Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kutuwezesha kuwepo hapa kwa siku hizi mbili ambapo tumeendelea na mjadala huu muhimu sana unaohusiana na uchumi na maendeleo ya watu wetu, lakini muhimu zaidi katika harakati ya kuwapatia nishati wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijasema lolote, naomba nianze kwa kukushukuru wewe binafsi kwa namna ambavyo umetuendesha kwenye mjadala huu kwa muda wa siku mbili, umekuwa mjadala wa tija sana kwetu kwenye sekta lakini na kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wameona namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge wanazungumza masuala yanayowahusu, toka mzungumzaji wa kwanza hadi wa mwisho, hakuna ajenda waliyokuwa wanaizungumza zaidi ya nishati kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwani kwa hali ya kushangaza kabisa, asubuhi nilivyoacha kukuona hapa, nilijua hutaweza, maana nilikuona kwenye TV ukiwa Dar es Salaam, lakini wakati Mpambe wa Spika anakuingiza humu ndani nilitarajia atasema Mheshimiwa Naibu Spika au Mwenyekiti, nikasikia anaita Mheshimiwa Spika mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni ishara kuwa unaipenda kazi yako na unapenda kuwahudumia Watanzania. Ulikuwa na sababu zote kabisa za kusema kuwa ulikuwa na majukumu mengine, na unao wasaidizi wengi ambao wangefanya hiyo kazi, lakini umeamua kuwahi ili kuja kuhitimisha hoja hii. Kwa niaba ya wenzangu Wizarani tunakushukuru sana kwa heshima hiyo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge imeonesha ukubwa wa sekta hii namna ilivyo muhimu katika maendeleo ya uchumi, maendeleo ya kijamii na pia namna wananchi kupitia Wawakilishi wao walivyo na kiu ya kuona huduma zinazotolewa katika Wizara na Taasisi zake hususan upatikanaji wa nishati ya umeme gesi pamoja na huduma nyinginezo zinawafikia kikamilifu na kutatua changamoto zinazowakabili.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, nitumie fursa hii kusema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati itahakikisha kuwa ushauri na maoni yote tuliyoyapata kutoka kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge yanafanyiwa kazi kwa haraka.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa mchango wake kwenye hotuba yetu ya bajeti ya mwaka 2025/2026, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hotuba hii kwa kauli na kwa maandishi. Tumeona Waheshimiwa Wabunge waliochangia jumla ni 49. Waliochangia kwa kusema ni 42 na Waheshimiwa Wabunge saba wamechangia kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika, niendelee kusema kuwa mchango yao yote waliyoitoa tutaizingatia. Tupo katika kujenga nyumba moja na hatuwezi kuendesha hii sekta peke yetu, tunahitajiana wote wakati wote, nami nataka nitoe ahadi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba yote waliyosema Waheshimiwa Wabunge tutakwenda kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, naomba sasa nitoe ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia. Aidha, niseme kuwa hoja zote tutaziandalia majibu ya maandishi na kuziwasilisha kwenye Ofisi yako kwa ajili ya rejea yako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza iliyozungumzwa kwa nguvu sana na Waheshimiwa Wabunge ni Mradi wa LNG, umeanza kusemwa kwa muda mrefu, kila mmoja angetamani mradi ule ukamilike jana; lakini mradi huu pamoja na kuanza muda mrefu, tukubaliane kuwa lazima tujadiliane ili tupate kilicho bora. Tunatamani mradi huo uwepo, lakini majadiliano haya ni lazima yatupe tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtakumbuka hapo nyuma Serikali baada ya kukamilisha majadiliano awamu ya kwanza ilirudisha majadiliano hayo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kupata maoni. Baada ya kupita kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ukweli ni kwamba kuna maeneo mengi ambayo yalikuwa wanahitaji kufanyiwa kazi zaidi ili kupata mkataba ulio mzuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, leo tunaweza kusema mradi huo uanze, lakini nataka niseme kwamba mkataba ulio mzuri leo, kesho unaweza kuwa mkataba mbaya. Nchi hii ina historia ya kupita kwenye mikataba hiyo inayolalamikiwa. Tumejifunza mengi kwa safari toka tumeianza extractive kwenye nchi yetu, yapo mambo na maeneo kadhaa