Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Shamsi Vuai Nahodha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ninaipongeza Wizara kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utendaji wa idara ya Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda kusema kwamba, Idara ya Mahakama imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha mifumo ya TEHAMA na kutumia Mahakama zinazotembea, ili kuimarisha ufanisi na utendaji wa kesi hasa kwa kutumia mikutano ya kimtandao (video conference). Hapana shaka matumizi haya ya teknolojia ya kisasa katika kuendesha kesi yamesaidia sana katika kupunguza gharama za uendeshaji na usafiri, hasa kwa Mahakimu na washtakiwa mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa maoni yangu, dhamira hii ya kutumia mifumo ya kisasa ya kiteknolojia katika kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi, inakwenda kinyume na dhamira ya kuongeza magari pamoja na matumizi makubwa ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika busara ya kawaida, unapokuwa na mifumo ya kisasa ya uendeshaji, matumizi ya magari yanataka kupungua kwa sababu kila magari yanapoongezeka na gharama zinazidi kuongezeka pamoja na ununuzi wa vipuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo nadhani ni vizuri nikaisemea, nafikiri Idara ya Mahakama ina haja ya kuangalia upya uamuzi wa kutaka kuanzisha karakana maalumu ya kutengeneza magari. Kwa maoni yangu, Mahakama ingepeleka magari yake katika karakana za Serikali ili Mahakama ikabakia na jambo lake la msingi la kuendesha kesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana nami kwamba, hivi sasa sisi kama Taifa tuna tatizo moja la msingi, na ni lazima tulisimamie kwa umakini sana. Makubaliano ya mikataba ya miradi yanachukua muda mrefu sana (negotiation). Nimeanza kusikia taarifa za kufanyiwa kazi miradi ya kusindika Gesi Asilia (LNG), pamoja na Mradi wa Chuma na Makaa ya Mawe Liganga tangu nikiwa Waziri mwaka 2013, mpaka leo bado tuko kwenye mijadala ya mikataba hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kuna haja ya kuifanyia kazi mikataba hii kwa umakini wa hali ya juu, lakini natambua pia iko tofauti kati ya umakini na kuchelewesha mambo. Athari yake ni nini kuchukua muda mrefu kuidhinisha mikataba hii? Kuna athari mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa duniani unafanyika utafiti wa matumizi ya Gesi ya Hydrogen kama chanzo cha nishati. Utafiti huu ukifanikiwa, gesi yetu itabakia chini ya ardhi kama makumbusho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, hivi sasa dunia inafanya utafiti juu ya kupata chanzo mbadala cha kutumia chuma. Badala ya kutumia chuma, watu wanafikiria kutumia madini ya platinum na titanium. Hilo likifanikiwa, chuma cha Tanzania kitabaki bila kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, suala la matumizi ya makaa ya mawe kama chanzo cha nishati, hivi sasa dunia inazungumzia juu ya haja ya kutumia nishati iliyo safi. Makubaliano hayo yakifikiwa, basi hapana shaka kwamba makaa ya mawe ya Tanzania yatakuwa hayana matumizi. Ndiyo maana ninasisitiza kuna haja ya kukamilisha miradi hii, na majadiliano haya yakamilike haraka iwezekanavyo, ili miradi hii ianze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mnasaba huo, naiomba sana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwapeleka vijana wake (wanasheria) nje ili wapatiwe mafunzo ya vitendo katika masuala ya majadiliano na maridhiano ya mikataba. Hapa sizungumzii shahada; unaweza ukawa na shahada moja, mbili, tatu, lakini weledi ukawa wa kiwango cha chini. Nazungumzia mafunzo ya vitendo ambayo utafundishwa maadili na mitazamo sahihi ya kufanya mambo, ndilo ninalolisisitiza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana nami kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inapaswa kuimarisha kitengo chake cha usuluhishi wa migogoro kati ya wawekezaji na Serikali. Tumekuwa tukipoteza hapa kesi nyingi sana, tunashtakiwa Serikali inapoteza. Hatuwezi kuendelea hivyo, kwa sababu Serikali inapoteza fedha nyingi sana. Ndiyo maana napendekeza kuna haja ya kuimarisha utendaji pamoja na mafunzo ya vijana wetu, ili wawe na weledi na umahiri wa kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)