Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Spika, nianze mchango wangu kwa kutoa pongezi nyingi sana kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko kwa kazi nzuri sana anayoifanya katika Wizara hii na nchi yetu kwa ujumla. Ametupa imani kubwa sana, tunaendelea kumwombea.

Mheshimiwa Spika, pia tunampongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Judith Kapinga, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, ninayo mambo machache katika mchango wangu. Kwanza napongeza kazi nzuri iliyofanywa na Wizara hii hasa katika Mkoa wangu wa Iringa. Mkoa wetu wote tumeshapata umeme katika vijiji vyote na sasa bado vitongoji tu baadhi bado, tunaiomba Serikali itenge fedha za kutosha ili wananchi wote waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna maeneo yaliyokuwa ya vijijini baada ya upanuzi wa miji yakaingia mijini na ilikuwa chini ya mpango wa REA. Naomba Serikali ifanye upembuzi yakinifu ili maeneo hayo yapate umeme.

Mheshimiwa Spika, kuhusu gharama ya usambazaji umeme, gharama za uunganishaji zimekuwa kubwa sana. Kuna baadhi ya malalamiko ya wananchi. Kumekuwa na tofauti kubwa sana ya kuunganishia umeme wananchi mfano wananchi wa vijijini, wanaunganisha kwa shilingi 27,000 na walio umbali wa mita 70 wanaunganisha kwa shilingi 515,617 na umbali wa mita 120 shilingi 696,669.64. Tunaomba Serikali iangalie upya hizi gharama za kuunganisha umeme.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu ujenzi wa vituo vya mafuta umeonekana kufanyika kwa namba, vipo jirani sana vingine karibu na makazi ya watu na inahatarisha sana maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Spika, naendelea kuipongeza Serikali, ilitangaza tender ya kujenga vituo vidogo vijijini na mikopo ya ujenzi wa vituo hivyo na ukaguzi na vibali vilitolewa, lakini hatujajua mpango huo ukoje? Umefikia wapi? Kwa kuwa ni mpango mzuri wa kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata mafuta ya uhakika na kutekeleza ukuaji wa uchumi nchini, nampongeza sana Mkurugenzi wa REA kwa kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni mpango wa Serikali wa kuzalisha umeme kwa kutumia Mto Ruaha ni wa muda mrefu sana. Je, lini sasa mpango huo utakamilika ili kuanza ujenzi wa njia ya kusafirisha Kv 400 kutoka Iringa mpaka Sumbawanga kupitia Tunduma?

Mheshimiwa Spika, kuhusu usambazaji gesi, nampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa kwa kupata tuzo kuwa kinara wa nishati safi ya kupikia. Najua hiyo yote ni juhudi ya Wizara hii. Tunaomba sasa Serikali iwe na mpango mkakati wa kuhakikisha bei ya gesi ya kupikia inakuwa ndogo na gharama ya mitungi ili ile dhamira ya kutunza mazingira na kumtua mwanamke kuni kichwani iweze kutimia.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache naunga mkono hoja.