Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia bajeti hii ya nishati, lakini ninachukua nafasi hii vilevile kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa neema na rehema ambazo amenipatia hata kufika na kuweza kuongea mbele ya hadhara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa zaidi namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo Sekta ya Nishati kwa kiasi kikubwa imepiga hatua katika nchi yetu. Nchi yetu sasa katika habari ya umeme imekuwa historia kwa sababu tuna umeme wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumshukuru tena na kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu kwa weledi na umadhubuti katika kuchangia stability katika Sekta ya Nishati. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Nollo hebu subiri. Mheshimiwa Getere sogea pale kwa Mheshimiwa Almas Maige.

(Hapa Mhe. Boniphace M. Getere alipita kati ya Kiti cha Spika na Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Kenneth Nollo, endelea.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, pamoja na kushukuru kwa kazi kubwa iliyofanywa na Waziri wa Nishati, lakini ninashukuru kwa namna ambavyo vitongoji vyangu ambavyo Serikali iliahidi, vile 15, tayari kazi ya kuweka umeme katika maeneo yale inaendelea. Vijiji vyetu vyote 59 katika Wilaya ya Bahi tuna umeme, na sasa matarajio yetu makubwa, kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji iweze kuongezwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina mambo matatu. Jambo la kwanza ambalo nataka nichangie, sasa tuna umeme wa uhakika lakini kubwa zaidi zipo tozo ambazo tunachangia kwenye mifuko hii. Mfuko ambao unaenda kuchangia katika kusambaza umeme katika maeneo yetu, fedha hizi, ile asilimia tatu, haziendi zote kama ambavyo tunatarajia. Fedha zile ziko ringfenced.

Mheshimiwa Spika, sasa, leo nimeuliza swali kuhusu Wizara ya Maji, kwamba fedha hizi zinakuwa na ukomo wa bajeti, ile ceiling. Sasa hizi ni fedha ambazo zinawekwa katika sekta maalumu kama hivi kwenye Nishati. Naishauri Serikali kwamba fedha hizi zitumike kama ambavyo tumekusudia kwenda kuendeleza Sekta hii ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu kuunganishiwa umeme (Connectivity) kwa mteja wa mwisho, ninadhani tutoke kwenye mazoea. Mteja sio kazi yake kununua nguzo zinazokuja kuunganishwa kwake. Duniani kote, mimi siwezi nikatoa capital investment ya shirika lile linalosambaza umeme. Kwa hiyo, tusifanye mazoea na TANESCO ibadilike, kwamba, inavyoniunganishia umeme mimi nitanunua umeme baadaye, lakini unavyokuwa na wateja wengi unatengeneza base ya kuweza kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata ile tofauti ya shilingi 27,000 kwa shilingi laki tatu mijini na vijijini, mimi ninadhani tungekuwa na flat rate walau ya shilingi 50,000, ambayo ile tunalipa kwa ajili ya administrative na labour cost. Habari ya mimi ninunue nguzo, ninunue material za kuunganishia umeme, nadhani siyo sahihi. Kufanya hivyo tutaweza kuruhusu Watanzania wengi waweze kupata umeme katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni habari ya matumizi ya gesi. Nchi yetu tunaagiza gesi hii tunayopikia majumbani. Gesi hii haifanani na gesi inayotoka Mtwara. Hii ni gesi ambayo ni LPG ambayo tunanunua, tunatumia fedha nyingi. LNG ndiyo gesi ambayo tunatoa Mtwara, siyo lazima tutoe bomba kutoka Da es Salaam ije mikoa mingine katika miji. Tunaweza tukafanya kama tunavyosafirisha mafuta. Tukaweka deport kubwa ya gesi hapa Dodoma na gesi ikaletwa hapa na ikaweza kusambazwa katika majumba.

Mheshimiwa Spika, siyo lazima Serikali ifanye kazi hii; tangazieni kampuni kubwa waje wawekeze, tuweze kusambaza gesi katika majumba.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa, taarifa.

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo,...

SPIKA: Mheshimiwa Kenneth Nollo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamis Mwagao Tabasamu.

TAARIFA

MHE. TAMASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba kubeba gesi hiyo ya CNG kuisafirisha, gari moja lenye ukubwa wa tani 40 inabeba mzigo wa tani tatu tu peke yake. Sasa, kuisafirisha kuitoa Mtwara mpaka kuileta Dar es Salaam kwa kutumia magari itakuwa ni hasara ambapo nchi itaingia katika hasara kubwa. Mheshimiwa endelea na mchango wako. (Makofi)

SPIKA: Kenneth Nollo, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa yake kwa maana ya kwamba mimi nimelinganisha LPG na Gesi Asilia. Utaalamu wake kwanza unaisafirisha ikiwa condensed, ikifika hapa inakuwa processed inakuwa ni gesi. Sasa hii tunayotoa nje ni sawasawa unajenga ghorofa kwa kutumia maji ya kwenye ndoo. Sasa hiyo ghorofa utaimaliza saa ngapi?

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, sasa tuna reli. Unaweza ukasema kwa mfano central zone unaitoa Dar es Salaam, ukaweka special train ambayo itafikisha Dodoma hapa na mikoa mingine hivyo hivyo. Pia, Serikali kama inavyosambaza umeme kupitia TANESCO, itangaze kwani zitapatikana kampuni ambazo zinaweza kuwekeza na wananchi waunganishiwe katika nyumba zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu kupitia Rais wetu, tumekuwa kinara katika kunusuru uharibifu wa mazingira. Sasa jambo hili kama nilivyosema, tukisambaza gesi katika nyumba zetu na kukawa na distribution nzuri, kwanza tutaondoa uharibifu wa mazingira. Miji yetu mikubwa; Dar es salaam, Dodoma na majiji mengine ndiyo yanayoongoza kwa kuchukua mikaa. Kwa hiyo uharibifu ni mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo TPDC wameanza pale Dar es Salaam kusambaza gesi, basi hata Dar es Salaam ingekuwa mfano. Jambo hili tukilifanya litasaidia kwa ajili ya kuondoa matumizi makubwa ya mkaa ambao unaleta uharibifu mkubwa wa mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tumepata umeme wa kutosha na ipo haja ya kujadili. Je, ile 75 kwa unit tuendelee nayo au kuna haja ya kufanya mjadala vilevile kwamba tunaweza tukashusha. Ukishusha unaruhusu majumbani watu waweze kutumia nishati ya umeme, tusiuogope sana umeme. Hoja yangu tusiuogope sana umeme. Kama ambavyo Serikali ime-subsidize kwa sababu tuna umeme wa kutosha, bado tuna nafasi ya kuweza ku-subsidize katika suala zima la kupunguza gharama za umeme.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)