Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAADA MANSOUR HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika Bajeti hii ya Nishati ya mwaka 2025/2026 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anazoendelea kuzifanya za kuwatumikia wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, naungana na Umoja wa Afrika (AU) kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa ajenda ya nishati safi ya kupikia Barani Afrika.
Mheshimiwa Spika, ajenda ya nishati safi ya kupikia ni muhimu katika kuokoa ukataji holela wa misitu kwa matumizi ya kuni na mkaa. Ukataji ovyo wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa unachangia sana mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuleta mafuriko ya mara kwa mara, jangwa na ukame.
Mheshimiwa Spika, wananchi tukilinda misitu yetu, mito yetu, na Bahari, nchi yetu itakuwa na neema ya mvua nzuri, uvuvi bora na ustawi wa chakula.
Mheshimiwa Spika, pia kwa kuimarisha Sera ya Nishati Safi Kupikia, tutalinda afya za wanawake dhidi ya magonjwa mbalimbali kama vile Kifua Kuu na Kansa.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili, najielekeza kuhusu Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere lililopo kule Rufiji. Naendelea kumpongeza tena Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana ya ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na kulikamilisha kwa wakati pamoja na miradi mbalimbali inayoendelea.
Mheshimiwa Spika, bwawa hili ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. Kule Zanzibar kuna uwekezaji mkubwa wa hoteli kubwa na ndogo ndogo katika mkoa wangu wa Kaskazini Unguja. Ujenzi wa hoteli hizo kwa kiwango kikubwa utakwenda kusaidia wananchi kwa kupata ajira na fursa za biashara.
Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kuipongeza Wizara ya Nishati chini ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko na Naibu Waziri Mheshimiwa Judith Kapinga na watendaji wote wa Wizara hii ya Nishati kwa kazi kubwa na nzuri wanazozifanya katika kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba kule Mkoa wa Kaskazini Unguja wanawake bado wanateseka na matumizi ya kupikia kuni na mkaa, nilikuwa naiomba Serikali, mkaa mbadala uweze kuingia Zanzibar na uanze kutumika ili wanawake hawa wapate kutumia kwa matumizi ya kupikia, pamoja na gesi kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.