ambayo ni lazima yafanyiwe kazi kabla ya mkataba huo kusainiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kukuhakikishia ni kuwa Serikali pamoja na wawekezaji, timu zinaendelea na majadiliano ili kuondoa changamoto zilizopo ambazo zimebaki chache sana na tunatarajia kuwa ndani ya mwaka huu 2025, kama tutakuwa tumemaliza mambo matatu yaliyosalia, nataka nikuhakikishie kuwa mkataba huo utasainiwa na mradi huo uanze mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge, naomba mtupe muda. Tunajua kuwa hili jambo linahitajika kwanza kwa uchumi wa nchi yetu, lakini kwa maendeleo ya watu wa Mikoa ya Kusini ambako gesi ipo. Ingekuwa ajabu sana siku moja tuingie mkataba, tumekubaliana na mwekezaji ndani ya mkataba ule, mwekezaji awe ameruhusiwa local content ya Tanzania isitumike, hakuna mtu angetuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna mtu angetuelewa kwamba bima zote ambazo zinatakiwa ku-cover huu mradi zote zitoke nje ya nchi bila ushiriki wa Watanzania; hakuna mtu ambaye angetuelewa kwamba tutachimba gesi, lakini domestic gas, yaani gesi ya matumizi ya ndani iwe angalau asilimia tatu, hakuna mtu angetuelewa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, yapo mambo mengi ya kiuchumi na ya kisheria ambayo tunayapitia. Jambo la kutia moyo ni kwamba wawekezaji wetu hawa tumekubaliana mengi sana, yaliyobaki ni machache, na hivi ninavyozungumza timu zetu zipo Arusha zinaendelea na hayo majadiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikuhakikishie, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati ananiteua kuwa Waziri wa Nishati aliniambia angetamani sana kuona mradi huu unakamilika kabla hatujaenda kwenye uchaguzi. Nataka nirudie hilo, mwenye kiu namba moja ya kuona mradi huu unakamilika ni yeye mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Spika na Ndugu zangu wa Mtwara na Watanzania pamoja na watu wa Lindi, naomba tuwe na subira, tunahitaji kilicho bora. Isingefaa leo tupitishe mkataba, na baada tu ya kupitisha mkataba tuanze kujitetea tena kwa miaka yote maisha yote mpaka mkataba uishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mikataba mingi tuliyopitia mnaifahamu, ambayo ilikuwepo baada ya kuwa imefungwa ina maisha ya miaka 20 huwezi kuivunja, tumebaki kulalamikiana humu ndani kuunda Kamati na kadhalika, lakini mkataba upo. Makosa ambayo tuliwahi kuyafanya huko nyuma, nafikiri ni muda muafaka sasa kuyarekebisha na kupata kilicho bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili, iliyozungumzwa ni ongezeko la vituo vya mafuta vinavyojengwa karibu karibu. Kanuni ya viwango vya upangaji miji za mwaka 2015, iliyotengenezwa chini ya Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355, inaelekeza kuwa umbali wa mita 200 kutoka kituo kimoja hadi kingine kama vituo hivyo vipo upande mmoja wa barabara na kama vituo hivyo vipo pande tofauti wa barabara, umbali huo unakuwa unatengenisha vituo hivyo.

Mheshimiwa Spika, kutokana na wasiwasi ambao umekuwa ukioneshwa na Waheshimiwa Wabunge na wananchi kuhusu ongezeko la vituo hivyo vya mafuta kuwa karibu sana kutoka kituo kimoja hadi kingine, Wizara ya Nishati imeanza mazungumzo na Wizara ya Ardhi ili kubadilisha kanuni hizo ili kuwezesha kuongeza walau umbali kidogo unaotakiwa kati ya kituo kimoja na kingine kwa kuzingatia masuala ya afya, usalama mazingira na shughuli za kijamii. Hili jambo lipo kwenye sheria, kwa hiyo, tunalifanyia kazi tuone namna gani tunaweza kuichukua michango ya Waheshimiwa Wabunge? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameeleza haya mambo kwa uzito mkubwa sana, hatuwezi kuyachukulia kwa wepesi tukayaacha yakapita. Nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, toka tumeanza kwenye Kamati, Kamati yenyewe ilikuwa na msukumo mkubwa wa jambo hili. Tayari tumeshaanza kazi ya kuzungumza na Wizara husika ili hili jambo lipitiwe tuweze kurekebisha jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa msamaha wa kodi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa CNG katika matumizi ya vyombo vya moto ikiwemo magari. Serikali ilishatoa msahama wa kodi ongezeko la thamani (VAT) kwa vifaa na mashine mbalimbali zinazotumika katika mnyororo wa thamani kwa miradi ya CNG na matumizi ya magari.

