Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwanga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa Bahati ya kupata nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwa mchana huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa jinsi ambavyo ameniongoza kuwatumikia wapigakura wangu wa Jimbo la Mwanga kwa kipindi changu hiki cha kwanza cha uongozi ambacho sasa kinaelekea mwishoni ili niweze kuanza cha pili. Namshukuru Mungu kwa ajili hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namwomba Mwenyezi Mungu kwamba neema na rehema zake ziniongoze katika kipindi cha pili ambacho ninaamini atanijalia, zikuongoze na wewe pamoja na Wabunge wote wa Bunge hili la Kumi na Mbili katika awamu ya 2025 kwenda 2030.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru sana wananchi wangu wa Jimbo la Mwanga kwa jinsi ambavyo waliniamini na kunipa dhamana. Hiyo peke yake isingetosha, waliendelea kunipa ushirikiano kwa dua na sala ambazo zimeniwezesha kufanya kazi vizuri kwa kipindi chote cha miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nakishukuru chama changu, Chama cha Mapinduzi na Serikali yangu kwa kuniunga mkono na kuniletea miradi mingi sana ambayo imeniwezesha kuwa na mafanikio makubwa ndani ya kipindi hiki. Hata hivi tunavyozungumza, tunaenda mwishoni lakini bado miradi inakuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi uliopita nilipata mradi wa umwagiliaji wa shilingi bilioni 16.874. Huu ni mradi mkubwa na unafanya kazi hii iweze kunoga. Kila nikiangalia bajeti inavyokwenda na mipango ya Serikali, naona kabisa kwamba huko mbele kunafurahisha zaidi. Kwa hiyo, ni vema sote turudi tuendelee kusimamia hizi kazi ambazo zinakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Waziri, rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro pamoja na timu yake yote, pamoja na taasisi zinazomzunguka chini ya Mheshimiwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Mkurugenzi wa Mashtaka pamoja na wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kazi nzuri ambayo wamefanya, wamesimamia vizuri uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta hii ya sheria na utoaji haki. Ujenzi wa miundombinu ya hali ya juu, mikakati katika masuala ya TEHAMA ambayo kwa kweli yameharakisha sana kumalizika kwa kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi ambao tumefanya kazi na Mahakama hii toka miaka mingi kidogo, tunaona tofauti kubwa sana kwamba kwa mara ya kwanza nilipoangalia taarifa za mwaka 2024, idadi ya mahabusu ilikuwa ndogo kuliko wafungwa. Hii inaonesha ufanisi kwenye upande wa Idara ya Mahakama pamoja na wadau wengine wa eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, suala zima la hakijinai. Kwenye hili, kwa kweli Mheshimiwa Rais amefanya kazi ya maana sana, kwa sababu haki jinai ndilo eneo ambalo lina uwezo wa kuichafua sana nchi na kuichafua Serikali kuonekana kwamba watu wananyimwa haki, kwa sababu haki jinai inawagusa watu wengi sana na watoto wadogo. lakini Tume ya Hakijinai imefanya kazi nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeiona taarifa yake na nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba sasa inaandaliwa sera ya haki jinai. Nina hakika ikiandaliwa inline na ile taarifa, basi hali yetu inaenda kuwa nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, suala la kutafsiri sheria kwa Kiswahili pia litasaidia watu wengi kuzielewa na kwenda mbele. Ukiangalia haya maboresho kwa ujumla, yanasaidia sana lile eneo la haki moja ya msingi sana ya kuifikia haki (access to justice).
