Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze moja kwa moja kumshukuru Mheshimiwa Rais. Sote tunafahamu kuna mvua za masika zinazoendelea sasa na upande wa jimbo langu kule Mlimba, barabara zimekuwa zikiharibika sana, lakini kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kweli namshukuru Mheshimiwa Rais, amechukua hatua. Alimwelekeza Waziri wa Ujenzi kaka yangu Mheshimiwa Ulega, naye ninamshukuru sana. Alipanda helikopta kutoka Dodoma na amekwenda kuchukua hatua kule na Serikali ipo kazini. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye hotuba hii ya bajeti ya leo. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayofanya, nami ninasema tu kwa dhati, ukiona Mheshimiwa Waziri unateuliwateuliwa kwenye Wizara moja mara mbili, maana yake wewe ni mbobezi katika eneo hilo. Hongera sana, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa jambo lingine mahsusi. Jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya ni kukamilisha ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama yetu ya Tanzania. Jambo hili ni la kumpongeza, kwani ameweka historia katika Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, namshukuru His Lordship Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Mahakama yetu Tanzania. Namshukuru kwa sababu moja, amefanya mageuzi makubwa sana kwenye Mhimili huu wa Mahakama. Siyo tu kuhamisha Makao Makuu, kusimamia ujenzi wa Makao Makuu Dodoma, lakini amefanya mageuzi mengi kama vile matumizi ya TEHAMA ambayo inasaidia katika kuharakisha kesi zikamilike kwa wakati na Watanzania wanatendewa haki. Kwa hili, ninampongeza sana Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, hakika atakumbukwa kizazi hata kizazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapompongeza Mheshimiwa Jaji Mkuu, ninanukuu maneno ya Rais wa Awamu ya 26 wa Marekani. Yeye alisema maneno haya, anaitwa Theodore Roosevelt. Anasema maneno haya; “People don’t care how much you know until they know how much you care.” Alikuwa na maana hii, unapopewa dhamana za kuhudumia watu, lazima utimize wajibu wako, kiasi cha kwamba unajali watu. Yaani unaacha matokeo, unaacha alama ili kusudi watu waone kweli wewe ulikuwa unajua katika kutimiza majukumu yako hayo uliyopewa. Sasa kwa hili, Jaji Mkuu wetu amefanya na Theodore Roosevelt anasema maneno haya, nami ninampongeza sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye eneo hili la Kampeni ya Msaada wa Kisheria wa Mama Samia. Yaani kama kuna jambo ambalo sisi Watanzania tuna kila sababu ya kujivunia ni kampeni hii. Wenzangu wamesema, Mheshimiwa Mnzava ameeleza hapa nami ninamuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzishwa kwa Mfuko Maalum wa Msaada wa Kisheria, kimsingi tunaona jambo hili lina tija kwa Watanzania. Sasa, naongeza jambo lingine, kwani kuna dhambi gani tukifanya iwe taasisi kwa mujibu wa sheria? Kwa sababu nafahamu, Mheshimiwa Rais analifanya jambo kwa utashi wake yeye binafsi. Sasa, akienda akapata awamu hii nyingine ya pili akahitimisha muda wake, sasa je, kampeni hii inakwenda kusimama?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lazima kama Serikali mchukue hatua. Tuanzishe taasisi kwa mujibu wa sheria ambayo kizazi hata kizazi kitamkumbuka Mheshimiwa Rais kwa ubunifu mkubwa wa kuwasaidia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nijielekeze eneo lingine la huo msaada wa kisheria kuimarisha Huduma za Kisheria za Msingi (Primary Legal Aid). Nataka kusema nini hapa? Tunafahamu kwamba pamoja na jitihada za Serikali katika kutoa msaada wa kisheria, kuna baadhi ya maeneo kama vile Magereza, kuna watuhumiwa na wafungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naomba ninukuu kundi moja la muziki huko nyuma linaitwa “Majitu”, walimshirikisha Inspector Haruni, wanasema hivi, “siyo wote wanaokwenda jela wana hatia, wengine wanakwenda kwa kesi za kusingiziwa.”