Mheshimiwa Spika, mashine na vifaa hivyo pamoja na mashine nyingine zinazotumika katika ujenzi wa vituo hivyo vyote hivi, vina msamaha wa kodi ya VAT. Mitungi ya CNG pamoja na vifaa vya kufunga mfumo wa kuwezesha magari kwa kutumia CNG vyote vina msamaha wa kodi wa VAT. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Wizara imewasilisha Wizara ya Fedha mapendekezo ya maboresho ya VAT katika gesi asilia ambayo inatumika katika magari ili kuhamasisha matumizi ya CNG kwenye magari ili wawekezaji waweze kupata faida na waweze kurudisha gharama wanazowekeza kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imeombwa vilevile kupitia Bunge hili kuwa, ilekeze nguvu zaidi katika uzalishaji wa umeme wa joroardhi na vyanzo vingine vya umeme. Nakubaliana kabisa na Waheshimiwa Wabunge, kwanza ni hatari kuwa na chanzo kimoja cha umeme pekee yake, lakini pili chanzo cha maji kinaweza kukumbwa na changamoto yoyote kama ambavyo hata chanzo cha gesi kinaweza kukumbwa na changamoto yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano mzuri tumeuona kwa wenzetu wa Zambia, walikuwa na umeme wa kutosha lakini wakapata ukame misimu miwili mfululizo uliowapeleka kwenye mgao. Kwa kulifahamu hilo, Serikali imeamua kwa makusudi kuchukua hatua ya kuongeza vyanzo mbalimbali. Ndiyo maana mtaona kwenye hotuba yangu nimeeleza vyanzo mbalimbali ambavyo tunaviendeleza mbali na vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo Kampuni ya TGC ambayo ilianzishwa mwaka 2013 na kuanza rasmi mwaka 2014 inaendelea na kufanya utafiti kwa ajili ya kuongeza reserve ya jotoardhi ili tuweze kuendeleza miradi hiyo. Tunayo maeneo zaidi ya 50 nchini kwetu ambayo yamebainika kuwa na joroardhi. Nataka nieleze miradi ya jotoardhi kwa asili ina sifa mbili. Moja, inahitaji muda mrefu sana wa utafiti, lakini pili inahitaji mitaji mikubwa ya uwekezaji.

Mheshimiwa Spika, wamejaribu wenzangu kueleza hapa Waheshimiwa Wabunge kwamba tuige mfano wa Kenya kwamba wao wanatumia jotoardhi. Ni kweli, lakini Kenya walianza lini, na miradi ya jotoardhi? Mara ya kwanza nchi ya Kenya kuanza miradi ya jotoardhi ilikuwa mwaka 1950. Wamekuja kupata plant ya kwanza mwaka 1981 miaka 31, maana yake ni kwamba hizi ni project ambazo ni capital intensive na time intensive huwezi kuanza leo kesho ukaipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linalotutia moyo kwetu sisi, pamoja na kwamba tumeanza mwaka 2013, tumeshapiga hatua ya mbali sana. Hapa ninaposimama tayari mkandarasi wa kufanya drilling yupo site na tayari reserve ile imeshaonekana. Nataka niwaeleze, hata kwenye bajeti hii tunayoiomba leo ni kwa ajili ya kazi hii. Tumeomba shilingi bilioni 34 ambazo tumetenga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya geothermal.