Mheshimiwa Naibu Spika, Ukitaka kujua vizuri dhana hii jinsi ambavyo ni kubwa ukisoma uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwenye ile kesi ya Julius Francis Ndyanabo maelezo ya Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa yaliyotoka ni mazuri sana chini ya aliyekuwa Jaji Mkuu kuonesha jinsi ambavyo haki hii ni ya msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, bila ya kuwa na miundombinu wezeshi yote ya kawaida, majengo na masuala haya ya TEHAMA na elimu, basi haki hiyo ni vigumu sana kuifikia. Pia ukiangalia maboresho haya yamegusa zaidi kwenye upande wa vocabulary kwa upande wa Kiswahili, kidogo inanisumbua, public law. The Public Law ni ile sheria ambayo inahusiana na mahusiano ya Serikali na mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa vipi Mamlaka ya Serikali na matendo yake yasimnyime mtu haki? Serikali imewekeza sana kwenye upande huu katika maana kwamba inajaribu kujidhibiti kwamba matendo yake yasiwanyime watu haki. Hili ni jambo la maana sana katika kusimamia utawala wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwenye private law, mambo ya mikataba yamefanyika, lakini naona kwenye upande wa public law ambao hasa ndiyo unagusa haki za msingi za watu, kazi kubwa sana imefanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamezungumziwa sana suala la ujenzi na kufunguliwa kwa jengo la kisasa sana la Mahakama, kwa kweli jambo hili ni kubwa sana na halipaswi kupitwa bila kutajwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hili lenye mita za mraba 63,244 ni la kwanza Afrika kwa ukubwa na jengo la sita kwa dunia, lenye thamani ya shilingi bilioni 127.7, kwa kweli ni jambo ambalo ni la kujivunia sana kwa Tanzania. Linafungua milango kwamba sasa tunayo Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa inayotarajiwa Makama ya Juu (Supreme Court) zikiwa mahali pamoja. Hiyo itarahisisha sana suala zima la uharakishwaji wa haki katika ngazi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika uboreshaji huu. Kazi inabaki sasa kwa watendaji kuhakikisha kwamba ukubwa huu wa namba moja Afrika usibakie kuwa wa jengo na miundombinu, ila uwe pia wa huduma ambazo zitatolewa pale, kwamba tuwe namba moja Afrika na namba sita Kidunia, uwe na thamani kubwa kama ile thamani ambayo imewekezwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni changamoto kubwa lakini ni changamoto nzuri kwa sababu tukifikia hapo hiyo itakuwa inachochea pia maeneo mengine ya uchumi na maisha ya wananchi wetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ina-deal na bidhaa isiyoonekana. Hakuna kuuza na kununua pale, ila ile bidhaa ya Mahakama au bidhaa ya sheria na haki kufanyika vizuri, hata hao wanaouza na kununua hawataweza kufanya vizuri. Kwa hiyo, hela yote ambayo imeingia pale kwa kweli inastahili, it is worth it lakini sasa tuitendee kazi ili isiwe hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo yanapaswa kuendana na uwekezaji huu mkubwa. Kwa mfano, hatutaona faida kubwa sana ya Mahakama ile katika ngazi ya juu kuwa ya thamani ile kama Mahakama za Mwanzo na Wilaya hazitafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu Mwanga nina Mahakama nzuri sana ya Wilaya, wanafanya kazi nzuri, lakini Mahakama za Mwanzo bado ni zile za mkoloni na hizo ndizo zinazohangaika na haki za watu za kila siku. Kwa hiyo, natoa wito tu kwamba uwekezaji pale uendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa inayoitwa Jipendea kwenye Jimbo langu la Mwanga iko Mahakama ya Mwanzo ya kisasa ambayo inatarajiwa kujengwa Kata ya Kwakoa. Naomba sana kwamba tujitahidi, sasa tunakoelekea bajeti ya mwaka huu ile Mahakama sasa ijengwe ili huduma iende moja kwa moja kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala lingine ambalo ninalisema leo Bungeni, nafikiri ni kwa mara ya tatu toka nimeingia