Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na wenzangu waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria kwa hotuba nzuri ya bajeti ambayo kwa kweli imebeba maono, imebeba mafanikio, lakini imeeleza hali halisi na hatua tuliyopiga kama Taifa kwenye upande wa sekta hizi muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mchango kwenye maeneo machache, kama manne, na kama muda utaruhusu, nitakuwa na mchango kwenye maeneo manne.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza, natumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya kwenye nchi yetu kwenye sekta zote. Kwenye eneo linalohusiana na hotuba na hoja iliyoko mbele yetu leo, Mheshimiwa Swalle amesema vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kama kuna jambo limekuja kuwakomboa Watanzania hasa wa vijijini, ambao walilazimika kutafuta fedha nyingi kupata mawakili, lakini kutembea umbali mrefu kupata huduma za kisheria, ni Kampeni ya Mama Samia (Legal Aid Campaign). Jambo hili ni jambo kubwa na zuri, na kwa kweli Wizara ya Katiba na Sheria mnastahili pongezi. Kwa jambo hili, mmemtengenezea Mheshimiwa Rais legacy kubwa sana ya kuacha kwenye Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu na ushauri wangu kwenye eneo hili, kiu ya msaada wa kisheria ni ya muda mrefu sana, na hatimaye sasa tumeona imeanza kufikiwa. Tunaomba jambo hili liwekewe utaratibu wa kuwa jambo endelevu. Ni vizuri kama nchi tukawaza sasa namna ya kuwa na mfuko maalumu kwa ajili ya shughuli za msaada wa kisheria, ili hata kampeni hii ikiisha, si unajua kampeni hii ni mradi; jambo hili liwe endelevu kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ni jambo la Wanakorogwe Vijijini Tarafa ya Bungu, wanatembea zaidi ya kilometa 50 kwenda Korogwe Mjini kufuata huduma za Mahakama. Jambo hili nimelisema muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo jengo la Mahakama pale Bungu, lakini ni chakavu, halitumiki. Tuliamua hata kutafuta jengo lingine tuwape wenzetu wa Mahakama ili angalau kuwe na huduma za Kimahakama pale Bungu. Wananchi wanatembea kilometa 50 kufuata viapo, kwenda kusikiliza kesi zao, kupeleka mashauri yao. Jambo hili siyo zuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Wizara, najua Mheshimiwa Waziri ni msikivu, ni mtu mzuri sana, tuwasaidie wananchi wa Tarafa ya Bungu wasitembee hatua nyingi kufuata huduma za Kimahakama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu, natambua kwamba Waziri wetu wa Katiba na Sheria ni Mwenyekiti wa lile Jukwaa la Mawaziri wa AU. Najua iko mikataba mikubwa tumeingia, ikiwemo ile convention ya kuzuia ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, sijajua sisi kama nchi tumefikia hatua gani kwenye kufuata taratibu zote za msingi ili tuweze kutekeleza mkataba ule. Kubwa ambalo nataka kulisema leo, tunayo timu ya wataalamu, tunao wanaharakati, tunazo Asasi za Kiraia ambao walianzisha mchakato wa kutengeneza sheria maalumu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, walianzisha mchakato, ninawashukuru sana. Nawapongeza wenzetu wa TANLAP ndiyo waliongoza jahazi kwenye kazi hii. Kazi hii ilifanyika vizuri, ilishafika Serikalini. Mara ya mwisho mlisema mko kwenye hatua ya kuangalia, kukusanya maoni ili muweze kuyafanyia kazi. Natamani Mheshimiwa Waziri anapokuja kwenye kuhitimisha hoja, atuambie jambo hili limefikia wapi kama nchi kwenye kutengeneza sheria hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la nne na la mwisho ambalo nataka kuchangia kwa siku ya leo, Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo custodian wa sheria za nchi hii. Ndiyo mna jukumu la kusimamia sera kwenye maeneo haya. Yako mambo ambayo inawezekana yakawa hayawagusi moja kwa moja Wizara ya Katiba na sheria, lakini hamwezi kukwepa jukumu lenu la kutusaidia kuwapa elimu Watanzania juu ya sheria mbalimbali tunazotunga kwenye nchi yetu ili mambo yawe mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko sana, wako watu wanazunguka huko mtaani wanawahadaa Watanzania, wanawadanganya na wanawaambia kama hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi. Kimsingi ukiangalia mabadiliko wanayoyasema ni mabadiliko ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utashi wake mkubwa wa kisiasa aliamua kuyachukua, akaamua kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ikaleta Bungeni mapendekezo ya Miswada ya sheria tatu, tukafanya kazi ya kuchambua sheria hizo na tukatunga sheria ambayo lengo lake ni kufanya hayo maboresho ambayo hawa wenzetu ndiyo wanapita wanawaambia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali mkiendelea kukaa kimya, wasiokuwa na nia njema na Taifa letu wataendelea kuchafua nchi yetu, wataendelea kuwadanganya Watanzania, wataendelea kuichafua na kuiharibu nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii leo niiombe Serikali, pamoja na kwamba mambo ya uchaguzi ni mambo yanasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, lakini jambo la uchaguzi ni jambo la kisheria. Serikali haiwezi kukwepa jukumu lake la msingi la kutoa elimu kuhusu sheria hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana 2024 tumepitisha sheria hapa, tumefanya maboresho makubwa sana. Nataka nitumie nafasi hii ya leo kuyasema ili Watanzania huko nje wajue kwamba Serikali na Bunge lao tulishafanya kazi kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya kwanza kwenye historia ya nchi yetu tumetengeneza Sheria Maalum ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Huko nyuma tulikotoka mambo yote ya Tume ya Uchaguzi, zaidi ya kwenye Katiba, lakini pia tulikuwa tunayakuta kwenye Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, kidogo na kwenye Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya kwanza kwenye nchi yetu tumetunga sheria maalum inayoshughulika na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Kwenye sheria hii tumefanya maboresho makubwa sana ambayo ndiyo yalikuwa yakipigiwa kelele muda wote. Wenzetu hawa kwa miaka yote wamekuwa wakilalamika juu ya uteuzi wa Wajumbe wa Tume, kwa maana wale Makamishna.