Mheshimiwa Spika, potential tuliyonayo kwenye nchi yetu kwenye miradi ya geothermal ni Megawati 5,000, maana yake Megawati 5,000 ni mradi mkubwa ambao Julius Nyerere inaingia karibu au zaidi ya mara mbili. Nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge miradi hii mkubali kwamba tunaendelea nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu umeme jua, kwa mara ya kwanza kwenye nchi yetu hatukuwahi kuwa na mradi mkubwa wa solar. Sasa hivi tunajenga mradi wa Kishapu Megawati 150 ambao ujenzi wake na utekelezaji wake upo 51%. Serikali inakaribisha sekta binafsi nyingine katika Mfumo wa IPP, wale wanaotaka kuja kujenga miradi ya solar waje, tunawakaribisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja tuliyoiona hapa ni tariff. Wengine wanakuja na tariff ya senti 24 hakuna mtu atanunua umeme huo. Hapa Bunge zima linazungumza umeme tunaouza bado ni ghali, akija mwekezaji anataka kuleta umeme kwa tariff ya senti 15, 20, haiwezekani, tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie kuwa miradi hiyo tunaendeleanayo kwa wingi. Miradi ya upepo kwa mfano, mradi wa jua hapa Zuzu megawati 130; Singida, Manyoni megawati 100, Same megawati 100, Singida, Ikungi ya kutumia upepo megawati 100. Hii yote ni miradi ambayo tunaifanyia kazi. Tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtukubalie tuendelee kufanya hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wameeleza kwa uchungu sana kuhusiana na kupeleka umeme vitongojini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Ibara ya 63, Kifungu Kidogo cha (b), kimeeleza hivi, “kukamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote na maeneo ya pembezoni mwa Miji ya Tanzania Bara kupitia mpango wa umeme vijijini, pamoja na kuandaa mpango kabambe wa umeme vijijini (Rural Energy Master Plan) kabla ya Mwaka 2025.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama kuna eneo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anapaswa kupongezwa sana ni eneo hili. Nasema hivyo kwa nini? Chama cha Mapinduzi mkataba wake na wananchi mpaka kufika 2025 haukuwa vitongoji, ulikuwa ni vijiji tu. Vijiji vimemaliza kabla ya wakati na kabla ya wakati imehamia vitongojini, na vitongoji 64,000 vitongoji 33 vyote vina umeme. Yaani kwa maneno mengine Chama cha Mapinduzi kimefanya kazi mpaka ikapitiliza kile ilichoahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeweza kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote 12,318 sawa na vile ilivyoahidi kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2020. Aidha, katika Ilani ya Uchaguzi 2020, malengo tuliyokuwa tumewekewa sisi ya kuhakikisha kuwa, maeneo ya pembezoni tunayapelekea umeme, Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza, visiwa 181 vyote vile tunapambana kuvipelekea umeme katika kipindi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kuwa mpango tulionao kwa sasa ni kwamba tunaendelea na mpango wa kuongeza vitongoji 9,000 ambavyo vimetangazwa, na wakandarasi wameshapatikana. Nataka niwahakikishie kuwa, hatujui Ilani ya Uchaguzi itatueleza nini baadaye? Sisi tumeanza hata kabla ya hiyo ilani kupeleka umeme vitongojini, ili wananchi waweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maelekezo yake kwenye kupeleka umeme. Hili labda niwape ushuhuda Waheshimiwa Wabunge kuwa katika kitu kimojawapo kilichofanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Energy Summit Africa na kuwaleta wakuu wa nchi wote Afrika, tulivyopimwa na World Bank, nchi iliyoongoza kwa kupeleka umeme vijijini tulikuwa sisi, Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpango wa kupeleka umeme kwa wananchi kupitia kile kinachoitwa Mission 300, mpango unaochukuliwa kwa mfano, ni Mpango wa Tanzania. Hivi ninavyozungumza hapa, Katibu Mkuu wetu alikuwa Marekani, kwa ajili ya kupeleka mpango wetu kwenda ku-present, maana hiyo ndiyo model inayotumiwa na wengine. Inawezekana hapa ndani