Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kavejuru Eliadory Felix

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru kwa kunipatia fursa hii kuwa mchangiaji wa pili jioni hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Nchi kwa baraka zake anazotujaalia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nakushukuru kwa kutuongoza vyema, hongera sana. Vile vile nampongeza kwanza kabisa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu. Hongera sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, pili ni ndugu yangu Dkt. Doto Mashaka Biteko, Naibu Mkuu na Waziri wa Nishati. Kazi kubwa ameifanya na inaonekana. Waswahili wanasema, wali wa kushiba huonekana kwenye sahani. Hakika matunda na matokeo ya kazi hii inaonekana hata kwa macho. Hongera sana.

Mheshimiwa Spika, pongezi za tatu zimfikie dada yangu Mheshimiwa Judith Salvio Kapinga, msikivu, mwerevu, mchapakazi, simu yake ipo wazi saa 24, ukim-beep ameshapiga, unatakaa nini? Ukimwelezea, tayari ameshaingia kukutatulia tatizo hilo. Ahsante sana na Mungu ambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pongezi nyingine ziwaendee Watendaji Wakuu wa hii Wizara ya Nishati. Zifike kwa Mramba F. Joseph na Naibu wake James Peter Matarajio na Khatib Malimi Kazungu. Vilevile, niwapongeze watendaji wetu waliopo mikoani, nikianza na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kigoma Ndugu Julius Sabu pamoja na Meneja wa TANESCO Wilaya ya Buhigwe Ndugu Abdallah Khamis Mulamuzi kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya kule Mkoani Kigoma. Tumepata miradi mingi, umeme unaendelea katika vitongoji. Sasa Mkoa wetu umeungwa kwenye gridi ya Taifa. Tunasema ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo haya nayo yamechangiwa na uundaji wako wa Kamati nzuri ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini. Nawapongeza; haya mafanikio tunayoyaona ni pamoja na mchango wao, wanakamati hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa, nianze na kutoa ushauri. Tumepiga hatua, na tunaipongeza Serikali yetu kwa kukamilisha mradi mkubwa wa umeme hasa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tumefikisha megawati 4031.71. Hongereni sana. Ni kazi kubwa na ni mapinduzi makubwa sana. Tumeonesha tunao uwezo kwa sababu nia ilikuwepo na uwezo umeonekana na tumefika hapo tulipokuwa tunapatarajia.

Mheshimiwa Spika, Tanzania hii ukiangalia kazi ambazo anaendelea kuzifanya Rais wetu kwa kila Wizara, ukianzia na hii Wizara ya Nishati, ukiangalia na shughuli zinazofanyika kwenye Wizara ya Kilimo, utaona hii nchi yetu inakwenda kufanya mapinduzi makubwa sana hususan kwenye kujenga uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, umeme ndiyo moyo wa viwanda. Tumeshuhudia Kigoma tu baada ya kuungwa kwenye gridi ya Taifa tayari tumepata viwanda vinne. Tumepata Kiwanda kikubwa cha Sukari, kinajengwa Kasulu. Pia tumepata tena kiwanda cha kuchakata mazao ya chikichi. Vilevile tuna kiwanda kitakachofunguliwa mwezi Mei cha kutengeneza cement; na tuna Kiwanda cha Magodoro. Haya ndiyo tuliyokuwa tukiyapigania na tuliyotamani kuyaona siku zote katika mkoa wetu. Bila umeme wa uhakika huwezi ukapata viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba hizi megawati 4031.71 tulizozipata hazitoshi. Ili tujenge uchumi wa viwanda hatuna budi kufanya juhudi kubwa zaidi kwa kujilinganisha na nchi ambazo zimepiga hatua. Nimejaribu kuangalia katika nchi zetu za ulimwengu wa tatu, nikianzia na Bara la Afrika. Nimejaribu kuiangalia Afrika Kusini ina-produce umeme umeme wa kiasi gani? Ina-produce umeme wa megawati 58,095, ni nchi ya pili.

Mheshimiwa Spika, nchi ya kwanza ni Egypt, ina umeme wa Megawati 59,442, na nchi ya tatu ni Nigeria. Ukiziangalia hizi nchi zimepiga hatua kimaendeleo kwa sababu wana umeme wa kutosha na ndiyo ume-stimulate, umechechemua ukuaji wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, nimejaribu kuja kuangalia kwenye Afrika Mashariki na Kati, sasa hivi pongezi kubwa sana kwa Tanzania tunaongoza. Baada ya sisi, wanaofuatia kwenye Afrika Mashariki ni Kenya ambao wana Megawati 3,300, na nchi ya tatu ni Congo DRC, inazalisha umeme Megawati 2,819, lakini wanao upungufu, wana deficit ya umeme wa Megawati 1,036. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, sisi Tanzania kama tutaongeza juhudi, na kwa sababu tuna vyanzo vingi ambavyo tunaweza tukaongeza tukazalisha, tayari tunaweza tukawauzia Wakongo na Warundi ambao wanazalisha umeme wa Megawati 39 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikaangalia nchi ambazo zina uchumi mkubwa katika dunia ya leo, ya kwanza yenye umeme mwingi ni China, ina Megawati bilioni 3.43; nchi ya pili ni United States of America, inazalisha umeme wa Megawati milioni 1.3; nchi ya tatu ni India, ambayo inazalisha umeme wa Megawati 470,448.

