Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa heshima uliyonipa ili niweze kuwa mchangiaji wa kwanza mchana huu katika Wizara hii ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri na mimi kama Mbunge wa wananchi wa Jimbo la Lupembe ukisoma katika bajeti hii ya Wizara ya Katiba na Sheria utabaini kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya reforms kubwa sana katika sekta ya sheria hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Naibu Waziri wake Mheshimiwa Jumanne Sagini, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, SG, AG wetu na DPP kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya chini ya Wizara hii ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwenye hotuba hii; miongoni mwa maeneo ambayo Mheshimiwa Rais amekuja na maono makubwa ya kuwasaidia Watanzania ni pamoja na kampeni maalum ya Mama Samia Legal Aid. Sisi Wabunge wa vijijini ambao tunajua changamoto za wananchi wetu, ambapo wapo wananchi wengi hawana uwezo wa kuzifikia Mahakama kwa sababu ya umbali pamoja na gharama za kutafuta mawakili kuwa kubwa na pia wapo wanananchi ambao hawajui taratibu za kupata haki zao; Kampeni hii ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign) imekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, tumemwona katika nchi yetu kwenye mikoa mbalimbali akiongoza kwa vitendo kampeni hii; na nimhakikishie Mheshimiwa Waziri, katika awamu yake ameifanya Wizara ya Katiba na Sheria kuwa karibu zaidi na wananchi wa Tanzania. Hongera sana kwake na timu yake yote ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka pia nitoe ushauri kidogo katika eneo hili la msaada wa Mama Samia wa Kisheria. Ili huduma hii iweze kuwa endelevu, pamoja na mipango mizuri ya Wizara hii ninaishauri sana Serikali, wako watu kwenye mikoa na wilaya wanaitwa paralegal; hawa watu wana NGO mbalimbali. Ninataka nimwombe Mheshimiwa Waziri kwamba atakapokuja ku-wind up jioni atuambie wana mpango gani wa kufanya ushirikiano wa kutosha kuwasaidia paralegal hawa kuwajengea uwezo wa mafunzo na kuwasaidia vitendea kazi ili huduma hii ya Mama Samia iweze kuwa endelevu leo na vizazi vijavyo. Kwa mfano, Jimbo la Lupembe tunao watu wa paralegal pale Nyombo wanaitwa Nyomapace wakiongozwa na mzee wangu Joakim Mwinami pamoja na Lucas Payovela.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda pia kwenye Mkoa wa Njombe tunao watu wa paralegal kwenye taasisi kubwa ya Mapao ikiongozwa na Mchungaji Sinene. Hawa watu wanahitaji kujengewa uwezo sana kupitia Wizara hii. Nimwombe Mheshimiwa Waziri atusaidie. Wengi hawana vifaa kama computer na hawana usafiri pia. Tukiwasaidia hawa, kwa kuwa wapo karibu na wananchi wataifanya huduma hii kuwa endelevu na kuwa na msaada zaidi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ninataka nitumie nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lupembe kutoa shukrani maalumu kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga Mahakama ya Mwanzo kwa zaidi ya shilingi bilioni moja pale Lupembe Barazani. Mahakama ya Lupembe pale Bararazani ilikuwa imechakaa sana na ilikuwa inavuja lakini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametujengea mahakama mpya ambayo itahudumia wananchi wa kata saba za Jimbo la Lupembe. Wananchi Idamba, Mfiriga, Lupembe yenyewe, Matembwe, Ukalawa, Ikondo hadi Kidegembye. Watapata huduma bora katika Mahakama ya Mwanzo ya Lupembe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri na Wizara husika, pia nilishatoa ombi kwa wananchi wa Tarafa kubwa ya Makambako ambao wanaomba kupata Mahakama ya Mwanzo pale Mtwango Barabarani. Mheshimiwa Waziri anapafahamu; anapita kila siku pale, umeshakuwa mji. Wananchi hawa kuna kata tano kubwa wananchi hawa: Kata ya Mtwango, Kichiwa, Ninga, Ikuna, na Igongolo. Wote hawa wanafuata mahakama mbali kule Mkoani Njombe au Makambako. Wanaomba Mahakama ya Mwanzo eneo hili ili wapate ukjaribu wa