Bungeni. Mabaraza ya Ardhi kuwa chini ya Wizara ya Ardhi hili ni tatizo, kwa sababu kesi nyingi ni za ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza la Ardhi liko chini ya Wizara ya Ardhi wakati migogoro mingi wananchi wanailalamikia hiyo hiyo Wizara ya Ardhi na Watendaji wake, hati yangu imefanywa hivi, double allocation na kadhalika. Sasa pale ambapo waamuzi ni waajiriwa wa Wizara ya Ardhi kunakuwa na tatizo. Kwa hiyo, natoa wito kwamba, hilo tulitazame ama turudishe chini ya Mhimili wa Mahakama kwa sababu hata ikiwa chini ya Wizara ya Ardhi, bado rufaa na nafuu nyingine zinarudi tena chini ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Jaji Mkuu analazimika ku-deal na watu ambao hawako chini yake. Hili nadhani ni tatizo ambalo ni vizuri likashughulikiwa. Kwa hiyo, zirudi chini ya Mahakama au basi sheria irekebishwe mtu awe na hiari ya kwenda Baraza la Ardhi au kwenda Mahakama ya kawaida kama ilivyo kuanzia ngazi ya High Court kwenda juu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo tunapaswa kulifanya ili tuweze kufurahia uwekezaji huu mkubwa ni kwa kadri itakavyowezekana turekebishe sheria zetu za mwenendo (procedural laws), na hili wananchi wengi hawatuelewi sisi wanasheria. Hata frustration zinazotokea kwamba mbona kesi zinachelewa wakati mwingine? Ni kwa sababu ya sheria zetu za mwenendo, kidogo kutokuwa rafiki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siyo muumini wa kusema kwamba sijui makosa fulani tunyime dhamana mpaka sijui kufanya nini, hapana. Mimi ni muumini wa kusema kwamba haki itendeke kwa haraka, hizo kesi zisikilizwe haraka. Hakuna sababu ya kesi ya kubaka ya kawaida, hizi za watu wazima, procedure yake iwe sawasawa na hii rape ya watoto wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa sababu ile ya watoto wadogo kitu cha kwanza ni tendo limefanyika; kuna taarifa ya Daktari jambo la pili aliyefanya ni nani? Cha tatu, umri wa mtoto, cheti cha kuzaliwa, habari imeisha. Kwa hiyo, hakuna vita kubwa kama ile ya kusema je, alikubali? Alifikaje hapo? Aliingiaje kwa watu usiku? Na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema hayo bila kusahau juhudi ambazo zimefanyika. Sote tumeona hii kesi ya juzi juzi hapa almaarufu ya afande jinsi ambavyo iliamuliwa kwa haraka. Lile ni jambo ambalo kwa kweli Mahakama na wadau wote wanastahili credit ya hali ya juu sana. Wanahitaji sifa na kupongezwa, kazi inafanyika vizuri, lakini bado tuweke mifumo ya kisheria. Tusitegemee lile ambalo lina kelele nyingi ili tuweze kumaliza haya mashauri kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mama Samia Legal Aid Campaign limezungumzwa sana. Kwa nini limezungumzwa sana? Kila mtu anajua haki yake. Shamba hili ni la kwangu kila mtu anajua. Mke huyu ni wa kwangu kila mtu anajua, hata wanyama pia wanajua. Ukimpa mbwa wako chakula, kikishakua nyama ile ni ya kwake, ukijaribu kumnyang’anya, atapambana na wewe. Ninachotaka kusema ni kwamba, kila mtu anajua haki yake.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili hiyo.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie.
NAIBU SPIKA: Haya, malizia.
MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo ni jinsi ya kupata ile haki, ndicho kitu ambacho huwa kinasumbua.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kampeni hii ya Legal Aid kama ya Mama Samia Legal Aid Clinic, hii inawafundisha watu jinsi ya kupata haki zao, kwa sababu watu wasipojua utaratibu wa kupata haki zao, maana yake ni kwamba watakimbilia kwenye vurugu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa champion wa kampeni hii kama ambavyo amekuwa champion kwenye maeneo mengine makubwa. Tumpongeze sana kwenye hili, na pia nisisitize lile nililosema kwamba kuwe na mfuko ambao utawezesha kazi hiyo iweze kufanyika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)