Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya Nishati kwa ujumla wake, na kipekee nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko. Kimsingi sisi watu wa Kanda ya Ziwa uwepo wa Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko ni hazina kubwa katika watu wa Kanda ya Ziwa, na ni moja ya vijana wenye matumaini katika nchi yetu, lakini pia ni moja ya Mawaziri watulivu sana wanaoweza kusikiliza mtu na kuamua kile wanachoamua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Naibu Waziri, ameteuliwa hivi karibuni, lakini ameshika nafasi kama mtu wa siku zote. Ni moja ya wanawake jasiri sana hapa Tanzania, tunampongeza kwa usikivu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru Rais wetu kwa kutoa umeme kwa nchi yetu ilivyokuwa megawatt 2,600 mpaka elfu nne na point na nchi ikatulia, akamaliza miradi yote ambayo yanahusika na umeme hasa mradi mkubwa wa Bwawa la Nyerere; tunampongeza sana sana sana Mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kusema kweli uwepo wa mama umeonesha kwamba mwanamke anaweza kutenda matendo yoyote bila kusaidiwa, anaweza kusimamia miradi mikubwa na ikawezekana. Naishauri TANESCO na watu wa Wizara ya Nishati, kuna jambo naliona hapa. Mradi mkubwa wa mapato ya Serikali ni umeme, lakini umeme huo tunavyouendesha ni kama vile bidhaa adimu hivi.

Mheshimiwa Spika, amezungumza hapa Mbunge aliyekaa sasa hivi hapa, yaani kumpelekea mtu umeme ni kama vile unampelekea vitu vya anasa sijui, umwambie anunue sijui NEAT, atengeneze sijui vitu gani, afanye mambo gani, alete gari ya kuleta umeme, asafirishe; ni kitu gani hiki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu watu wote wa Tanzania wanahitaji umeme. Wote wanahitaji umeme. Siku hizi hakuna mtu anataka kukaa giza, hakuna. Watu wangu wa jimboni, ule umeme wanapelekewa wa REA imekuwa vita. Watu wanaenda wanauliza sasa umeme huu Mbunge amekatalia, umeme Mbunge amekatalia, umeme Mbunge amekatalia, umeme Mbunge amekatalia.

Mheshimiwa Spika, nimewauliza, mimi kazi yangu ya Ubunge ni kupeleka umeme kwenye Kijiji A au kwenye kitongoji A; kazi ya kugawa umeme kwa watu, uende wapi, siyo yangu, ni ya Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji, lakini mtu anapiga simu Mbunge umeninyima umeme, umeninyima umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naamini kabisa biashara kubwa hapa Tanzania ni umeme. Tufanyeje? Tukopeshe watu umeme, watalipa. Si wanalipa TANESCO! Wanalipa umeme, si walipe! Si tupeleke hata tufanye pilot area hata Mkoa mmoja hata wa Mara? Tufanye pilot area, watu wote wanaouhitaji umeme wapewe halafu walipe, tutafute fedha benki watu walipe umeme, wakopeshwe umeme watalipa humo humo kwenye umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu umeme sasa tukienda nao hivi hatutafika. Tumeongeza umeme wa Bwawa la Nyerere, sasa huu unatosheleza. Tugawe umeme kwa kuwapa watu wenye uwezo, hivi kiwanda kinakosaje umeme? Si kipelekewe kilipe? Mtu anafanya biashara, ana mashine ya unga, ana mashine nyingine, ana viwanda vidogo, si wapelekewe walipe kwa mkopo? Kwani shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale ni wateja wetu, kiwanda hakina umeme. Mtu anasema shilingi milioni 38. Yaani kupeleka maji kwenye kisima cha pump cha kijiji ni shilingi milioni 38; anatoa wapi? Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Dkt. Doto, nadhani sasa hivi amefika hatua nzuri, nami nilikuwa naelewa kidogo, sasa nimeelewa sana.