tukajidharau, lakini huko kwingine nje wanatuona sisi ni wakubwa mno, tunahitaji kuigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tembeeni kifua mbele, tembeeni mkijiamini kuwa Sekta ya Nishati ipo mikono salama chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, na sisi wasaidizi wake hatutamwangusha kwenye jambo hili. Tutasimama wakati wote kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata umeme. Huwa ninawaeleza wenzangu kwenye sekta ya nishati, kama kuna sekta haihitaji kusema sana ni hii ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeme ukikatika huhitaji maelezo, umekatika. Hayo maelezo mengine baki nayo, watu wanachotaka ni umeme, basi. Hata ungekuja na misamiati yoyote unayoijua, ukajieleza kwa ufundi unaoujua, kama watu hawaoni umeme ni kama tu unapiga gitaa kwa wimbo ambao watu hawaujui. Nataka nikuhakikishie kuwa, tutahakikisha kwa kila linalowezekana kazi ya kupeleka umeme inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imeelezwa kwa uchungu sana, bei ya kuunganisha umeme kwa wananchi vijijini na mijini na mapendekezo yaliyotolewa na kamati. Labda nieleze la kwanza, kwamba, Serikali bei ya kuunganisha umeme kwa sasa ni shilingi 97,000 kwa maeneo ya vijijini na vijiji miji. Serikali inaendelea kuunganisha umeme kupitia mpango mahususi wa nishati (National Energy Compact) kwa mwaka wa fedha 2025/2026, yaani bajeti hii tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia REA imetenga shilingi bilioni 40, ili kuanza kuunganisha umeme wa wananchi kwa shilingi 27,000 katika maeneo mbalimbali yenye sura ya vijiji miji. Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya wastani wa 58% ya gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi, lakini wananchi hulipia kiasi fulani ambacho bado Wabunge wamesema ni kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwa tumejadili jambo hili kwa kina kwenye Kamati tuliamua kuunda Kamati kwa sababu, hili ni jambo linalohusiana na uchumi na linahusiana na fedha, haliwezi kutamkwa bila uchambuzi. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa heshima na unyenyekevu mkubwa mtupe muda. Tuna timu tumeiunda ya kwenda kuangalia namna gani tutapunguza gharama ya kuwaunganisha wananchi vijijini kwa ajili ya kuwapelekea umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, kwenye Mradi wetu wa Compact ambao Benki ya Dunia, FDB, wanatufadhili pamoja na wafadhili wengine. Tumepewa target ya kuunganisha wateja milioni nane, ukijumlisha na wale waliokuwepo, milioni tano, tunatakiwa itakapofika mwaka 2023 tuwe tumeunganisha wateja zaidi ya milioni 12.

Mheshimiwa Spika, sasa tumeambiana Wizarani kuwa, kwa hali ya kawaida, kama tumeunganisha wateja 5,200,000 kwa kipindi chote toka tumekuwepo, ni muujiza gani huu tutakaokuwanao wa kuwaunganisha wateja milioni nane ndani ya miaka mitano? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba, lazima kuwe na utaratibu ambao siyo wa kawaida uliozoeleka, tuliokuwa tukiufanya miaka yote katika uunganishaji wananchi. Mojawapo ni kuangalia ni kitu gani kinachowakwamisha wananchi kuunganishwa na huo umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kila Mbunge ameeleza hapa kwamba, moja ni gharama, lakini pili ni hizi gharama zote hawaziwezi wananchi. Tumeunda hiyo timu ikatufanyie uchambuzi ituletee majibu na ninaamini wakati fulani tutawahusisha na Waheshimiwa Wabunge, ili mweze kujua ni kitu gani mnachokifanya.