Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia na kuwa mtu wa pili baada ya mwenzangu Mheshimiwa Tadayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambazo amekuwa akizifanya ndani ya nchi yetu, pia amekuwa na utayari katika kutoa fedha ama kuruhusu Wizara mbalimbali kuongezewa fedha ikiwemo hii Wizara ya Katiba na Sheria. Nampongeza sana kwa mabadiliko makubwa ambayo ameyaleta katika sekta ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nawapongeza Wizara kwa kusimamia sekta hii ya Wizara ya Katiba na Sheria vizuri. Vilevile, nampongeza Jaji Mkuu, Mtendaji Mkuu wa Mahakama na taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema, kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuja na hii Mama Samia Legal Aids, kwani imekuwa ni msaada mkubwa kwa jamii yetu na hasa katika mikoa mbalimbali ambayo nimeweza kutembea na kufika, imewasaidia wananchi ambao kwa namna moja ama nyingine hawana fedha za kuajiri mawakili au wanasheria kupeleka kesi zao Mahakamani au kusimamiwa katika vyombo vya haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mama Samia Legal Aids imekuwa na msaada mkubwa na bajeti ambayo wanayo ingependeza bajeti yao ya mwakani iongezeke zaidi ili kazi hii iweze kufanyika kwa ukubwa zaidi, iweze kushuka katika Wilaya zetu na iwepo kwa muda mrefu, kwani imekuwa na manufaa makubwa, na watu wengi wanahitaji kupata huduma. Kwa sababu ya ufinyu wa muda, nadhani kwa kuwa pia inazunguka mikoa yote nchi nzima, tukiiongezea bajeti kwa bajeti ya mwakani, itatusaidia kuongeza wigo mpana wa watu kupata haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa na utayari wa kuleta mabadiliko mbalimbali katika Mahakama zetu. Tumeona Mahakama zilivyobadilika, hasa Mahakama Kuu, katika ngazi ambayo leo kesi mbalimbali zinaendeshwa kwa teknolojia ya hali ya juu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji mkubwa umefanywa, fedha nyingi zimewekwa na tumeona majengo makubwa hata jengo kuu tuliona juzi Mheshimiwa Rais alizindua, kwa Afrika inawezekana ikawa namba moja na duniani ni namba sita, hongera sana. Huu ni utayari wa kutoa fedha katika uwekezaji, ninaamini fedha hizi katika uwekezaji huu utaenda katika level za mikoa, ninajua mikoani pia kuna Mahakama mbalimbali zimebadilishwa ikiwemo Tabora, kuna Mahakama kubwa inajengwa sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara, katika Wilaya yetu ya Igunga, tuna Mahakama ambayo ni ya Mwanzo, ndiyo imekuwa Mahakama ya Wilaya, nasi tunaomba Wilaya yetu ya Igunga ipate Mahakama yenye hadhi ya kuwa na jengo la Mahakama. Mwakani tuongeze fedha, tujenge Mahakama za Wilaya katika Wilaya mbalimbali nchini ambako hakuna Mahakama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata Mahakama za Mwanzo mtuongezee katika ngazi zetu za Vijiji na Kata tupate hizi Mahakama ambazo zitaweza kuwasaidia wananchi kuwapunguzia mzigo mkubwa wa kusafiri kutoka eneo moja kwenda eneo lingine kufuata haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wamekuwa wanasafiri kutoka kilometa zaidi ya 50, 60 mpaka 100 kwenda kusikiliza kesi. Wakati mwingine wanakata tamaa kwa sababu hawana hata fedha za kuwasafirisha kufika kwenye Mahakama hizi. Hii inawapelekea wengine kupoteza haki zao za msingi kwa sababu hawana nauli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara ya Katiba na Sheria watenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama za Mwanzo katika Wilaya mbalimbali. Lingine napenda tu kusema tumeona malalamiko, watu wanalalamika juu ya mabadiliko ya sheria mbalimbali za masuala mazima ya uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2024 ilikuwa mwezi wa Kwanza kwenda Bunge la mwezi wa Pili, Mheshimiwa Rais aliruhusu mabadiliko ya sheria za uchaguzi na tukakaa hapa, lakini pia ikatangazwa Tanzania nzima, na wakaitwa wadau, wengine wakaja hapa Bungeni katika Ukumbi wa Msekwa kutoa maoni juu ya namna gani tunaweza tukafanya chaguzi zetu na zikawa bora?