Mheshimiwa Spika, kwa nini Waziri wa Nishati na baadaye akapewa Naibu Waziri Mkuu? Kumbe nikakuta fedha nyingi zinazoendesha hii nchi zipo Wizara ya Nishati, miradi mikubwa ya mabilioni na matrilioni ipo Wizara ya Nishati. Kwa hiyo, ana nguvu zote Mheshimiwa Dkt. Doto, sasa watu hawamkaribii. Yeye aamue anachoamua, watu wapate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, nafarijika sana na kauli yako, uliwahi kusema, jamani hapa TANESCO, watu hawajui optical fiber, sijui hawajui umeme wa Megawatts 200 au 300 hawajui, wanataka umeme. Sasa na wewe hiyo lugha yako umeifanya imetusaidia sasa tutafute alternative ya kukopesha watu umeme ili watu wapate umeme. Mashine zote zipate umeme, viwanda vyote umeme, shule za sekondari zilipe kwa sababu wanapewa ruzuku, na shule za msingi walipe. Kwa hiyo, naomba watu wote wapewe umeme.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nataka kushauri ni moja tu. REA wanapeleka umeme kwenye vitongoji na kwenye vijiji. Sasa hoja inakuja, ni nani aliyejua kitongoji A kinahitaji kilometa mbili, kitongoji C kinahitaji kilometa tatu, kitongoji A sijui ngapi? Au kitongoji hiki kinahitaji kilometa nne; nani aliyejua? Kwa nini tusiende kufanya survey kwenye vitongoji na vijiji halafu tukarudi kuja kuwapelekea umeme?
Mheshimiwa Spika, unaweza kukuta eneo moja lina nyumba ambazo zipo msongamano wa karibu ukawapelekea kilometa mbili, ukakuta nyumba zenye msongamano wa mbali mbali ukapeleka kilometa tatu, sasa unakuta unaleta vita kubwa. Tunaomba sasa REA waende kwanza wakaangalie mazingira yaliyopo kwenye kitongoji A, na kitongoji B, wapime halafu wakirudi waamue pale tupeleke tatu, pale tupeleke nne, pale tupeleke tano. Itasaidia kujua kwenye eneo ambalo linahitaji umeme mwingi wapelekewe umeme mwingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kusema kweli watu wa REA wanafanya kazi nzuri sana, lakini Wakandarasi wa REA hatujui ni kitu gani kinatokea? Tunapima umeme mwezi wa Kwanza, kazi inakwenda kufanyika mwezi wa Sita. Wananchi wanaona kama vile wameenda kudanganywa. Tumekwenda kufanya hiyo survey mwezi wa Kwanza, tunakaa mpaka mwezi wa Sita ndio tunaenda kutekeleza umeme na hata wakati tunatekeleza tunatekeleza kitongoji kimoja, hapa viwili, hapa vitatu, hatuendi kwenye kasi inayohitajika, na tatizo kubwa wanasema ni nguzo.

Mheshimiwa Spika, naomba kumwambia Mheshimiwa Dkt. Doto, tuna miti mingi, tuna zile nguzo sijui wanaita za zege, kwa nini sasa tena tunakuwa na matatizo makubwa kama haya? Tunaomba kama tumeamua kupimiwa umeme, tupelekewe kwa wakati muafaka ili wananchi waone kwamba kazi gani inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Mkuu, mwisho nakuomba, ile Bunda ni ya kwako na bahati nzuri wewe inaonekana wazazi wako walitokea maeneo yale. Sasa nakuomba, nina vitongoji vya Kata ya Kitale vingi havina umeme, vitongoji vya Kata ya Mihingo vingi havina umeme, vitongoji vya Kata ya Mgeta vingi havina umeme, vitongoji vya Kata ya Hunyari vingi havina umeme, vitongoji vya Kata ya Mang’uta vingi havina umeme, na vitongoji vya Kata ya Salama vingi havina umeme. Nakuomba kama mzaliwa wa Bunda pale, tafadhali utusaidie umeme.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja (Makofi/Kicheko)