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi huduma za misaada ya kisheria zikienda kwenye maeneo kama Magereza, najua zipo, lakini zikaimarishwa, zikawa funded, zikawekewa mpango maalum wa fedha ili hawa paralegal pamoja na Serikali watengeneze mfumo ambao utafanikisha wafungwa kupata msaada wa kisheria ili waweze kujitetea na wasihukumiwe bila kuwa na hatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala la RITA. Tunafahamu kazi kubwa wanayofanya RITA (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini), wanafanya kazi nzuri. Leo hii tunaona sasa hivi usajili wa vyeti vya kuzaliwa unafanyika kupitia mtandao. Jambo hili ni jema sana, lakini kwa sisi hasa Wabunge wa Vijijini kama pale Mlimba, mwananchi anayetoka Kata ya Masagati anatembea umbali wa kilometa takribani 223, anakuja Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Kilombero kufuata cheti cha kuzaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni ushauri wangu kwamba Serikali sasa ione haja ya kuwekeza fedha. Taasisi yetu ya RITA ipewe fedha za kutosha ili kusudi vyeti vikiwa tayari, basi viende kwenye Kata zetu na mwananchi apate cheti kwa wakati kwa kutumia gharama nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine niende kwenye Mahakama yetu ya Mwanzo ya Mlimba. Hii naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, na nimpongeze Mheshimiwa Waziri na pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais. Jengo lililojengwa pale Mlimba lina hadhi ya kuwa Mahakama ya Wilaya, na limejengwa, na wakati huo lilianza na mzee wangu Mheshimiwa Prof. Kabudi, ndiyo alianzisha ujenzi wa ile Mahakama. Jengo hili ni la kisasa, lina hadhi ya Mahakama ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri ikimpendeza pamoja na kwamba Mlimba ni Halmashauri ya Wilaya, tunakwenda kutafuta hadhi ya Wilaya kamili, basi Mahakama itangulie. Ile Mahakama ya Mwanzo ya Mlimba pale ipate hadhi ya kuwa Wilaya, itoe huduma kwa wananchi wale wa Mlimba.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nitoe wito na niwakumbushe ndugu zetu wote ambao wamepata heshima kubwa katika taasisi au vyombo vya dola katika utoaji wa haki. Niwape rai moja, na hapa naomba ninukuu maneno ya Biblia, wakasome Zaburi ya 90:10 inasema maneno haya, “uhai wetu hapa duniani ni miaka 70, tukiwa ni wenye nguvu 80, kiburi chake ni taabu na mateso duniani.” Maana yake nini? Duniani tunapita. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukipewa jukumu la kutoa haki hebu toa haki vizuri kwa kuzingatia misingi ya sheria, kwa sababu duniani tunapita. Nimesema, na Biblia inasema ukizidi miaka 80 na kuendelea, kiburi chake ni taabu na mateso. Maana yake nini? Hata suti ya shilingi 1,000,000 ukiwa na miaka 90 huwezi kuvaa. Hata nyama huwezi kutafuna, ndiyo taabu na mateso duniani. Kwa hiyo, duniani maisha yetu ni temporary. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorinto anasema, “nikiitazama dunia ni ubatili mtupu.” Kwa hiyo, tunavyokwenda kutoa haki iwe katika level ya familia, iwe katika level ya taasisi za Serikali au Mahakama, tusimamie misingi ya haki tukijua kwamba hapa duniani tumekasimiwa haya majukumu kama neema; tumepewa kwa neema. Sasa hebu tutumie neema hii vizuri kuwatendea haki ambao kimsingi hawana hatia na wanataka kutendewa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yaliyopo duniani tuwe na mali, tuwe na fedha tutaziacha duniani na tutatangulia mbele za haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja, na itoshe tu kusema tumsaidie Mheshimiwa Waziri bajeti yake ipite kwa sababu nia njema ya Mheshimiwa Rais ni kuimarisha misingi ya haki nchini, ahsante sana. (Makofi)