Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini vilevile kwa kuimarisha vyombo vyetu vya utoaji haki na usimamizi wa haki kwa mujibu wa Katiba, naomba nimpongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kulitekeleza hilo, naomba niungane na wenzangu waliozungumzia issue ya Samia Legal Aid. Kwa kweli, dhamira ya Mheshimiwa Rais ni nzuri sana, lakini ili tuweze kuiboresha, ninao ushauri kwenye maeneo mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ni kwamba, tuhakikishe kwamba, katika tarafa zetu, kwa sababu, kuna tarafa na kata sita mpaka 10, kwa bahati mbaya sana zote hizi zinategemea Mahakama moja ya Mwanzo, jambo ambalo linawafanya wananchi wanakimbia au wanatembea umbali mrefu, ili kutafuta haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana wenzetu waliangalie hili, ili kuweza kutimiza azma ya Mama kuhakikisha kwamba, wananchi wanapata haki zao sawasawa. Kwa maana hiyohiyo, iko hoja ya Mahakimu wetu kuwa na kazi nyingi kwa sababu, Mahakimu ni wachache, kesi ni nyingi, uwezo wetu mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana wataalamu wetu wale wa mambo wanaohusika na Mahakimu wahakikishe kwamba, wanaongeza idadi ya watumishi ambao wataweza kuhudumu, ili iweze kupunguza mlolongo na msongamano wa kesi kwa Mahakimu wetu. Kweli wana kazi kubwa sana na watu hawa ndiyo wanaanza kufuatilia mienendo ya kesi mpaka waweze kutoa hukumu. Naomba sana Wizara iliangalie hili kwa macho mawili kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kusimamia Wizara hii vizuri, pamoja na taasisi zake zilizo nyingi. Pamoja na hilo, naomba pia kwenye hili Waheshimiwa Wabunge, ni juu yetu kwa sababu, kesi ni nyingi, wananchi wana malalamiko mengi, lakini bado hatujawezesha Wizara hii kupata fedha ya kutosha, ili kufanya Wataalamu wafanye kazi zao vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wenzetu wanaohusika na bajeti, pamoja na bajeti iliyotengwa hapa, ili tuweze kuondoa malalamiko yaliyopo na tuweze kupunguza yatakayokuja, naomba sana tuone ni namna gani tunaweza kuwasaidia kwa kuongeza bajeti kwa sababu, bajeti hii ni ndogo sana kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye ukurasa wa 15 na 16 wa kishkwambi, kwenye bajeti hii, mchanganuo wa matumizi ya kawaida kwa mwaka 2024/2025, kwa mfano, utagundua Ofisi ya Mwanasheria Mkuu mpaka kufikia Februari imepata 49%. Kwenye fedha za maendeleo, hapo hapo tu, wala siendi pengine, imepata asilimia 5.3. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa akili zangu za haraka haraka zinaniambia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ndiyo tunayoitegemea kwenye mambo mengi sana. Kwa hiyo, unapokuwa unaiwezesha kwa staili hii, maana yake ndiyo yale yale aliyosema mtaalamu kwamba, tunachelewesha haki. Tunapochelewesha haki maana yake ni kwamba tumekataa. Kwa hiyo, ombi langu kwenye hili ni bado Serikali ama Wizara iangalie namna gani itaboresha taasisi hizi, ili kuhakikisha wanafanya kazi zao za kutoa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwenye suala la wananchi kuelewa haki zao kwa sababu, mwaka 2021 Serikali ilianzisha issue ya Mahakama Mtandao. Naiomba sana Serikali tuone namna gani tutatoa elimu kwa sababu, inaonekana hata wanasheria au baadhi ya wanasheria hawajui maana ya neno “Mahakama Mtandao.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mimi sikusoma sheria, lakini sina hakika kama tumepewa nafasi ya kuamua wapi naweza kusikiliza kesi? Bunge hili na Serikali tumetunga sheria ili kuhakikisha kwamba tunatoa haki ya kila mwananchi kwa haraka iwezekanavyo. Ndiyo maana leo tumeweza kuweka mifumo ya kusikiliza kesi nchi nzima. Wapo watu leo wanadhani hili hawalitambui wakifikiri kwamba hii siyo sheria. hii ni sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, wenzetu hawa pamoja na kuelewa sheria waendelee kuisoma vizuri sheria kwa sababu haki inatakiwa itolewe popote; uwe Mahakamani ama upo gerezani, iwe wewe ni mfungwa ama wewe ni mshitakiwa bado tunatakiwa tukupe haki yako kwa wakati. Kwa hiyo, Serikali ilipoanzisha Mahakama Mtandao, maana yake ni kwamba imesogeza huduma za Kimahakama kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, na Serikali kwenye hili walichukue sana, wafanye kazi ya kutufundisha na kufundisha public ili waelewe madhumuni ya kuanzisha Mahakama Mtandao ili kuharakisha utaratibu wa kutoa haki kwa wananchi. Hajapewa mtu mamlaka ya kuamua wapi nataka nikasikilize kesi, hii hakuna. Unless, mtuambie kwamba ipo sheria imetungwa kwingine, lakini hapa hatujatunga sheria ya kwamba mimi nataka nisikilize kesi nikiwa nyumbani kwangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana tuendelee kutoa elimu ili watu waelewe kwamba kwenye hili popote tulipowekewa kwa mujibu wa sheria, ndipo ambapo kesi itaweza kusikilizwa. Kwa maana hiyo hiyo, lengo la Serikali na kwa utaratibu wetu wa kisheria taasisi hii ndiyo inayosimamia haki zote, kwa sababu ina vyombo vingi ambavyo vinasimamia haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu, naomba sana, kwa sababu inaonekana tunao mlolongo wa kesi nyingi, inaonekana kama vile wananchi hawaelewi haki zao, inaonekana hakuna anayejua haki yangu nitaipata wapi, nikikosa haki?
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile inaonekana kwamba hata wale wanaosaidia kutoa taaluma ya sheria, bado ni wachache. Ombi langu kwa Serikali tutafute namna nzuri ya kuongeza wasaidizi hawa na kuongeza watu ambao wataendelea kutoa taaluma ili wananchi wa kawaida kabisa waweze kuelewa haki zao watazipata wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, hiyo ajira ,zile za Mahakama ziongezwe ili tuweze kuongeza nafasi na tuweze kutatua matatizo ya haki ya kuwapa wananchi haki zao kwa muda unaostahiki. Nashukuru sana. (Makofi)