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumefanya mabadiliko ya sheria tatu za uchaguzi. Tumetengeneza Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Tumetengeneza Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na tumetengeneza Sheria ya Vyama vya Siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, malalamiko yalikuwepo, na hasa mengi yaliyotolewa yalikuwa yakihusu Wakurugenzi kusimamia uchaguzi, Wajumbe kuteuliwa na Rais, na jina la Tume. Bahati nzuri nami nikiwa mdau katika Kamati ile, wadau mbalimbali na vyama vyote vya kisiasa vilishiriki na wakatoa maoni yao katika kuboresha sheria hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona katika Sheria za Uchaguzi ambayo tulienda kubadilisha, tukabadilisha. Kwanza walisema jina la Tume tulibadilishe, tukabadilisha. Sasa hivi inaitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambapo walikuwa wanalilalamikia, wanasema hili jina halipo sahihi, tulifanye liwe hivi, tukakubali tukalibadilisha. Hili lilikuwa ni ombi lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, wakasema Wakurugenzi nao wasiwe sehemu ya kusimamia uchaguzi, na yenyewe tumebadilisha. Sasa hivi tumeweka Maofisa Waandamizi kutoka Halmashauri, watakuwa Wasimamizi wa Uchaguzi, maana yake malalamiko yao yote yamefanyiwa maboresho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia juu ya wateule wanaosimamia uchaguzi katika ile Tume Huru ya Uchaguzi, katika malalamiko yao walisema wote walikuwa wanachaguliwa. Ni kweli, kwa utaratibu wa Sheria ya Uchaguzi, Wajumbe wote walikuwa wanateuliwa na Mheshimiwa Rais, lakini katika maboresho sasa Wajumbe karibu wote wanapitia kwenye usaili.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanapopitia kwenye usaili, ni nani anasimamia usaili wao? Wanaosimamia usaili wa kuwapitisha Wajumbe wa kwenda kusimamia uchaguzi wanasimamiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania. Jaji Mkuu ndiye anayewasaili watu wanaotaka kwenda kusimamia kuingia kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Mjumbe mwingine ni Jaji Mkuu wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Mkuu wa Zanzibar na tuna Mwenyekiti wa Haki za Binadamu, naye ni mjumbe katika wale ambao wanakaa kuwasaili Wajumbe watakaokwenda kuwa katika Wajumbe wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa hiyo, unaweza ukaona watu hawa wana uzito na mjumbe mmoja anateuliwa na Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hawa watu wanne wanafanya usaili wa wajumbe kwenda kuingia kwenye Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa hiyo, unaweza ukaona hawa wanaofanya usaili kwa nyadhifa zao ni Jaji Mkuu. Nani anamtilia mashaka Jaji Mkuu? Nani anamtilia mashaka Jaji Mkuu wa Zanzibar? Hawa ni watu ambao wana weledi mkubwa. Ni nani anamtilia mashaka Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu? Ni nani anamtilia mashaka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa ndio wanakaa, wanapitia, kuwafanyia usaili Wajumbe wote. Hata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wanapitia kwenye hii tume, wanapelekwa kwa Mheshimiwa Rais kuchagua katika wale waliopita kwenye hii Tume ya Usaili, ambayo yuko Jaji Mkuu wa Tanzania, yuko Jaji Mkuu wa Zanzibar, yuko Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa vyama vyote vimeshiriki. Leo kinaibuka chama, mtu amechaguliwa juzi tu kuwa Mwenyekiti, wanasema hatuendi kwenye uchaguzi. Hatuendi kwenye uchaguzi, tufanye nini? Tuvunje Katiba yetu? Katiba inasema nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba inasema, kila baada ya miaka mitano tufanye uchaguzi. Sasa miaka mitano imeisha, na hili Bunge ni la mwisho, na hapa zimebaki siku chache twende kwenye uchaguzi. Mtu anasema tubadilishe Katiba. Tubadilishe Katiba kwa Bunge gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Wabunge tuliomo humu muda wetu umeshaisha. Ili tuweze kutengeneza Katiba inayotakiwa na Watanzania, maana yake ni twende kwenye uchaguzi mwaka 2025, tutakaporudi tunaweza sasa tukatengeneza au tukaanza kuunda Bunge la Katiba. Lile Bunge la Katiba ndiyo ambalo litaenda kujadili masuala yote ambayo tunahitaji mabadiliko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba ambao wanatembea huko, wanasema tusiende kwenye uchaguzi. Maana yake kwanza tunavunja Katiba yetu wenyewe, ambapo ni dhambi kubwa tunayotaka kuitenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Katiba inatuambia tufanye uchaguzi kila baada ya miaka mitano. Sasa, sisi hapa tunaenda ku-expire muda wowote. Sasa tunaendaje kutengeneza utaratibu mwingine ambao uko nje ya utaratibu wa Katiba?