Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbeya Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii.
Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Naibu Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza Mhimili wa Bunge.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.
Mheshimiwa Spika, hotuba ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri imejaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ushindani wa Kimataifa (National competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.”
Mheshimiwa Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Nishati, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimazi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno kuinua uchumi katika kipindi hiki kigumu.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kuendelea kutekeleza kwa ufanisi mkubwa miradi ya umeme ikiwemo Miradi ya Kusambaza Umeme Vijijini (REA) kwa 100% na ujenzi mkubwa wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2115. Miradi hii ya kusambaza umeme vijijini umeiweka Tanzania katika nafasi ya juu Afrika na umeweza kuchochea kasi ya ukuaji wa viwanda na uchumi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za vita ya Ukraine na Urusi na kupelekea kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, naipongeza Serikali kwa kuishirikisha Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, EWURA na wadau wengine, kuimarisha Mfuko wa Kudhibiti Mabadiliko ya Bei za Mafuta (Fuel Price Stabilization Fund) ili kukabiliana na kupanda kwa bei za mafuta.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali ichukue hatua stahiki za kuanzisha Hifadhi ya Taifa ya Kimkakati ya Mafuta (Strategic Petroleum Reserve - SPR) ili kukabiliana na dharura na kuimarisha usalama na uhakika wa mafuta kwa Taifa.
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kuchochea upatikanaji wa US$ hasa kutoka vyanzo vya madini na kilimo na ikiwezekana kuanzisha utaratibu wa biashara ya Serikali kwa Serikali na nchi rafiki zinazozalisha mafuta kwa makubaliano ya kulipa baada ya makusanyo ya mauzo ya madini na kilimo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaweza kuratibu mfumo mzuri wa kununua dhahabu yote toka kwa wachimbaji wadogo kwa shilingi na kulipa bei nzuri zaidi kuliko hata ya soko, na ikifanya hivyo kwa mazao ambayo yamekuwa yanatoroshwa kinyemela nje ya nchi; dhahabu na mazao yaliyonunuliwa kwa shilingi yapate soko zuri kwa wanunuzi kwa dola za Kimarekani kusaidia uagizwaji wa mafuta.
Mheshimiwa Spika, mfumo wa kununua mafuta kwa pamoja (BPS) umeonesha mafanikio makubwa na napendekeza uendelee ikiwa ni pamoja na kuvutia kutumika kwa mahitaji ya mafuta kwa nchi jirani. Mfumo huu uboreshwe hasa katika kuweka vinasaba kwa kutumia mashine (automation) na pia kuwepo na ulinganifu wa taarifa ya kila siku kati ya kiasi cha vinasaba vilivyotumika na kiasi cha mafuta yaliyopakiliwa na pia magari ya kubeba vinasaba yafungwe kamera kwa ajili ya udhibiti mafuta yanayoenda nchi za nje pasipo kutorudi kinyemela kutumika nchini.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto za kupakua mafuta bandarini, napendekeza kupanua na kuboresha miundombinu ya kupakulia na kupokelea mafuta ikiwemo kupakua mafuta kwa saa 24. Napendekeza pia kujenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta kwa matumizi ya ndani na pia kwa nchi jirani na usafirishaji uwe wenye tija kubwa ikiwemo kusafirisha kwa treni.
Mheshimiwa Spika, pia Serikali iangalie uwezekano wa kujenga bomba la mafuta kwenye MKUZA wa TAZAMA na kujenga miundombinu ya kuhifadhi mafuta kwenye bandari kavu Mbeya kwa matumizi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani za DRC, Zambia, Malawi na hata Zimbabwe.
Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa kufikisha umeme kwa 100% kwenye vijiji vyote na pia kwa mkakati wa kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote vya Jimbo la Mbeya Vijijini. Napendekeza kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mradi wa Ujazilizi (Densification).
Mheshimiwa Spika, napendekeza utekelezaji utoe kipaumbele kwa vitongoji kwenye idadi kubwa ya wakazi na maeneo yenye shughuli za kiuchumi na kijamii, ikiwemo Shule ya Sekondari Lwiji. Katika vijiji vilivyopatiwa umeme kwa kiasi kikubwa imechochea ukuaji wa viwanda hasa vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Nashauri TANESCO iongeze speed ya kuunganisha umeme na pia kushughulikia maombi ya wateja wengi wanaosubiri umeme ikichukuliwa kuwa hii ni fursa pia kwa TANESCO kuongeza mapato ya shirika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na vyanzo vya sasa, napendekeza Serikali itekeleze miradi ya vyanzo vingine, kama vile vyanzo vya jotoardhi, umeme wa jua, upepo na makaa ya mawe ili nchi yetu iendane na mahitaji makubwa ya umeme kwa hapa Tanzania na hata kuuza kwa nchi nyingine za Afrika.
Mheshimiwa Spika, ni muda mrefu sasa, TANESCO kupitia Kampuni Tanzu ya Uendelezaji wa Jotoardhi Nchini (TGDC) inaendelea na tafiti katika maeneo mbalimbali nchini kama vile eneo la Ziwa Ngozi lililoko Mkoani Mbeya ambapo ndipo yalipo makutano ya Bonde la Ufa la Upande wa Mashariki na lile la Magharibi.
Mheshimiwa Spika, napendekeza Serikali iharakishe utekelezaji wa miradi huu wa jotoardhi na ule wa Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Kiwira ili tuweza kuzalisha umeme zaidi kwa mahitaji ya ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.