Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, umenipa nafasi, nami nichangie Wizara hii muhimu ya Katiba na Sheria. Naomba nianze kwa kunukuu Ibara ya 74 (8) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema: “74.-(8) Bunge laweza kutunga sheria kwa ajili ya kuweka masharti ya kuweka utaratibu wa kusimamia uchaguzi wa Wabunge wanaowakilisha majimbo ya uchaguzi.”
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeanza na quotation hiyo kwa sababu uongo ukisemwa sana na usipotolewa ufafanuzi, unageuka kuwa kweli. Yapo maneno ambayo yanajaribu kupotosha kwamba kitendo cha Bunge na Tume ya Uchaguzi kuwalazimisha vyama vya siasa kusaini Kanuni za Maadili ni kinyume na Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 74(8) ya Katiba, baada ya kutoa mamlaka yao kwa Bunge, mwaka 2024 Bunge hili Tukufu nami nikiwa sehemu ya Wabunge tulitunga sheria mbili. Ieleweke kwamba utungaji wa sheria hizi mbili ulipelekea kufutwa kwa sheria kubwa mbili. Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya Mwaka 1979. Tukatunga sheria na kupitia sheria hiyo tukasema Tume ya Uchaguzi kwa kushauriana na Serikali na vyama vya siasa watatengeneza kanuni za namna bora ya uendeshaji wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Rais, Wabunge na Madiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na masharti yote, mkataba huu ambao Tume ya Uchaguzi ilitakiwa kuutengeneza ulikuwa unavilazimisha vyama vya siasa na wagombea kwanza kujadiliana masharti yapi ya uchaguzi wanayataka, lakini pili wagombea na vyama vya siasa ni lazima wasaini masharti hayo ili kwanza tuweze kufanya uchaguzi wenye staha, uchaguzi wa kuheshimiana, uchaguzi wa kufuata sheria, kanuni, mienendo, taratibu na mila za Mtanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo ndugu zangu wa CHADEMA, wenyewe wanasema kwamba hawapo tayari kusaini Kanuni za Maadili za Uchaguzi. Kanuni hizi zimetoa adhabu kwa chama ambacho kitakataa kusaini masharti ya uchaguzi, na imewekwa clear kwamba watu hao hawatashiriki uchaguzi; na siyo Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 tu, na chaguzi zote ndogo zitakazofuata, mpaka pale watakapotunga masharti mapya 2030. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, chama changu hiki cha CHADEMA kinacho room ya kutoa sababu ya kwanini walishindwa kushiriki kusaini kanuni na wanaweza kushawishi Tume na Msajili wa Vyama vya Siasa ili waweze kusaini masharti haya kwa sababu nje ya hapo, itakuwa ni uvunjifu wa sheria, ni uvunjifu wa kanuni na uvunjifu wa Katiba yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maneno ya wasomi wanasema hakuna kanuni itakayokwenda kinyume na Katiba, it is not true. Kila haki ina wajibu, huwezi kuomba haki wakati hutaki kutekeleza wajibu. Ni kama tu ambavyo leo hii tunasema kwamba huwezi kwenda kupiga kura kama hujajiandikisha kwenye Daftari la Kupiga Kura. Huo ni wajibu wako, kama hujajiandikisha kwenye daftari huwezi kupiga kura.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kulipwa mshahara kama hujafanya kazi. Ili ulipwe mshahara ambao ni haki yako ya msingi ni lazima ufanye kazi. Huwezi kushiriki uchaguzi kama hujakubaliana na wenzio kwamba yapo masharti ya kutunza staha za watu, yapo masharti ya kutunza heshima za watu, yapo masharti ya kuheshimu sheria za nchi ambayo tunakubaliana sisi Serikali, Tume ya Uchaguzi na vyama vya siasa kwamba tutayafuata kwenye chaguzi zote kuanzia 2025 mpaka 2030.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashauri CHADEMA, hakuna namna ya kusema kwamba watashiriki uchaguzi kama hawatakubaliana na Kanuni za Uchaguzi. Naomba nifafanue kidogo kuhusiana na hoja yao ya no reform, no election. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2024 Bunge hili Tukufu kwa weledi lilipitia sheria namba moja na sheria namba mbili ya Tume Huru ya Uchaguzi na likapitia Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za utunzi wa sheria zinataka wale wanaoleta mapendekezo, wakusanye maoni ya wadau; lakini ili kuondoa mashaka katika utungaji wa sheria hizi mbili sensitive, Bunge liliita wadau hapa Bungeni kwa ajili ya kutoa maoni. Chama cha CHADEMA kiliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Chama, John John Mnyika, wakaleta maoni hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, haikutosha,, wakaja Baraza la Vijana wakaleta maoni; haikutosha likaja Baraza la Wanawake wakaleta maoni; haikutosha, wakaleta hilo wanaloliita Bunge la Wananchi, chini ya mama yangu Suzan Lyimo, wakaleta maoni. Kwa taarifa tu, kwenye Bunge hili Tukufu, zaidi ya 95% ya maoni yalitolewa yakachukuliwa yakaingizwa na tukatunga sheria hizi mbili za uchaguzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunajua ndani ya Bunge hili masharti kwamba ya ubadilishaji wa zile sheria yalikuwa ni magumu sana, joto lilikuwa kubwa sana pale Msekwa. Hebu fikiria mazingira ambayo tunataka sisi Wabunge ambao kimsingi ndio tunaoshiriki uchaguzi tubadilishe sheria ambayo kimsingi ilikuwa inawa-favor Wabunge wengi ya kupita bila kupingwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna kifungu kinasema ikitokea vyama vingine vimekosekana kushiriki uchaguzi, basi mgombea huyo atakuwa amepita bila kupingwa. Leo akibaki mgombea mmoja, sheria mpya inasema atapigiwa kura ya Ndiyo na Hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni nani anaweza akakubali kitu cha namna hiyo? Joto la uchaguzi lilivyokuwa kali, lakini Bunge hili liliridhia mtu anapigiwa kura ya Ndiyo na Hapana, na yale yalikuwa ni maoni ya Vyama vya Upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira ya kawaida, Wakurugenzi wa Uchaguzi tulizoea, wana machinery zote za kusimamia uchaguzi, lakini maoni ya Serikali yalikuwa ni lazima wasimamie uchaguzi, na kesi zilipelekwa mpaka Mahakamani. Sisi kama Bunge tukaridhia, na Mheshimiwa Rais akasaini, kwamba sasa Wakurugenzi watakaa pembeni, atasimamia Mtumishi wa Serikali Mwandamizi na atasaidiwa na raia wa kawaida ambao watafanya maombi na watafanyiwa usaili, na watakapofanikiwa wale waliochaguliwa kusimamia uchaguzi kama wasimamizi wasaidizi watabandikwa kwenye Gazeti la Serikali, kila mtu ataona kwa uwazi ili tuweze kuwajibisha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nani anaweza akakubaliana na kifungu cha namna hiyo? Lakini Serikali hii chini ya Mheshimiwa Rais, ilikubali ili kuhakikisha kwamba uchaguzi unakuwa huru na haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wote tunafahamu hapa kwamba, kwenye Sheria ya Tume ya Uchaguzi, lengo la kila chama cha siasa ni kushika dola; na ili ushike dola unajua kwamba kuna mambo ambayo ni privilege utayapata.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais alikuwa na privilege, alikuwa na upendeleo wa kipekee wa kuchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, lakini leo ameamua kijivua madaraka yale, amekabidhi Kamati Maalum, ameweka Majaji, akaweka element ya Muungano, Sekretarieti ya Haki za Binadamu na mjumbe mmoja, na kusema wale ndio watampelekea majina matatu ambayo yata-qualify kuweza kupata Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi. Wanataka tufanye nini ili waweze kuelewa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea ushauri, lakini ni lazima tukubaliane, hapa tusipotoshe umma kutaka kutekeleza jambo ambalo tunajua kwamba hata wale wanaolipendekeza hawajatekeleza wajibu wao. Wote tunajua hapa wanasema no reform, no election, well and good.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa utunzi wa sheria unasema mtu binafsi Mbunge au Wizara yenye dhamana wanaweza kupeleka mapendekezo ya mabadiliko ya sheria au utunzi wa sheria Serikalini. Ukipeleka Serikalini mapendekezo yale yatapelekwa kwenye Baraza la Mawaziri, kwa maana ya Katibu Mkuu na Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuchakatwa yakitoka pale yataletwa Bungeni. Bungeni tutakuwa na public opinion kusikiliza, tukitoka hapo maoni yale yataingizwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo Tundu Lissu, siyo TLS, siyo mwanasheria, siyo Mbunge; hakuna hata mtu mmoja aliyeanzisha mchakato wa mabadiliko ya sheria. Leo unasema no reform, no election! Utafanyaje reform kama mchakato wenyewe wa kubadilisha sheria haujafanyika?