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba na Watanzania wafahamu kwamba, Wabunge ndio wana jukumu la kutengeneza hayo maoni. Kwa kuwa, sisi Wabunge muda wetu unaenda kwisha, tuombe Mwenyezi Mungu atujaalie tuweze kurudi. Tukirudi tena hapa tutengeneze utaratibu wa kuwa na Bunge la Katiba, maoni yakachukuliwe kwa Watanzania, yaje yachakatwe na baadaye yapitishwe, kama Watanzania wataridhia katika yale ambayo watu wanayahitaji. Kwa sasa hivi, mwaka huu ni wa uchaguzi na kwa sababu ni mwaka wa uchaguzi, tunaenda kwenye uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba Watanzania wote tujitokeze kwenda kupiga kura, kwenda kuchagua Wabunge na Madiwani na pia, kwenda kumchagua Rais ili sasa jukumu lingine la mabadiliko ambayo tunayahitaji ama wanayahitaji yataenda kupitia kwenye mchakato ambao ni rasmi. Tukisema tu tufanye sasa hivi, tunavunja Katiba yetu, lakini pia, ni nani anakubali kutenda dhambi hii? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukiweza kutenda dhambi hii, tukaenda kienyeji, tukajiongezea muda pasipo kufuata utaratibu, Katiba imeshatuambia ukomo wetu ni miaka mitano. Tukaenda kujivunjia kwa sababu tunaamua tu wenyewe kwamba, tuongeze muda tujitengenezee mazingira, maana yake ni kwamba, tuna miaka mingine tujiongezee kama miwili hapa. Kimsingi itakuwa tunavunja Katiba, kwa hiyo, lazima tuchaguliwe kwanza, turudi, halafu ndiyo utaratibu mwingine uweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba, sana sana, wale wote ambao wanahitaji kutengeneza mabadiliko wanayoyataka ni lazima twende kwenye uchaguzi, ili tuweze kupata sasa yale mabadiliko mengine ambayo watu wanayahitaji. Tofauti na hapo, itakuwa ni jinai; tofauti na hapo ni uasi kwenye Katiba yetu na uvunjaji wa Katiba. Maana yake tukitenda kosa hili, kesho na kesho kutwa mtu anakuja kutokea tu anaamua akae kwenye madaraka hapa miaka 20 au miaka 100 kwa sababu, si tunaichezeachezea Katiba! Ni lazima tuiheshimu. Huu ndiyo Msahafu wetu sisi Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Msahafu huu ndiyo unaotuongoza. Tutafanyaje kazi zetu? Ajira zetu zitakuwaje? Tutafanyaje masuala ya uchaguzi na viongozi watapatikanaje kuanzia ngazi ya kitongoji, ngazi ya kijiji, ngazi ya kata mpaka level ya Ubunge pamoja na Rais? Kwa hiyo, huu utaratibu ni lazima tuuheshimu, na ni lazima kama kuna masuala, ambayo yanahitaji maboresho, maana yake sisi Watanzania tuna desturi zetu, tunakaa tunazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alivyoruhusu mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi, kama ameweza kuongeza wajumbe ambao sasa hawateui yeye, katika wajumbe tisa, wajumbe saba hawateui yeye. Wajumbe wote wanapitia kwenye usaili wa Jaji Mkuu wa Tanzania, wanapitia kwa Jaji Mkuu Kiongozi, wanapitia kwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu. Unataka tuwatoe wapi hao wajumbe tofauti na hawa watu wakubwa; tofauti na hawa wabobezi wa Sheria?
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, na Watanzania kwa ujumla, kwa hiyo, nawaomba kwamba, tufuate utaratibu na tunaamini kwamba, jambo hili tutavuka salama. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuwa na utayari wa kuhakikisha kwamba, tutakwenda kwenye uchaguzi mwaka huu kwa sababu, hana tamaa hiyo. Amesema tutafanya uchaguzi mwaka huu, ili Watanzania wachague Rais wanayemtaka, wachague Mbunge wanayemtaka, wachague Madiwani wanaowataka, ili kazi iweze kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo, nakupongeza wewe, na pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kutupatia mialiko kwenda kule Morocco. Huu mwaliko tunaujua, tumeupokea, japo fainali ya mchongo, lakini tunaupokea na tutashiriki. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)