shirika liangalie namna ambayo inaweza ikapunguza bei ya unit, ili wananchi waweze kuunganisha umeme kwa wepesi kwa sababu, gharama inapokuwa kubwa, ile substation pale uzalishaji wake ni mkubwa, lakini matumizi yanakuwa chini ya kiwango, maana yake, inazalisha chini ya 50%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la umeme wa kupikia katika maeneo yetu ya vijijini. Ili kuendelea kulinda afya ya Mtanzania ni lazima kila mwananchi atoke kwenye matumizi ya nishati chafu kwenda nishati safi ya kupikia, lakini changamoto kubwa tunayoipata kwa sasa, tunaomba Serikali, kwa kuwa, imeshaleta ruzuku kwenye mitungi ya gesi, iongeze ruzuku kwa sababu, bado wananchi wengi wana uhitaji mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ya upatikanaji ni kubwa, kwa hiyo, ikiendelea kuongeza ruzuku; kwanza nishukuru kwa sababu ruzuku imewekwa, lakini bado tunahitaji iongeze zaidi, ili wananchi waende kutumia gesi safi ya kupikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba sana ipunguze gharama za unit ya umeme ili wananchi waweze kutoka kwenye matumizi ya kuni na kupikia majiko ya umeme katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi, naona umewasha taa, lakini niseme kwamba, naiunga mkono bajeti. Nawatakia kila la heri Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake, sisi tunaendelea kuwaunga mkono ili dhamira ya Mheshimiwa Rais iende kutimia kwa 100%, nakushukuru. (Makofi)