Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Bajeti hii ya Wizara ya Katiba na Sheria. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, yeye ambaye ametupa uzima kwa siku zote hizi kabla ya kuzaliwa kwetu na hata kufikia siku ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo anaendelea kuendeleza Taifa letu na kutuhudumia kwa jinsi ambavyo Mungu anampa afya. Pia, nawapongeza Wizara ya Katiba na Sheria, kwa maana ya Waziri mwenyewe, wasaidizi wake, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, kwa jinsi ambavyo wanaendelea kuongoza Wizara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naipongeza Mahakama yetu ya Tanzania kwa jinsi ambavyo inaendelea kutoa haki kwa wananchi wetu na kuendelea kufanya mhimili huo kuonekana kweli kwamba, ni mhimili unaotoa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu kwa kuipongeza Mahakama ambavyo imejenga jengo ambalo limeshatajwa hapa, ni la sita aidha Barani Afrika au ulimwenguni. Ni jengo zuri na ambalo linaipatia sifa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naipongeza Mahakama kwa jinsi ambavyo inaendelea kuboresha miundombinu ya Mahakama za Wilaya na za Mwanzo na kujenga Mahakama mpya. Hivyo, hii ni kazi nzuri na njema, ambayo inatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais anayependa haki kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninaomba sasa Mahakama, kwa Maana ya Wizara, ikumbuke kukarabati Mahakama za Mwanzo ambazo zimetelekezwa tangu enzi za ukoloni. Majengo ya ukoloni ndiyo yapo mpaka leo hayajawahi kukarabatiwa, mengine yametelekezwa kabisa na hayo maeneo sasa yanaendelea kuwa hayatumiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi, kuna Mahakama kama tano, kwa maana ya Mahakama ya Emaoi, inahitaji irekebishwe, ifanyiwe marekebisho mazuri ili iweze kutoa huduma, ambapo yenyewe inaendelea kutoa huduma mpaka sasa, lakini jengo hilo ni la zamani sana, la kikoloni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Mahakama ya Kisongo, ambayo imetelekezwa pia, haifanyi kazi kwa sasa. Pia, Mahakama ya Musa katika Kata ya Musa kwa sasa haifanyi kazi na jengo lipo, ni yale majengo ya kikoloni. Mahakama ya Nduruma, yenyewe inafanya kazi kwa sasa, lakini bado ni yale majengo ya zamani sana ya kikoloni. Mahakama ya Ngateu yenyewe sasa haifanyi kazi na ni yale yale majengo ya kikoloni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamaanisha kwamba, kwa kuwa, wakati ule wakoloni walipokuwa wamejenga hizo Mahakama watu walikuwa ni wachache. Kwa sasa watu ni wengi, wananchi wamekuwa wengi, migogoro ni mingi, kesi ni nyingi. Hizi Mahakama za Mwanzo zikifufuliwa zitatengenezea Mahakama yetu kutoa haki kwa haraka na kuifanya Mahakama Kuu na Mahakama nyingine za juu ziweze kuwa zinatoa haki kwa mujibu wa utaratibu zilizojiwekea na wananchi wanapata haki kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la marekebisho ya Sheria. Kuwepo kwa sheria yoyote inatokana na kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata haki, lakini pia, kuboresha uchumi wa nchi na kuleta usalama, umoja na mshikamano ndani ya nchi yetu. Jambo hilo limekuwa likifanyika katika nchi yetu mara kwa mara, kama ambavyo inaonekana na inaelezwa kwamba, sheria zinarekebishwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema, mfano Sheria ya Ardhi. Sheria ya Ardhi inahitaji sasa kuangaliwa, kurekebishwa, kwa sababu, kwa mfano kwenye umiliki wa ardhi inakwambia kwamba, mgeni hamiliki ardhi, lakini ukienda kwa undani zaidi ni kama tu anamiliki ardhi, kwa sababu, mtu ambaye ana title ya miaka 99 ni miaka mingapi hiyo? Ni kama anamiliki na baada ya hapo ana uwezo wa kuuza hiyo ardhi kwa kiasi anachotaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ina maana hapo ni kujidanganya kwamba, wageni hawamiliki ardhi, lakini wanamiliki ardhi kwa upande mwingine. Kwa hiyo, hii sheria inatakiwa iangaliwe kwa sababu, bado ni changamoto katika utekelezaji wa umiliki wa ardhi, hasa katika uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ardhi Na. 4 na Na. 5, kama nilivyosema, bado haitoi ule utaratibu wa umiliki wa ardhi. Inakwambia miaka 99, haiji chini kusema labda mtu amiliki kwa miaka, kwa maana ya wageni, wamiliki kwa miaka mitano, miwili, mitatu. Kwa sababu, huwezi kumwambia mtu leo anamiliki miaka 99 halafu unasema ni mwekezaji, bado hii siyo sawa. Iangaliwe