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie kuwa, tunalifanyia kazi jambo hili, ili uunganishaji uweze kuwa rahisi na hili linalozungumzwa la watu kuweza kuunganishiwa umeme kwa bei nafuu tutalifikia. Niunganishe hilo hilo pamoja na gharama za umeme. Gharama za umeme (tariffs) kwenye nchi yetu hazijapitiwa kwa muda wa miaka 10. Kwa sasa tunazipitia kupitia EWURA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, naomba mnikubalie, kwamba jambo hili ni la kiuchumi, ni la kisayansi, linahitaji uchambuzi na kuwashirikisha wadau mbalimbali watoe maoni yao. Naomba tuwape nafasi EWURA, kama regulator independent afanye kazi yake bila kumwingilia, ili atuletee taarifa hizi za gharama ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni nini, na nini kifanyike, ili wananchi waweze kupata nishati ambayo inahimilika? Kwa hiyo, hili na lenyewe tunalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imeelezwa hapa habari ya vituo vya kupooza umeme, ili kukabiliana na changamoto ya kukatika umeme. Serikali ilikuja na Mpango wa Gridi Imara kwa kujenga vituo vya gridi vya kupooza umeme kwa kila wilaya. Hatua zifuatazo zimechukuliwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja, tumeshanunua viwanja, kwa ajili ya kujenga vituo, kwa ajili ya wilaya zote nchini. Pili, tumeamua kujenga kwanza vituo 14 vya kuanzia na Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, Wakili Olelekaita, ni mmojawapo wa watakaoanza kujengewa katika awamu ya kwanza, lakini utekelezaji utaendelea katika wilaya nyingine kadiri tunavyoendelea na wilaya nyingi zinahakikishiwa kuwa, tunazijengea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunahitaji vituo 216 vya kupoozea umeme katika nchi yetu. Vilivyopo ni vituo 132. Maana yake ni kwamba, tuna upungufu wa vituo 84. Kituo cha kupoozea umeme cha grid (grid substation), gharama ya kujenga kituo kimoja ni shilingi bilioni 35, it’s expensive na kituo cha kawaida, kile kinachopokea umeme kwenye msongo wa kilovoti 33, kituo kimoja ni shilingi bilioni nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba, zinahitajika fedha nyingi ili tuweze kujenga. Hatuwezi kufanya vyote mara moja, tunachohitaji ni mahali pengine tutaweka switching station, ili tugawanye njia. Kwa mfano, pale Mto wa Mbu kwa sababu, ile line ya kutoka Arusha kwenda mpaka Ngorongoro ni ndefu sana, ile line peke yake ina urefu wa kilometa 1,400. Maana yake ni kwamba, line yote ile haina substation, haina chochote, hata akitokea mtu anaendesha gari akagonga nguzo moja, maana yake ni wote walio upande mwingine wanakosa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeamua kuweka mkakati maalumu wa kuweka switching station kwenye maeneo ambayo tunadhani ni nafuu, ili tuweze kutenganisha hizo njia, watu waweze kupata umeme. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, hasa wa Mkoa wa Lindi, nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa Kuchauka, ni kweli, Lindi kule wanachukuwa umeme kutoka kwenye Kituo chetu cha Makumbika, ni mbali sana. Ukienda Liwale kwa Mheshimiwa Kuchauka umeme unakatika sana. jamani Waheshimiwa Wabunge, umeme haukatiki kwa sababu, hakuna umeme, unakatika kwa sababu ya miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwape taarifa ndogo. Juzi tumezindua Taarifa ya EWURA hapa, wakati tumezindua ile Taarifa ya EWURA tumeonesha kwa mwaka mmoja tatizo la kukatika umeme limepungua kwa kiasi gani? Hili tulikuwa tunazungumza mpaka tunakuja kumaliza mwaka 2024. Kukatika kwa umeme katika nchi yetu, kwa Taarifa ya EWURA iliyofanyiwa utafiti, kumepungua kwa 48% na dakika za kukatika umeme zimepungua kwa 64%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipotoka hali ilikuwa mbaya zaidi kuliko tulipo hivi sasa. Sehemu nyingi ukiona umeme unakatika ni mahali ambapo tunatengeneza miundombinu. Lazima tukubali kwamba, hatuwezi kula keki na tukabakinayo. Wakati tunajenga hii miundombinu ni lazima tutazima umeme mahali fulani, ili tuweze kujenga hiyo miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tumetoka kwenye dakika 1,536 mwaka 2022 mpaka dakika 5,554 mwaka 2024, tumepunguza kukatika kwa umeme kwa 68%. Naomba mtuamini kuwa, hili jambo tunalifanyia kazi, tena hakuna jambo linawakera wananchi kama kukatika umeme, hasa kama hawajapewa taarifa. Ndiyo maana tumeamua kituo chetu cha huduma kwa wateja tukiimarishe, umeme unapokatika watu wapewe taarifa.

