Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiwani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. RASHID ABDALLA RASHID: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kupata fursa hii ya kuchangia hii Bajeti yetu ya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia jioni hii kupata fursa ya kuweza kuchangia.
Mheshimiwa Spika, namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambazo anazifanya na kuhakikisha kwamba, anamwaga fedha nyingi katika miradi mingi mikubwa ya maendeleo katika nchi yetu, miradi ambayo ni kielelezo cha kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nampongeza na kumshukuru Rais Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, kwa kazi kubwa anayoifanya Zanzibar kwa ajili ya kutekeleza miradi mingi mikubwa ya maendeleo ambayo inaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kadhalika, lazima nimpongeze na kwa kishindo kikubwa sana ndugu yangu Dkt. Doto Biteko, naye kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha kwamba, anamsaidia Rais katika majukumu aliyompatia na lile la Wizara ya Nishati ambapo tunaona hasa kule Zanzibar nishati ya umeme na gesi imetindimaa. Kadhalika sitaweza kumsahahu Naibu Waziri wake Mheshimiwa Judith Kapinga naye kwa kazi kubwa ambayo anamsaidia Mheshimiwa Doto Biteko kadhalika na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika jambo hili la nishati sitaweza kumsahau Mheshimiwa Shaib Hassan Kaduara, Waziri anayeshughulikia nishati kwa upande wa kule Zanzibar. Pia, sitakusahau wewe Mheshimiwa Spika kwa kazi kubwa ambayo unaifanya wakati ukiwa ni Spika wa nane wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ukiwa Spika wa Pili Mwanamke. Hiyo kama haitoshi, ukiwa Spika wa Pili wa Mabunge ya Dunia, kwa kweli na wewe unahitaji pongezi zako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli tuseme unatuendesha vizuri na unatuongoza vizuri. Wakati mwingine wapo ambao kidogo wanataka kupotea, lakini busara inakutawala na unatuendesha ukiwa kama mama, kwamba huwezi kukubali mtoto wako apotee. Hili kwa kweli tunakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia matukio mengi hapa, unajua kabisa kwamba huyu hapa anakwenda vibaya, lakini kama mama unasimama unaona hapa acha nimweke sawa Mheshimiwa ili mambo yaende vizuri. Kwa hiyo, kwa jambo hili, ni lazima tukupongeze, na tukushukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeanza na Mheshimiwa Rais, kwa nini? Rais huyu Mheshimiwa Dkt. Samia amefanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba miradi yote mikubwa na ya kimkakati anaikamilisha kama ambavyo mtangulizi wake Mheshimiwa Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli aliiacha. Tunapozungumzia Bwawa la Mwalimu Nyerere, kama zilivyo hadidu huko kwamba lilikuwa na 18% au 20% lakini sasa limefika asilimia kubwa. Jambo ambalo hata kwa upande wa Zanzibar umeme huu sasa umetindimaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulikuwa tunapata mgao wa umeme kwa sababu ya upungufu wa umeme ambao tumeunganishwa nao kutoka gridi za Taifa. Kwa mfano, kama Kisiwa cha Pemba kimeunganishwa kutoka Majani Mapana Tanga hadi Ndagoni Wesha, ambapo umeme huo unatusaidia sisi wananchi wa Kisiwa cha Pemba.
Mheshimiwa Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Waziri kwamba umeme huo ndiyo ambao kwa upande wa jimbo langu umemaliza vijiji vyote kuungwa baada ya ule umeme wa mwanzo, ambapo tulikuwa tunatumia vinu vya majenereta kwa ajili ya kupata umeme ule. Tunamshukuru na tunampongeza sana kwa jitihada zake Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko za kuhakikisha kwamba nishati ya umeme Kisiwani Pemba inatindimaa.
Mheshimiwa Spika, kwenye hili lazima tuseme, kuna kitu kimoja ambacho kinahitaji kipatiwe marekebisho kidogo. Umeme unaotoka Tanga kwenda Pemba kuna kituo pale Majani Mapana ambacho ndicho ambacho kinasoma units zote ambazo zinapelekwa Pemba. Sasa, kwa sababu ya usafirishaji wa mkondo huu mkubwa wa Kv 33 ambazo zinasafiri ndani yake, kuna umeme unapotea.
