Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Niseme hivi kwamba Mama yetu ametupatia elimu, ametupatia afya, ametupatia maji, ametupa bei ndogo za mahitaji yetu kwa ku-maintain inflation nchini, ametupatia umeme, ametupatia barabara, ametupatia freedom of speech, watu kuzungumza wanavyoweza kuzungumza, na anavumilia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtu amekupa hayo yote, sasa anakuletea haki kwamba na upate na wewe haki yako pale ambapo kunakuwa na msuguano kati ya binadamu na binadamu, taasisi na taasisi, na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hiyo akapenda pia kwamba atupe safu nzuri kwenye Mhimili wa Mahakama na kwenye Wizara hii ambayo inasimamia masuala mazima ya Sheria na Katiba. Amepanga safu nzuri na ninaamini wote tunampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu, Jaji Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mheshimiwa mpendwa wetu Profesa Elisante Ole Gabriel na watendaji wengine pamoja Majaji na Mahakimu, tumepewa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba huyu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wetu ni mtu kweli anajali maisha ya binadamu holistically, kwa ujumla wake, tunataka kuishi namna gani? Ndiyo maana naamini kwamba anatekeleza kwa vitendo lile lengo la kwamba maendeleo ni maendeleo ya watu na sisi tunaona ya kwamba tunapata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tukiangalia, mimi nipo kwenye Kamati ya Bajeti. Kwa hiyo, tumepitisha kwa urahisi sana mapendekezo ya bajeti ya Mahakama. Tumepitisha kwa urahisi kwa sababu inaleta tija na unaona vitendo vikifanyika. Unaona wakitekeleza malengo yao kwa vitendo na kwa ufanisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme, ukiangalia dira yao kusema kweli watapunguza gharama za Mtanzania na mwananchi kufikia kupata haki yake. Pia, watapunguza gharama kwa wananchi kuanzia mdogo mpaka wa juu na taasisi pia kuweza kupata haki kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki kimefanyika zaidi kwa kuingiza mageuzi makubwa kwenye delivery ya justice, utaona kwamba na niseme ndiyo sababu nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na hususan Mtendaji Mkuu. Nampongeza sana kwa sababu mageuzi siyo kitu kinachokubalika kwa binadamu, hata kiumbe mwingine yoyote ambaye ana uhai, tuna resist mageuzi kwa sababu tunataka kukaa kwenye comfort zone. Sasa watu wanatutoa kwenye comfort zone, wewe bado unabaki upo happy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba kwenye Mahakama kumetokea mageuzi makubwa ambayo kwa kwa namna yoyote mimi nilifikiri kwa sababu Majaji wengi ni watu wazee kama mimi, (aah, mimi siyo mzee), wangekuwa wana-resist haya mageuzi, kwa sababu ni TEHAMA; wanaingiziwa TEHAMA, wanaingizwa kwa speed ambayo huwezi ku-cope kwa sababu lazima upate mafunzo, utumie mbinu za kisasa za kuweza kujiingiza kwenye mageuzi yale na kutekeleza wajibu ambao unafanya. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwamba Mahakama wameweza, na niseme kwamba kwa namna ile wameweza kupunguza sasa gharama za kutoa haki, jukumu lao hilo na ni kitu ambacho kusema kweli kinafurahisha sana. Niseme kwamba pamoja na TEHAMA, utaona kwamba Mtendaji Mkuu wa Mahakama ambaye ndiye anafuatilia utekelezaji wa mambo mengine nje tu, siyo pale tu kwenye kutoa haki ameweza kubadilisha sana miundombinu kama tulivyoonesha kwenye ripoti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu ya Mahakama kuanzia Mahakama za Juu, kule juu ameshaweza sana mpaka kwenye Wilaya kwa kiasi, lakini sasa bado kidogo kwa sababu maendeleo ni hatua, bado kidogo kwenye Mahakama za Mwanzo hajaweza kukamilisha dira yake. Hata hivyo, kwenye bajeti ya mwaka huu ambayo tunapendekeza tupitishe, ameweka fedha za kuendeleza mchakato huu wa kuboresha majengo ya kutolea haki kwenye ngazi zote hizo za Wilaya pamoja na za Mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, alikarabati Mahakama moja ya Mwanzo pale kwenye Jimbo langu kwenye Kata ya Kilema Kati ambayo haijakamilika, lakini natumaini atakamilisha. Pia, tuna Mahakama nyingine kwenye Kata ya Mamba Kusini ambayo imekwisha kabisa pamoja na hizo nyingine kwenye Kata nyingine za Mwika, Kata ya Marangu pamoja na Kata za Mkuyuni na kule Kirua Vunjo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba ile pale Kisambu ina matatizo, inatakiwa iangaliwe kwa jicho la kipekee kwa sababu hata Hakimu hamna sasa hivi. Kwa hiyo, naomba kwamba katika changamoto tuliyoona mojawapo kwenye suala zima la utekelezaji wa majukumu ya Mahakama ni upungufu wa watumishi. Wanahitajika watumishi na waliomba kuajiri zaidi ya 1,000, lakini wamepata 600 tu kwa mwaka huu 2024/2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba wakati huu unaofuata mamlaka itaweza kukubali waongeze ajira kwenye eneo hilo ambalo ni changamoto kubwa kwa Mahakama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine ambayo yamefanyika na ambayo yanafurahisha sana ni uwezo wa Mahakama sasa hivi kutoa proceedings za mashauri pamoja na tafsiri zake kwa Kiswahili papo kwa hapo, baada tu ya kukamilika mawasilisho husika. Sasa hiyo wametumia akili mnemba na TEHAMA zinazohusika ili kuweza kufikia lengo hilo. Napongeza sana kusema kweli kwamba mashauri ya muda mrefu yamepungua, na ni kama yamekwisha. Wanasema, “justice delayed is justice denied.” Sasa naona hilo kweli wamezingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kulikuwa na mashauri ya muda mrefu yaliyozidi mwaka mmoja takribani 60,000 na sasa wameyapunguza mpaka 1,700. Wamepunguza kwa 97%, kwa hiyo, ni kitu ambacho nakipongeza sana na ni jambo ambalo limesaidiwa sana na matumizi njia hii mpya.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kimei, kengele ya pili hiyo.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, kengele imelia?

NAIBU SPIKA: Ukizungumza vitu vizito muda unakwenda upesi sana.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi naunga mkono hoja. (Makofi)