Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuchangia hoja. Awali ya yote naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema na baraka zake na kutujalia tuwepo hapa siku ya leo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili; kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa sana, naomba nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika Taifa letu, lakini kwa mahususi kwa kazi kubwa inayofanyika katika Sekta ya Nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya misingi ya ukuaji wa kiuchumi na maendeleo katika Taifa lolote ni uwekezaji katika Sekta ya Nishati. Uwekezaji usipofanyika vizuri katika Sekta ya Nishati, unaweza kuchangia kupungua kwa pato la Taifa kwa hadi asilimia mbili na ndiyo maana tunaona leo Mheshimiwa Rais, ameweka nguvu kubwa sana katika kuwekeza katika Sekta ya Nishati kwa ajili ya kutegemeza sekta nyingine katika ukuaji wa kiuchumi wa Taifa letu na vilevile, katika kutegemeza sekta zinazotoa huduma za kijamii katika Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kweli tunaendelea sana kumpongeza Mheshimiwa Rais na hata pongezi hizi zote ambazo zinatolewa kwa kweli ni pongezi zinazostahili sana kwa jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie pia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa miongozo mingi wanayotupatia katika utekelezaji wa shughuli zetu.
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba pia nikupongeze wewe Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo unatuongoza vizuri sana hapa Bungeni. Kwa kuwa nami ni kiongozi mwanamke, naomba niseme yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, wengi tunamfahamu kwa sifa zako kama Spika wa Bunge, lakini Spika wa Mabunge Duniani, lakini wengi hawafahamu kwamba Spika huyu pamoja na shughuli nzuri za kuwalea wanawake TWPG, lakini ndio mlezi wa Wabunge vijana wanawake kwa miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na shughuli zako za Bunge tunaendelea kukupongeza kwa mchango mkubwa unaouweka katika kumwinua mwanamke kiongozi. Ahsante sana na Mungu akubariki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia niwashukuru Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wote ambao kwa kweli wanafanya shughuli zao vizuri hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika, kipekee naomba niipongeze Kamati yetu ya Kudumu ya Nishati na Madini inayoongozwa na kaka yangu Mheshimiwa Dkt. David Mathayo pamoja na Wajumbe wote wa Kamati. Kwa kweli kwa kipindi chote hiki ambacho mimi nimekuwa Naibu Waziri, tumefanya kazi vizuri sana na kwa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.
TAARIFA
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Elibariki Immanuel Kingu.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa dada yangu Mheshimiwa Judith, Waziri mchapakazi kabisa kwamba, uzalendo na utendaji wake mzuri wa kazi ambao ninajua ameurithi kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, umeimarisha diplomasia ya mabunge na juzi Bunge lako limeweza kutoa mtu ambaye amechaguliwa kuwa Katibu wa Maziwa Makuu katika Ukanda wa Nchi 12.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nampa taarifa mdogo wangu Judith kwamba diplomasia aliyoimarisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Kimataifa umeirithi kuiimarisha kwenye mabunge ya Afrika na Dunia, jambo lililopelekea Tanzania juzi kupata nafasi ya kushinda kiti cha Katibu wa Maziwa Makuu katika ukanda wa Afrika, ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Judith Kapinga, unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa nzuri ya kaka yangu Mheshimiwa Kingu. Naomba niendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Kamati, kwa kweli tumefanya kazi vizuri na tunaendelea kuishukuru kwa miongozo yao ambayo imekuwa ikitupatia wakati wote.
Mheshimiwa Spika, jana wakati tumeanza kuchangia bajeti hii, kwa kweli Waheshimiwa Wabunge kuanzia jana mpaka leo tumewasikia vizuri sana, nami ningependa kipekee niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli michango yao imegusa mioyo yetu, pongezi walizozitoa kwa Mheshimiwa Rais, kwa kweli ni michango yenye uungwana mkubwa sana kwa kazi nzuri iliyofanyika katika Serikali ya Awamu ya Sita; na sisi Waheshimiwa Wabunge kwa kweli hatuna la kuwalipa zaidi ya kuwatakia mema kuelekea 2025 mwaka huu muhimu. Ninaamini wote tutarudi hapa Novemba na tutaapa tena hapa na tunawatakia kila la heri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru Watendaji wetu Wizarani; Katibu Mkuu pamoja na Naibu Makatibu Wakuu, Wenyeviti wa Bodi, Wakuu wa Taasisi na Wafanyakazi wengine wote ambao tunafanya kazi kwa pamoja katika Wizara ile ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, ninapomalizia sehemu yangu ya kwanza ya utangulizi, wakati ninaanza kazi yangu ya Unaibu Waziri ambayo nimepewa dhamana na Mheshimiwa Rais na ninamshukuru sana kwa kuniamini kwa nafasi hiyo, kazi hii nimeifanya vizuri sana kwa sababu ya kiongozi mahiri, mwalimu mwema ambaye anatuongoza wote katika Wizara ya Nishati Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko.
Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nimshukuru sana bosi wangu Mheshimiwa Waziri kwa miongozo ambayo amenipa kwa kipindi chote hiki ambacho nimekuwa Naibu Waziri. Nimekuwa bora sana kwa sababu nipo chini ya kiongozi kama yeye ambaye kwa kweli anapenda hata sisi wa chini wake tuendelee kuwa bora. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa namna ambavyo anaendelea kutuongoza vizuri Wizarani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kumaliza hayo ya utangulizi na shukrani, naomba sasa nijikite kwenye kueleza baadhi ya hoja ambazo zimeongelewa hapa na Waheshimiwa Wabunge. Mojawapo ya masuala ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyaongea kwa nguvu sana ni kuhusiana na ile mikoa ambayo bado haijaunganishwa katika gridi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumesikia Waheshimiwa Wabunge kutoka katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Rukwa, Katavi pamoja na Mkoa wa Kagera. Nikianza na mkoa mmoja mmoja, katika Mkoa wa Rukwa, Serikali tayari imeshaanza kufanyia kazi. Tunao mradi mkubwa ambao unapeleka umeme katika Mkoa wa Rukwa kwa kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Iringa - Tunduma hadi Rukwa, na vilevile kujenga kipande ambacho kitatuunganisha na Zambia.
Mheshimiwa Spika, mradi huu sio kwamba tu unapeleka umeme katika Mkoa wa Rukwa, ni mradi ambao unaenda kunufaisha na mikoa mingine ambapo ipo Nyanda za Juu Kusini, kwa sababu inaenda kujenga vituo vya kupooza umeme katika maeneo haya ambapo mradi unapita. Vipo vituo ambavyo vinaenda kujengwa ikiwemo Kisada pale Mafinga, Iganjo - Mbeya, Nkangamo - Tunduma pamoja na Malangali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni mradi ambao pamoja na kwamba unapeleka gridi katika Mkoa wa Rukwa, utatusaidia vilevile kujenga vituo vya kupooza umeme katika namna ya kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, na Rukwa. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Mkoa wa Rukwa, Serikali ipo kazini kuhakikisha kwamba gridi inafika katika Mkoa wa Rukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mikoa ya Mtwara na Lindi, tayari mkandarasi yupo site na tumemsikia Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru Kusini akisema jana, kwamba Mkandarasi alikuwa ameondoka site kwa takribani miezi minne. Mradi wa kupeleka umeme katika Mkoa wa Mtwara na Lindi ni kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Sita. Mkandarasi sasa amerudi site na mradi huu umeanza kwa kujenga njia ya umeme kutokea Songea kwenda Tunduru, Masasi hadi Mahumbika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi, suala la kupeleka gridi katika mikoa hiyo kwa kweli ni suala la kipaumbele na Mkandarasi yupo site. Taarifa njema ni kwamba tarehe 25 tumeanza kulipa fidia katika eneo la Tunduru hadi Masasi, takribani shilingi bilioni 4.6 na eneo lililobakia la Songea kuelekea Namtumbo na Tunduru tutaendelea kulipa fidia hiyo ya takribani shilingi bilioni 2.7. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa mikoa ya Mtwara na Lindi, bado suala la kupeleka gridi katika mikoa hiyo ni kipaumbele na kazi hiyo inaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kagera, kazi pia inaendelea kupitia kujenga njia ya kusafirisha umeme ya Benaco – Kyaka, huko pia miradi ya kupeleka gridi inaendelea. Katika Mkoa wa Katavi kwa kweli mradi upo katika hatua za mwisho kabisa, tunayo imani ndani ya mwezi mmoja maximum grid itakuwa imefika katika Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika Mikoa yote, kazi hii inafanyika na inakamilika katika Serikali ya Awamu ya Sita, ni kuonesha commitment ambayo Mheshimiwa Rais anayo ya kutaka Watanzania wote waendelee kupata umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la kushukuru sana katika Awamu hii ya Sita ndipo ambapo pia na gridi imefika katika Mkoa wa Kigoma. Kwa hiyo, nikuendelea kuwathibitishia suala la kupeleka umeme katika mikoa ambayo haijaunganishwa na gridi ni kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Sita, wakandarasi wapo site na umeme utafika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja ya hoja ambazo zimezungumzwa pia na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusiana na umeme wa visiwani. Tunavyo visiwa takribani 118 ambavyo kwa kweli Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakilalamikia kuhusiana na masuala ya umeme, nami nakubaliana pia.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tumewasikia Wabunge wa Ukerewe wakisema, na ni kweli kabisa kulikuwa kuna visiwa pale takribani 20, kulikuwa kuna mkandarasi anaitwa Jumeme, Serikali ilimwezesha kwa fedha takribani shilingi bilioni 2.1 miaka ya 2017 huko nyuma kwa ajili ya kuweka mifumo jua, lakini sasa mradi ule umekuwa una changamoto kiasi cha kufanya wananchi wasiendelee kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Spika, tumewasikia Waheshimiwa Wabunge, na ndiyo maana Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kupeleka mifumo mingine ya jua ya umeme katika visiwa 118. Visiwa hivyo havitakuwa tu Mwanza, ni visiwa ambavyo vipo katika Mikoa zaidi ya mitano ambayo yote watapelekewa mifumo ya umeme jua, lakini mahsusi kwa ajili ya Ukerewe ambapo Waheshimiwa Wabunge takribani wawili wamezungumza. Ukerewe pale tunao mradi kupitia gridi imara katika awamu ya kwanza ambao unalenga kujenga kituo cha kupooza umeme pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Bunda hadi Ukerewe.
