Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata fursa ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa mtetezi wa haki za binadamu namba moja hapa nchini na kwa kuhakikisha kwamba Serikali inaimarisha mazingira ya haki jinai hapa Tanzania, na pia kuharakisha upatikanaji wa haki kwa kuja na hii Samia Legal Aid Campaign ambayo imeleta mageuzi makubwa katika kuharakisha upatikanaji wa haki ngazi ya jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kufikia maono haya ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika eneo hili mahususi la haki jinai, mimi napenda kujielekeza katika maeneo mawili yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza, ni katika eneo la matukio ya ukatili kwa maana ya ubakaji na ulawiti kwa watoto. Kwa mujibu wa taarifa ya Jukwaa la Haki Jinai Mkoani Kagera, kwa masikitiko makubwa ni kwamba Mkoa wa Kagera kwa mwaka 2024 umeongoza hapa nchini kwa matukio ya ukatili kwa maana ya ubakaji, ukatili na mauaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika, katika mwaka huu wa 2025 kati ya mwezi Januari hadi Machi, 2025, Mkoa wa Kagera tumekuwa na matukio ambayo yameshawasilishwa Mahakamani 67 ya ubakaji na ulawiti wa watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo kwa Mkoa wa Kagera pekee yake, lakini kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio ya ubakaji na ulawiti kwa watoto nchini kwetu hapa Tanzania. Kutokana na mianya ambayo ipo, kumekuwa kuna ucheleweshaji na wakati mwingine kutoweka kwa upatikanaji wa haki kwa wahanga wa watoto wa matukio ya ukatili, ubakaji na ulawiti. Kwa hiyo, ningependa kuishauri Serikali kwenye mambo yafutayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, watuhumiwa wa vitendo vya ukatili kwa watoto kwa maana ya ubakaji na ulawiti wasipate dhamana. Haya yaongezwe kwenye makosa ambayo hayapewi dhamana. Nasema hivi kwa sababu, pale ambapo mtuhumiwa wa ubakaji au ulawiti wa mtoto anaporudi katika jamii ile kwa sababu amepewa dhamana, moja ya vitu wanavyokwenda kufanya ni kwenda kuharibu ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa pili, yule mtoto kama bado yupo kwenye jamii au ile familia, tunakwenda kumwathiri zaidi kisaikolojia kwa kuendelea kuonana na huyu mtu ambaye ni mtuhumiwa. Tatu, inafifisha jitihada kubwa za Serikali za wananchi kuweza kujitokeza na kuwasilisha mashitaka haya. Kwa hiyo, nisisitize kwa Serikali, ione namna ya kuongeza makosa ya ubakaji na ulawiti kwa watoto kwenye orodha ya makosa ambayo hayapati dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni kwamba, pale ambapo kunakuwa na kesi za watoto kwenye masuala ya ubakaji na ulawiti zimefikishwa Mahakamani, kumekuwa na desturi ya kesi hizi kuchukua muda mrefu sana. Unakuta mawakili saa nyingine wanaowatetea wale watuhumiwa wanatumia mianya ya kuahirisha kesi mara kwa mara na matokeo yake zile kesi zinakuja ama kushindwa ama kujikuta hata wale ambao ni wahanga wamechoka katika ufuatiliaji wa kesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali iweke kwamba inapotokea hizi kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto zisikilizwe ndani ya muda mfupi kwenye Mahakama na haki itendeke kwa maana ya maamuzi ya Mahakama yatolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kesi itasikilizwa, isikilizwe mara moja au mara mbili, lakini haikubaliki kwamba kesi ya mtoto aliyebakwa ama amelawitiwa ichukue miezi mitatu, miezi sita au miezi saba na wakati mwingine mpaka mwaka jambo ambalo kusema kweli linafifisha jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha haki jinai na kuimarisha ulinzi wa watoto wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iweke ukomo wa muda ambao unapaswa utumike katika Mahakama zote hapa nchini kwenye kesi zinazohusu ubakaji na ulawiti kwa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la pili, ningependa kuchangia katika eneo hili la msaada wa kisheria. Kwanza kabisa napenda kuipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo inashirikiana na mashirika ambayo siyo ya Kiserikali (NGOs) ambao ndio wanafanya kazi kubwa sana katika kutoa msaada wa kisheria ngazi ya kijamii kwa kushirikiana na wasaidizi wa kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba haya matokeo makubwa yaliyopatikana na mafanikio makubwa yaliyopatikana na Samia Legal Aid Campaign yawe endelevu, basi napenda kuishauri Serikali kwamba iende itekeleze takwa la kisheria katika maeneo mawili. Sheria inasema kwamba katika kila Kata kuwe kuna wasaidizi wa kisheria, jambo ambalo bado halijatekelezeka. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iende ikatekeleze takwa hili la kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni kwamba ili Samia Legal Aid Campaign iendelee, lazima kuwe kuna rasilimali fedha na sheria tayari ilishaliona hili, ndiyo maana ikaelekeza kwamba Serikali ianzishe Legal Aid Fund.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu mkubwa, naiomba sana Serikali iende kuweka mpango madhubuti wa kuja na Legal Aid Fund ili matokeo haya yaliyopatikana na Samia Legal Aid Campaign yawe ni endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha, naomba nirejee, tena naiomba sana Serikali, watuhumiwa wa makosa ya ubakaji na ulawiti kwa watoto wasipate dhamana. Hali kadhalika, naiomba sana Serikali, muda wa kusikiliza hizi kesi za watoto ambao wamebakwa na kulawitiwa ndani ya Mahakama zitengewe muda mfupi (isikilizwe ama mara moja au mara mbili) na uamuzi wa Mahakama utolewe ili haki ipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni kwamba Serikali ihakikishe tuna wasaidizi wa kisheria kama ambavyo sheria inaelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhitimisha, Serikali ihakikishe inaanzisha Legal Aid Fund ili haya matokeo chanya makubwa tuliyoyapata kupitia Samia Legal Aid Campaign yaweze kuwa endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa fursa hii na ninaunga mkono hoja. (Makofi)