hiyo sheria, hayo maeneo ya umiliki wa ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Sheria ya Uwekezaji (Tanzania Investment Act), ambayo ni ya Mwaka 1997 na yenyewe inatakiwa iangaliwe. Kwa mfano, kama kwenye madini tunachukua asilimia tatu, asilimia tatu kwenye madini bado naona ni kidogo, kwa sababu, kama ingewezekana tuongeze na tuangalie sera yetu ya madini, ili tuweze kufanya mabadiliko ya sheria hii, ili iweze kuwa na tija na kujenga uchumi wetu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, madini yamechangia sehemu kubwa sana kwenye uchumi wetu. Sasa hivi iko kwenye 10% ya kuchangia kwenye bajeti ya Taifa. Kwa hiyo, hii nayo iangaliwe, kwa sababu, tukiboresha sheria zetu hizi za kiuchumi tutajenge uchumi wetu wa ndani na kuwafanya wananchi waweze kufurahia rasilimali tuliyonayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakumbuka kwamba, suala la sheria ya utoaji wa haki, kwa maana ya Mabaraza ya Ardhi, kwa kweli yanatakiwa yahamishwe yaende kwenye mkondo wa Kimahakama, jinsi Mahakama ilivyo, kwa sababu, Mabaraza haya hayasimamiwi na mtu yeyote, yanasimamiwa na Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ana muda mrefu kwenda kuangalia kwamba, hiyo Mahakama inafanya kazi namna gani? Hana muda kwa sababu, ana mambo mengi. Mabaraza haya ndiyo yanatoa haki ya ardhi. Ardhi ni mali ambayo ni muhimu sana kwa wananchi wetu wa Tanzania. Sasa ina maana kwamba, haki inacheleweshwa. Unakuta kwenye Baraza la Ardhi kesi inaweza ikapigwa tarehe miezi sita mbele bila kusikilizwa, mpaka mwaka bila kusikilizwa, lakini ukija kwenye Mahakama za kawaida zina muda wa kusikiliza mashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani hebu muiangalie hii kwa sababu, kwa kweli inawatesa wananchi wengi. Madhumuni ya kuwepo kwa haki ni ili mtu apate haki mapema iwezekanavyo, kama ambavyo Katiba yetu inasema katika ile Ibara ya 107(A), ambapo ukisoma Kifungu cha Kwanza na cha Pili, naomba ninukuu Kifungu (b).
Mheshimiwa Naibu Spika, inasema, “Not to delay dispensation of justice without reasonable ground.” Kwa hiyo, Katiba inatusisitiza kwamba, haki lazima itolewe kwa wakati. Aidha, kama umekosa, hiyo ni haki pia; kama umepata, ni haki pia; lakini kuchelewesha haki kwa haya Mabaraza ya Ardhi, pia, naona kwamba, ni uvunjifu wa Katiba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuchelewesha haki itakuwa ni kuwanyanyasa wananchi kwa sababu, hawajui pa kwenda zaidi ya kwenye Mahakama. Kwa hiyo, tunatoa ushauri kwamba, haya Mabaraza sasa imefikia mahali yahamishwe yaende kwenye Mahakama ya kawaida, ili yasimamiwe na Jaji Mkuu na mfumo mzima wa Mahakama. Vinginevyo tutakuwa tunajidanganya zaidi pale ambapo tunasema tunawapa wananchi wetu haki, lakini bado hawapati kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana kuna msemo unasema “Justice delayed is justice denied.” Haki iliyochelewa ni sawa na haki iliyonyimwa. Kwa hiyo, naomba kusema, ushauri wetu au ushauri wangu, naomba sana Mabaraza haya yaweze kuangaliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la msaada wa kisheria unaotolewa na Mheshimiwa Rais; nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ubunifu wake na moyo wake huu wa utashi wa kujaribu kuwasaidia Watanzania, na hasa wale maskini ambao hawana uwezo wa kuweka mawakili binafsi, ili waweze kupata haki zao. Suala hili ni muhimu sana liendelee kutiliwa maanani na litengewe bajeti ambayo inatosheleza, ili wale wananchi maskini wapate haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba twende mbali zaidi katika kuanzisha taasisi ambayo inasimamia kusaidia watu maskini, kama ambayo Rais aliweza kuanzisha, kwa sababu, tukiacha hivi, baada ya muda inaweza ikaja ikapotea moja kwa moja, na ni jambo zuri ambalo limeanzishwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi wote ambao ni Watanzania, na tunaamini katika kupata haki kwa kila mmoja wetu tunaomba sana sheria hizi, zikiwemo na sheria nyingine ambazo nimezitaja hapa, na sheria nyingine ambazo bado zinakuwa hazitoi haki mapema, lakini bado itakuwa haileti kuchochea uchumi wa Taifa kwa haraka, basi ziangaliwe ili ziweze kurekebishwa kwa haraka kwa sababu Bunge hili lipo kwa kazi hiyo. Pia, ninaamini hakuna kiongozi yeyote ambaye atakataa sheria zisirekebishwe, ambazo zinaleta manufaa kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)