Mheshimiwa Spika, tulizoea kutoa tangazo tu mara moja, tunawapa taarifa kuwa umeme umekatika kwa sababu hizi na hizi. Tumeamua, kila wilaya, kila Mkoa, kuwe na ma-group ya WhatsApp, meneja kazi yake awe admin kwenye yale ma-group kuwapa taarifa watu maana siku hizi wananchi, hata mimi wananiandikia message. Umeme ukikatika wanakuandikia message. Natamani sana waendelee kufanya hivyo kwa sababu, kwa kufanya hivyo, wanatu-hold accountable kila mmoja kujua wajibu wetu, kuwapatia umeme Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo moja lenye upekee ambalo nimelisikia hapa ni kuhusu transformer tano ambazo zimeungua, Ngara. Imenisikitisha na ikaniogopesha kwamba, transformer tano zinaungua halafu hatujafanya kazi. Baada ya kufuatilia pia, nimegundua kuwa, mkandarasi aliyepewa hizi transformer zilikuwa chini ya uangalizi wake kwa hiyo, alipewa wajibu wa kuzibadilisha ili aweke transformer nyingine.

Mheshimiwa Spika, nimewaelekeza leo TANESCO kwamba, sisi tupeleke hizo transformer, wananchi wasihangaike, halafu ninyi TANESCO mdaiane na huyo mkandarasi. Kwa sababu hiyo, wananchi wa Ngara ndani ya wiki hii mpaka wiki inayokwisha transformer zote zile ziwe zimebadilishwa na wananchi wapate umeme bila matatizo yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni upungufu wa wafanyazi ambao Waheshimiwa Wabunge wameueleza. Nataka kutoa taarifa tu kuwa, tumepata kibali cha kuajiri watumishi 570 kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Utaratibu unakamilishwa watumishi hao waweze kupangiwa majukumu hayo. Vilevile Serikali imepanga kuajiri watumishi wengine 1,000 katika mwaka wa fedha 2025/2026, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi kwenye maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kadiri tunavyoendelea kusambaza umeme ndivyo mahitaji ya watu wa kuhudumia hizo line yanavyoongezeka. Kwa hiyo, tumepata nafasi ya kuajiri watu wengi zaidi ili tuweze kufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, nimezungumza suala la vitendea kazi, hususan magari, ili kupunguza changamoto ya usafiri huo katika Wilaya za ki-TANESCO mwaka huu wa 2024/2025. Serikali imefanya manunuzi ya magari 50 ambapo magari haya yamesambazwa katika mikoa na wilaya zenye uhitaji mkubwa. Magari hayo yanatarajia kupelekwa mwezi Agosti na aidha itakapofika Septemba, 2025 magari haya yatakuwa yamefikishwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwenye mwaka huu wa fedha, kwenye bajeti hii tunayoomba, TANESCO imetenga fedha za kununua magari 200, ili kuendelea kupunguza changamoto hii ya kuwapatia huduma wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo machache nilitaka nichangie na kujibu hoja kwa Waheshimiwa Wabunge, lakini nimalizie kwa kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwamba, mmetutendea wema mwingi mno kwa kutusimamia na kutushauri. Nawashukuru sana na kwa kweli, nawaombea kwa Mungu, kila mmoja aliyemo humu, wananchi wake mahali popote walipo, waangalieni Wabunge hawa kwa jicho la wema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kama kuna mtu anapewa kazi, kwa kawaida anadaiwa hesabu mikononi mwake. Waheshimiwa Wabunge hawa hawadaiwi kwa sababu kazi wameifanya, wamezungumza, wengine wakati wanaingia kwenye uongozi walikuwa na maeneo hayana umeme, wamesema hapa vijiji vyote vina umeme.

