Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa maoni yangu katika hoja iliyopo mbele yetu. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanazozifanya katika Sekta ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, toka walipoingia pale wametatua changamoto nyingi, lakini kubwa zaidi nawashukuru wao Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa ushirikiano wanaoendelea kutupatia sisi Wabunge wenzao, wamekuwa wepesi wa kutusikiliza. Siyo kusikiliza tu, pamoja na kutatua changamoto zinazotukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa slogan yake ya kunena na kutenda. Amekuwa akiitekeleza vilivyo; anasikiliza pamoja na kutenda, haishii kusikiliza tu, baadaye mnaanza kupishana kwenye makorido na kutazamana pembeni. Nakupongeza sana Naibu Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mama yetu Dkt. Samia Suluhu alipoingia madarakani, Jimbo la Meatu utekelezaji wa umeme katika vijiji ilikuwa ni 40%. Hivi tunavyoongea, toka mwaka 2024 umeme huo umesambazwa katika vijiji kwa 100%. Kata saba kati ya 16 ambazo tulipoingia madarakani zilikuwa hazijapata umeme, ikiwemo Kata ya Mwamanimba, Mwamalole, Mbushi, Mwabuzo, Mwamanonga, Imalamako, pamoja na Kabondo, sasa hivi wanawasha na wananchi wananufaika na umeme huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna siku tulikutana na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu, tukatoa kero zetu. Mojawapo ya kero katika Jimbo la Meatu ilikuwa ni kukatikakatika kwa umeme ambako kulikuwa kunatokana na wilaya hii kuwa pembezoni.

Mheshimiwa Spika, sisi Wilaya ya Meatu tulikuwa mbali na kituo cha kupozea umeme kwa sababu kituo hiki kilikuwa kinapatikana Ibadakuli Shinyanga, na Mkoa wa Simiyu bado tulikuwa hatujapata kituo cha kupozea umeme. Nilipomtolea hii hoja Mheshimiwa Waziri alifanya utekelezaji mara moja. Tunachukua umeme kutoka katika Kituo cha Kupozea Umeme Singida, ambacho kinaingilia Mkalama mpaka Bukundi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unafuu upo, pamoja na kukatikakatika kwa umeme, lakini kuna unafuu. Wakati mwingine Ibadakuli wanapofanya matengenezo tunawasha ule wa kutokea Singida. Inapotokea Singida kuna matatizo, tunawasha ule wa Ibadakuli, na wakati mwingine wote kwa pamoja unafanya kazi. Huu wa Singida unanufaisha Kata ya Bukundi, Kata ya Mbushi, Kata ya Mwanjolo, na Vijiji vya Mwabagalu na Itaba, vilivyoko Kata vya Nkoma. Nashukuru sana sana kwa hatua aliyoichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa vitongoji 15 tulivyoipewa vya ujazilizi, ambavyo mkandarasi sasa anaendelea. Ameshaanza kusimika nguzo, ameshafikisha transformer pamoja na nyaya zinazotakiwa tayari kwa utekelezaji. Nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna vitongozi 15 kwa jimbo, mkandarasi alikuwa ana changamoto za kimkataba. Zile changamoto zimeisha, sasa hivi ameanza kazi ya kuchimba mashimo kwa ajili ya kusambaza umeme huu. Tayari ameshaanza kusomba nguzo pamoja na transformer. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kushukuru sana kwa kazi nzuri zinazofanywa. Katika tenda iliyotolewa ya kutangaza kazi, sisi Jimbo la Meatu tutanufaika na vitongoji 55. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini nitoe ombi langu. Kipaumbele chetu katika Jimbo la Meatu, kwanza ni kufikia umeme katika taasisi za Serikali. Katika vile vitongoji 15 tulishindwa kufikisha katika taasisi za Serikali kutokana na kwamba hakukuwa na line kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kwenye hivi vitongoji 55 vilivyotangazwa kuwepo na main line ambayo itatusaidia ku-supply katika taasisi za Serikali, na hata sekta kubwa, vitongoji vikubwa vilivyochangamka ambavyo vilipitwa na umeme kutokana na kukosa line kubwa. Nafahamu, pamoja na changamoto tulizonazo, tunatekeleza mradi mkubwa wa kituo cha kupozea umeme katika Mkoa wetu wa Simiyu, kilichopo Imalilo, Wilaya ya Bariadi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2024 wakati ninachangia katika hotuba hii, mkandarasi alikuwa ametoka site. Yule wa line kubwa alikuwa anadai shilingi bilioni saba. Leo kwa moyo wangu wa dhati niko mbele yako nikiishukuru Serikali. Mkandarasi huyu tayari ameshalipwa hili deni na amerudi site kwa ajili ya kuanza kazi. Kwa kuwa tulikuwa 30%, basi asimamiwe naye ajitume, twende kwa kukimbia kwa sababu ameshalipwa lile deni lake alilokuwa anadai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia, naomba yule mkandarasi wa substation naye alipwe ili waende pamoja, kwa sababu zile substations zitawezesha wilaya zilizoko pembezoni ziweze kupokea umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kushukuru kwa Mradi wa Utafiti wa Mafuta unaofanywa katika Wilaya ya Meatu katika Ziwa Eyasi, Wembele. Kazi inaendelea vizuri, lakini sisi wananchi tulitamani kuona sasa tunanufaika na huu mradi kwa sababu umechukua muda mrefu, utafiti unaendelea.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)