huduma za kisheria na mashauri yao yaende kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia nitumie nafasi hii kuiomba sana Wizara hii iendelee kutoa elimu kwa Watanzania kwamba haki ya kusikilizwa; na mimi nimefanya kazi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sehemu ya sheria; wapo watu hawajui umuhimu wa haki ya kusikilizwa. Wananchi wakiwa na changamoto mbalimbali, nimesoma kwenye hii taarifa, huduma ya Mama Samia imewafikia zaidi ya Watanzania milioni 6.4; wamesikilizwa kesi zao. Wananchi wakisikilizwa kesi zao hata kama hawatapata ufumbuzi, lakini wanapata amani katika maisha yao. Ni muhimu sana haki ya kusikilizwa ikaendelea kujengewa msingi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninataka nijielekeze kutoa ushauri kidogo kwenye eneo la haki ya kupiga kura kwa mwaka huu 2025. Ninataka nitumie nafasi hii ndani ya Bunge lako Tukufu kutoa shule kidogo kwa Chama cha CHADEMA na wafuasi wao. Haki ya kupiga kura ni haki ya Mtanzania. Ukisoma kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 5. Ninaomba nisome kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania, inasema “Kila rai awa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi nchini Tanzania”

Mheshimiwa Naibu Spika, haki ya kupiga kura ni haki ya uraia wa Tanzania. Hakuna mtu mwenye haki ya kuvuruga haki ya mtu mwingine ya kwenda kupiga kura. Maana yake haki pekee walionayo vyama ambavyo havishiriki uchaguzi, wana haki ya kutokushiriki uchaguzi na wana ya kutokupiga kura wao, lakini hawana haki ya kuzuia Watanzania wengine kupiga kura katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ukisoma Ibara ya 30 ya Katiba hii imeeleza vizuri; kwamba uhuru wa watu wa kutumia haki yao ya kujieleza unapaswa ukome inapoanzia haki ya watu wengine. Mheshimiwa Rais alikuja na 4Rs katika nchi yetu; zimekuwa ni matunda makubwa; zimefanya reforms katika sheria na zimesaidia kuleta utulivu nchini, lakini inaonekana wenzetu wa CHADEMA wamevimbiwa na 4Rs za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupata uhuru wa kujieleza na uhuru wa maandamano wameanza kuvuka mipaka kwenda kuvuruga haki za wengine kupiga kura. Ninataka niiombe Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara hii ya Katiba na Sheria, tunaomba mlinde haki zetu sisi Watanzania ambao tupo tayari kwenda kupiga kura Oktoba mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jana niliangalia kule Ruvuma – Songea vyama 12 vimekaa vimesema vitashiriki uchaguzi; na sisi Wananchi wa Lupembe kwa kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta maendeleo kwenye maji, shule, ujenzi wa Mahakama na barabara tumejiandaa kwenda kupiga kura. Tunaiomba Serikali isifanye mchezo na jambo hili. Lazima ilinde haki ya sisi Watanzania kwenda kupiga kura Oktoba mwaka huu 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kwa mchana huu; ninataka pia nitoe wito kwa vyama vyote vya siasa. Kama alivyosema Dkt. Nchimbi kwamba uchaguzi wa mwaka huu siyo uchaguzi wa mwisho, upo uchaguzi mwingine baada ya 2025 watashiriki huo na ziko njia mbili tu za kufanya reforms kwenye sheria. Njia ya kwanza unafanya reform kupitia Bunge hili. Unaleta sheria ndani ya Bunge kisha unafanya reform na njia ya pili kwa mujibu wa sheria za nchi yetu unafanya reform kupitia Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama iko sheria ambayo haiku sawa Katiba imetoa nafasi ya mtu kwenda Mahakamani ku-challenge hiyo sheria ili iweze kurekebishwa. Ipo mifano mingi. Mwaka 2004 Bunge hili lilitunga sheria ambayo haikuwa nzuri, Sheria ya Takrima. Wanaharakati walienda Mahakamani sheria hii ikaondolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nitoe wito, hatuwezi kufanya reform ya sheria kwa kufanya maandamano mtaani Kariakoo. Huwezi kufanya reform ya sheria kwa kuhamasisha watu wasiende kupiga kura, reforms zinakuja Bungeni.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)