Mheshimiwa Spika, kama walikuwa wanasema kuna maeneo hayakuwa na zahanati na vituo vya afya, wanaeleza wakiwa Bungeni, sasa vijiji hivyo vina zahanati na vituo vya afya. Kama walikuwa wanasema kuna maeneo hayakuwa na high school, wakiwa humu Bungeni, sasa wanasema maeneo yao yana shule na high school. Kama walikuwa wanasema, wanatamani kujengwe Vyuo vya VETA kwenye maeneo yao, wakiwa kwenye nyumba hii, kunajengwa Vyuo vya VETA kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama walikuwa wanasema, wananchi walikuwa wanahangaika na ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo, pamoja na usimamizi mzuri kwenye sekta ya kilimo, wakiwa kwenye nyumba hii, leo wanasema ruzuku ya kilimo inapelekwa. Kama walikuwa wanasema mitandao ya barabara ilikuwa kidogo kwenye maeneo yao, wakiwa kwenye nyumba hii, wanasema mitandao imeongezeka na wanahitaji fedha zaidi barabara ziboreshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wamefanya kazi yao, ikiwa mwanadamu hataona, basi mbingu zitaona. Nawaombea Waheshimiwa Wabunge kwamba, tembeeni kifua mbele mkiamini kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuijenga hii nchi, tena siyo kwa maneno. Mheshimiwa Rais anapenda kusema kidogo na kutenda zaidi. Ametufundisha falsafa, “nia njema haishindwi.” Tembeeni mkiwa na nia njema ya kuwahudumia Watanzania, nami ninaamini kwa sababu, nia njema haishindwi, ninyi mtaibuka washindi na Mungu awasaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa wananchi wa Mbeya, hatuna cha kuwafundisha, mnajua cha kufanya. Mshairi mmoja alisema, “usione, ukadhani.” Nafikiri wakati fulani watu wa Mbeya walikuona wakadhani, lakini umethibitisha sio Tanzania, lakini na dunia kwa ujumla, kwamba Tanzania, nchi mojawapo katika Ukanda wa Afrika Mashariki inaweza ikamzaa binti, ikamlea, ikamsomesha, ikamfanya kuwa mtu wa msimamo wa kipekee.

Mheshimiwa Spika, umelithibitisha hilo kwenye Mabunge ya Dunia. Umetupa heshima Watanzania. La muhimu zaidi umempa heshima mtoto wa kike wa nchi yetu. Tunawaomba watu wa Mbeya, kama kuna jambo mlilowahi kufanya jema ni kutuletea Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson na kama kuna jambo Chama cha Mapinduzi kiliwahi kufanya ni kumteua na kumleta tumchague, Dkt. Tulia Ackson kuwa Spika wa Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajifunza mengi kwako pamoja na wasaidizi wako, Mheshimiwa Zungu na Wenyeviti wote wa Bunge hili, kwa namna mnavyotuendesha. Kwa kweli, mahali ambapo kanuni zinakiukwa unakuwa mkali, hata kama ni rafiki yako huangalii uso wa mtu, lakini mahali ambapo mtu anahitaji haki, anaipata. Tunawatakia kila la heri viongozi wetu wa Bunge hili, mwendelee kutusimamia vizuri na sisi kama Wabunge tulio kwenye nyumba hii tutaendelea kuwaombea na kuwatakia kila la heri ili kazi yenu iweze kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho ambalo nilitaka niliweke vizuri, kuna mkanganyiko mdogo umetokea wakati wa michango ya Waheshimiwa Wabunge. Kutenganisha kati ya gesi ya LPG na natural gas. Niliona clip moja ya mtu mmoja, nazungumza Watanzania ni kama hatuna akili. Gesi ipo hapa Mtwara, mnaenda kununua gesi ya kupikia India na mahali kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nadhani ni suala la uelewa tu. Natural gas na LPG ni gesi mbili tofauti zenye matumizi mawili tofauti, na zenye chemistiry mbili tofauti. Sasa kwa sababu, mimi pamoja na kwamba, ni Mwalimu, siyo kazi yangu kusimama hapa na kufundisha. Naomba unikubalie, unitengee siku moja wataalamu wangu wafanye semina kwa Wabunge wote, ili tujue tu tofauti ya LPG pamoja na natural gas, ili tuone tofauti hiyo ipoje, halafu tuweze kuichangia zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa nafasi, naomba kutoa hoja. (Makofi)