Mheshimiwa Spika, mradi huu upo na mkandarasi amepatikana, tunaendelea kufanyia kazi ili sasa mradi uweze kuanza. Kwa hiyo, kwa ndugu zangu wa Ukerewe tunataka tuwahakikishie kwamba mikakati ipo kwa ajili ya kujenga kituo cha kupoza umeme na njia ya kusafirisha umeme kutoka Bunda hadi Ukerewe.
Mheshimiwa Spika, kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wanatokea katika visiwa vingine vyote, tayari Serikali imetoa fedha takribani shilingi bilioni 9.89 kwa ajili ya kupeleka mifumo ya jua kwa ajili ya kuimarisha umeme. Tutatoa mifumo karibia 20,000 katika visiwa vyote hivi 118. Kwa hiyo, kwa kweli tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia fedha ili wananchi hawa ambao wapo katika visiwa hivi 118 waendelee kupata umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja ya mwisho ambayo ningependa kuizungumzia ni kuhusiana na maboresho ya umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam. Tulisikia Mheshimiwa Mbunge akizungumzia kuhusiana na umeme katika maeneo ya Mbagala pamoja na Temeke. Nami nataka niseme, ni kweli tulikuwa na changamoto ya kukatikakatika kwa umeme, lakini katika kufanyia kazi suala hili katika kituo chetu cha kupooza umeme cha Mbagala kilikuwa kimezidiwa.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa kuna transfoma pale yenye uwezo wa MVA 50, kwa sasa kwa kweli wataalam wetu wanafanya kazi usiku na mchana, tunaweka pale transformer mpya yenye uwezo wa MVA 120 kwa ajili ya kuongeza ukubwa wa kile kituo ili wananchi wa Mbagala, Temeke, Yombo, Mkuranga pamoja na baadhi ya maeneo ya Kigamboni waendelee kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge hususan wale ambao wanatokea katika maeneo ya Mbagala na Temeke pamoja na Yombo, Mkuranga na baadhi ya maeneo ya Kigamboni, kazi hii imefikia mwishoni muda wowote kuanzia sasa transformer ile itaanza kufanya kazi na kwa kweli tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya kukatika katika kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika eneo la Kigamboni kwa kweli tuliwasikia wananchi pia wakilalamika katika feeder yetu ya Mwongozo, Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu alitoa maelekezo na tulitenga fedha pale kwa ajili ya kuboresha matengenezo kinga lakini vilevile maboresho ya voltage, vilevile kubadilisha baadhi ya mifumo kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Kigamboni kupunguza tatizo la umeme. Kazi hiyo imefanyika, na kwa kweli kuna maboresho na uwezeshaji mkubwa sana katika feeder ile ya Mwongozo pale Kigamboni na wananchi kwa kweli wamefurahi kwa mabadiliko hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninapomalizia, kwa mara nyingine tena kazi hizi zimefanyika vizuri sana kwa miongozo ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na ndiyo maana tunaona mafanikio makubwa ambayo yapo katika sekta ya nishati. Tunaendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi ambacho miradi ya umeme hususan ya uzalishaji imekamilika, katika historia ya Taifa letu ni katika kipindi cha Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mheshimiwa Spika, miradi mingi ambayo Waheshimiwa Wabunge wanaisema hapa, Mradi wa Rusumo, Kinyerezi One Extension, Bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingine inayoendelea kama Malagarasi ambayo Waheshimiwa Wabunge wanaisema, ni miradi ambayo imekamilika na ni miradi ambayo inaendelea kutokana na uwekezaji mkubwa na commitment ambayo Mheshimiwa Rais anayo katika sekta ya nishati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninavyomalizia kabisa, tunaendelea kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano ambao mnaendelea kutupatia, nasi tunaendelea kumwomba Mwenyezi Mungu basi atujalie ili tuendelee kufanya vizuri shughuli zetu, vilevile nawatakiwa kila la heri katika uchaguzi ambao unakaribia hapa karibuni.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana, na ninaunga mkono hoja. (Makofi)