Mheshimiwa Spika, nikajaribu kuangalia vyanzo ambavyo vimezisaidia hizi nchi kupata huu umeme mwingi, sisi tunavyo. Mfano mzuri ni India, wananunua makaa ya mawe, ikiwa wananunua kutoka Tanzania na nchi nyingine. Hao wanazalisha umeme mwingi sana. Ukiangalia hizi nchi nyingine, kwa mfano Morocco, Ethiopia ambao wana-produce umeme wa Megawati 5,200 na wameweka plan, kati ya miaka 10 ijayo watafikia Megawati 17,000. Ukiangalia vyanzo walivyonavyo, sana sana ni maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tunayo biomass ya kumwaga! Tunayo natural gas, hydro, coal ambayo ni makaa ya mawe ambayo tunayauza. Bado tuna geothermal, tuna solar, tuna upepo, na tuna uranium. Kwa hiyo, ni mpango tu wa maamuzi wa kupanga na kuweka mikakati ya pamoja. Endapo kutakuwa na plan ya kuongeza umeme ndani ya miaka 10 kwamba tuzalishe zaidi ya Megawati 10,000 kwa Tanzania, uwezo huo upo. Tukishazalisha umeme mwingi tutakuwa tumetengeneza mazingira mazuri ya kuwavuta wawekezaji kuja kuwekeza kwenye nchi yetu, kwa sababu tayari tutakuwa na umeme wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo tunatakiwa tushushe bei ya umeme ili viwanda vitakavyozalisha gharama yake iwe chini. Tukifanya hivyo, tutakuwa tume-accelerate mapinduzi makubwa kwenye viwanda vyetu, na kwenye kilimo ambacho tunazalisha. Badala ya kusafirisha malighafi nje, tutakuja kuwa na viwanda vingi ambavyo vitakuwa hapa nchini, na nchi yetu itakuwa imesonga mbele, na itakuwa imefikia lile lengo la kuwa na uchumi wa viwanda. Huo ndiyo ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wa pili pamoja na shukrani kwa Mkoa wa Kigoma, kuna mradi wa kuzalisha umeme kutoka Mto Malagarasi Megawati 49.5. Mheshimiwa Waziri wa Nishati, ongeza jitihada, umeme ule unahitajika kwa majirani kwa sababu tayari kuna deficit kwa majirani zetu wa Congo DRC na Burundi.

Mheshimiwa Spika, tukizipata zile Megawati 49 zikaingia kwenye gridi ya Taifa na ukijumlisha tena na kilovolt 400 ambazo tayari wameshatuunganishia kutoka Nyakanazi, tayari ziko Kigoma na wakakamilisha tena mradi mwingine wa ile line ya kilovolt 400 ambayo wanataka sasa kuitoa Sumbawanga na kuileta Mpanda na kuileta Kigoma, kwa hiyo, tutakuwa na ziada ya umeme mwingi na tutapata fursa ya kwenda kuwauzia majirani.

Mheshimiwa Spika, tutajenga uchumi wetu na tutakuwa tumetengeneza Kigoma kuwa hub na geti la kibiashara, lakini itakuwa ni hub ya kujenga viwanda ambavyo tayari viko karibu na masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru sana kwa umeme ambao unaendelea kwenye vitongoji, miradi yote ambayo iko kwenye vitongoji vya Wilaya ya Buhigwe. Wakandarasi wapo wanaendelea na kazi. Ahsante sana Naibu Waziri Mheshimiwa Judith, umeifanya kazi. Nimekuwa nikikusumbua, na kule kazi inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wa mwisho; juhudi na mpango wa kutengeneza na kujenga vituo vya kupozea umeme kwa kila wilaya ni jambo la maana na zuri ambalo litaokoa upotevu wa umeme. Itafutwe fedha ili kukamilisha miradi hiyo. Umeme unaokuwa umezalishwa, basi uweze kusafirishwa kwenda kwa wahitaji, kwa maana kila siku mahitaji ya umeme yanaongezeka.

Mheshimiwa Spika, huu umeme ambao tumeupata, tumeufikia wa Megawati 4,000, ndani ya miaka mitatu, miaka minne, miaka mitano unaweza ukawa mdogo kwa sababu ule uhitaji wa viwanda vinavyoenda kujengwa na umeme unaokwenda sasa kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini pamoja na kwenye makazi ambapo kila Mtanzania ana kiu ya kupata umeme nyumbani, unaweza usitosheleze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunahitaji kufanya mapinduzi na kufanya maamuzi, tena ya kijasiri ya kutumia sehemu zile ambazo sources ambazo hatujazi-detect, kwenye uranium, kwenye makaa ya mawe, hata kwenye jua, bado hatujazitumia. Kwa hiyo, tuwekeze zaidi ili tuzalishe umeme mkubwa utakaotengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, na Mungu awabariki. (Makofi)