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Sheria ya Taifa ya Uchaguzi tuliyoitunga, ukienda Kifungu cha Tano, Sita, na cha Tisa, tumekuja na utaratibu mpya. Yako mambo makubwa matatu yamefanyika kwenye namna ya kuwapata Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, kwa mara ya kwanza Mheshimiwa Rais pamoja na kupewa mamlaka na Katiba kuteua Wajumbe wa Tume, lakini tumeweka utaratibu mzuri wa kisheria unaoleta uwazi na usawa. Tumetengeneza Kamati ya Usaili ambayo itakuwa na jukumu moja la kupendekeza majina; Jina la Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwenda kwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pamoja na Katiba kumpa mamlaka Rais, lakini hayachagui tu mwenyewe. Kuna Kamati ya Usaili inayopendekeza majina kwenda kwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo tumefanya, tumetengeneza utaratibu wa Wajumbe wote wa Tume, kuomba nafasi kwenye Kamati ya Usaili. Kamati ya Usaili inawafanyia usaili, inatoa mapendekezo na kuchagua wale ambao watakuwa wamekidhi vigezo. Zaidi sana, tumeenda mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii Kamati ya Usaili imewekwa watu ambao kwa nafasi zao, kwa mchakato wa upatikanaji wao, ni watu wasiotiliwa shaka kwenye nchi yetu. Kamati inaongozwa na Jaji Mkuu, inaongozwa na Jaji wa Zanzibar, inaongozwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora. Unataka watu gani wengine? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda duniani kote huwezi kuutoa kabisa mchakato wa kutengeneza Tume na Serikali iliyopo. Tunaye Rais; hii nchi siyo kwamba ipo tu haina Rais, Rais yupo, huwezi kumtoa; lakini nchi zote wanachotumia ni utaratibu kama huu, unakuwa na Kamati au unapeleka Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi humu tungeweka sheria kwamba Wajumbe wa Tume waletwe wapitishwe Bungeni, bado wangepiga kelele, wangesema Wabunge wengi ni Wabunge wa CCM. Tumeunda Kamati ambayo ina watu kutoka kwenye Vyombo vinavyoaminika, vyenye sifa za kustahili kuwa na haki ya kutenda kazi kwa usawa kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tumefanya, muda mrefu tumelalamikiwa kuhusu uteuzi wa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa mara ya kwanza Mheshimiwa Rais amekubali na tumepitisha sheria Bungeni. Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi hateuliwi tu na Rais mwenyewe, lakini Tume ya Uchaguzi ndiyo imepewa jukumu la kutafuta na kupendekeza kwa Rais mtu wa kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kuna reform gani nyingine inahitajika zaidi ya reform hizi ambazo zimefanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu, tumekuwa pia na muda mrefu tukilalamikia uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi. Sheria tuliyokuwanayo, Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ilikuwa inatamka na kutoa sharti moja kwa moja kwamba, kila Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Mkurugenzi wa Manispaa, ndiyo atakuwa Msimamizi wa Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sheria hii tumempa nafasi Rais aweze kutafuta mtumishi yeyote wa Umma, Mwandamizi, ambaye mara nyingi huyu atakuwa siyo lazima awe mteule wa Rais, hali ambayo inamwondolea wasiwasi na kumfanya atende kazi hii kwa usawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi sana, kwa mara ya kwanza tumeweka sheria kwamba Msimamizi huyu wa Uchaguzi...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa unazungumza mambo muhimu, nakuongeza dakika moja.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka kwenye sheria kwamba, msimamizi huyo wa uchaguzi, kuna na sifa ya ziada kwamba, ni lazima awe hajashika nafasi yoyote kwenye chama cha siasa kwa muda usiopungua miaka mitano. Hili ni jambo ambalo ni kubwa na jambo ambalo halikuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mambo yaliyofanyika ni makubwa. Ukiangalia utaratibu uliowekwa ni utaratibu mzuri. Jambo hili limekaa kwenye namna ya kuwapata watumishi wa kawaida mpaka wasimamizi wa vituo; mpaka wasimamizi wa vituo vya kuandikisha na vituo vya kupigia kura wanaomba kazi, wanafanyiwa usaili, wanaajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara na niiombe Serikali; kwenye mambo ya msingi kama haya tusiwachekee watu wenye nia mbaya. Kama tumefanya yote haya na bado watu hawaoni, watu hawa wana jambo lao lingine. Tutoe elimu kwa Watanzania wajue ukweli, lakini tusimamie sheria nchi yetu iendelee kuongozwa kwa mujibu wa utaratibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)