Mheshimiwa Spika, umeme huu unaopotea unapopokelewa katika Kituo cha Ndagoni kule Pemba, unapokelewa ukiwa tayari kuna asilimia kadhaa za umeme ambao umepotea, lakini, hesabu pale zinachukuliwa hizi za huku Majani Mapana jambo ambalo kidogo linaathiri kule kwa wenzetu TANESCO, kwamba wanalipa umeme ambao unapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa namwomba sana Mheshimiwa Dkt. Biteko, na kwa heshima sana hesabu za umeme kwa maana ya units zinazopokelewa kule Ndagoni Wesha pemba ndizo hizo ziingie kwa ZECO ili yale mahusiano yaendelee kwenda vizuri. Sisi kama Wabunge tunafahamu sana kwamba kuna mahusiano makubwa sana kati ya ZECO na TANESCO, na kati ya Wizara ya Nishati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Maji, Nishati ya kule Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, tunaona katika forum mbalimbali viongozi wa Wizara ya Nishati Zanzibar wakishiriki kwenye makongamano na shughuli mbalimbali zinazotayarishwa na Wizara ya Nishati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kadhalika ZECO, kwa maana ya viongozi, nao tunawaona wakishikiri katika makongamano, mambo na shughuli mbalimbali za kiufundi na za kiuongozi kwa wenzao wa TANESCO. Jambo hili linaleta faraja kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, hata ukiangalia, Wizara ya Nishati siyo Wizara ambayo ni ya kimuungano, lakini tunaona mahusiano yaliyopo, hata safari za nje wanatoka Zanzibar wakiambatana na wenzao wa Wizara ya Nishati ya huku wakienda kule.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunashukuru sana kwa jitihada hizi ambazo Mheshimiwa Dkt. Biteko anazichukua, za kuhakikisha kwamba mahusiano ya hizi Wizara mbili yanakuwepo kwa sababu ndani yake kuna jambo muhimu sana la nishati ya umeme ambapo umeme ndiyo maisha ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kadhalika kwa upande wa Zanzibar tulipokea majiko ya gesi zaidi ya 10,000 ambayo yanatumiwa na wajasiriamali, akina baba na akina mama. Tunajua Mheshimiwa Rais hapa alifanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba kila Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kila mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar anapata majiko 100. Ndiyo maana kwa upande wa Zanzibar majimbo 50 tunasema kwamba zaidi ya majiko 10,000 yalitolewa. Majiko haya yamewasaidia sana wajasiriamali akina baba na akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hapa ni lazima tukumbushane au tuombe jambo hapa. Hili suala la bei ya ku-refill ile gesi, hapa ni lazima kuwe na bei elekezi. Hii ni kwa sababu tumegawanyika katika maeneo mbalimbali. Utaikuta ile chupa ambayo tulipatiwa wenzetu wengine wanainunua kwa shilingi 22,000/=, wengine shilingi 23,000/=, lakini maeneo mengine inafika mpaka shilingi 32,000/=. Sasa, hili siyo jambo zuri sana kwa wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba, kama yalivyo mafuta kwa bei elekezi kwa kupitia EWURA na kule Zanzibar mafuta kwa kupitia ZURA, kwamba kuna bei zinatolewa, hizo ndizo bei elekezi. Haya majiko, kwa maana ya kwenye hii gesi ni lazima kuwe na bei elekezi, kwa haya majiko. Maana yake ni nini?
Mheshimiwa Spika, Maana yake ni kwamba, zile chupa ambazo zimetolewa kwa nia safi na Mheshimiwa Rais kupitia Mheshimiwa Waziri zitumike, na siyo baada ya kutumika hizi chupa ziendelee kubaki ndani ya nyumba bila kutumia. Lazima hapa kuwe na bei elekezi ili wananchi waweze kujaza gesi na kuendelea kutumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hali za wananchi zimeboreka, na mazingira yameboreka kupitia gesi hii. Kwa hiyo, ni lazima jambo hili tulifanyie kazi vizuri ili tuweze kuweka ustawi mzuri wa bei hizi za hii nishati ya gesi.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, najua sasa hivi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuna mchakato wa kuongeza cable nyingine ya kutoka Tanga kwenda Pemba kwa sababu ile iliyopo, uwezo wake ni mdogo kwa sasa, kwa sababu ya maendelo makubwa ambayo ameyaleta Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Zanzibar kuna viwanda vingi, hasa Pemba, kuna viwanda vingi na majengo mengi makubwa yameongezeka. Sasa ile cable iliyopo inayobeba mawimbi ya Kv 33 haitoshelezi tena. Kwa hiyo, wapo na mkakati huo, tunaomba pale ambapo watakuwa wamekwama, basi tuweze kuwasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya muda, naomba kuunga mkono hoja hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)