Mheshimiwa Naibu Spika, utafanyaje reform? Hakuna mtu aliyejitokeza, hakuna Mbunge, sio wa upinzani wala wa chama tawala, hakuna Serikali ambayo ime-move motion ya mabadiliko ya sheria hiyo, no reform ni ya kwenye majukwaa! Hatuwezi kukubaliana na jambo hili, tusipotoshe umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimwambie Mheshimiwa Attorney General, ameishauri vizuri sana Serikali kwenye hili, kwa sababu ili tuweze kufanya mabadiliko ya sheria pengine linahitaji muda zaidi, lakini Bunge hili uhalali wake mwisho ni tarehe 27 mwezi wa Sita, likivuka hapo tunakiuka Katiba. Je, wanataka tufanye hivyo? Hatupo tayari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali umeongoza vizuri jopo la mashauriano, nakupongeza. Waziri wa Katiba na Sheria umeongoza vizuri jopo la mashaurino, mimi nawapongeza. Hatuwezi kufanya mabadiliko ya sheria bila kufuata mifumo na utaratibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukubaliane hapa kwamba hakuna Serikali hapa duniani ambayo viongozi na wasimamizi wa uchaguzi wanatoka from the vacuum, haiwezekani. Iwe ni Kenya wanapopasifia, iwe ni Ulaya wanapopasifia, wote wale wanatokana na uteuzi wa Mheshimiwa Rais, wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, na ndiyo maana ya uchaguzi wa mwaka 2015, tofauti ya kura ilikuwa ni ndogo sana kwa sababu mgombea wa upinzani aliweza kusimama akamshawishi msimamizi wa uchaguzi wa kwenye kata yangu kule Ibadakuli, akamshawishi msimamizi wa uchaguzi pale Shinyanga, akamshawishi Mheshimiwa DC, pengine akamshawishi Mkuu wa Mkoa, vyombo vya dola na ndiyo maana tofauti ya kura ikawa ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani under the sun wewe huwezi kushawishi vyombo vyote hivyo halafu unataka Tume ya Uchaguzi itoke kutoka kwenye roboti, haiwezekani! Ni lazima tuweke candidate wenye ushawishi ambao wanaweza kushawishi kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya kijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tofauti na hapo, ukiweka wanaharakati, ukaweka watu wanaopiga kelele majukwani; hata viongozi wa dini hawapendi viongozi wanaotukana matusi hadharani, hawapendi viongozi wanaodhalilisha watu, na hawependi viongozi hawaheshimu mifumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu anataka kiongozi ambaye anaheshimu demokrasia na amani ya nchi. Kwa maana hiyo, mimi nawashauri ndugu zangu, sisi tunakwenda kwenye uchaguzi; it is either waende wakasaini fomu za maadili au wajitoe na hawatashiriki uchaguzi mpaka 2030. Huo ndiyo ukweli, na tusipotoshe jamii kwa kusema kwamba…
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Nani Taarifa?
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni mimi hapa.
NAIBU SPIKA: Wewe nani? Simama basi nikuone. Huonekani.
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, Stella Fiyao, kushoto.
NAIBU SPIKA: Haya. Mheshimiwa Stella.
TAARIFA
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka kumpa tu taarifa Mheshimiwa mzungumzaji kuwa hata maandiko matakatifu yanasema, iheshimuni sana mamlaka maana imetoka kwa Bwana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salome, nimekuongezea muda kidogo.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa ya mdogo wangu Mheshimiwa Stella Fiyao. Ukweli ni kwamba hata wao wakifanikiwa kuingia madarakani, yaani wataona hii sheria kama Mheshimiwa Rais, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa ameilegeza sana. Wataona kama ilikuwa imelegezwa sana. Sidhani kama kwa utashi walionao wanaweza wakakubali eti washauriwe na kuletewa majina matatu ya Msimamizi wa Tume Huru ya Uchaguzi, sidhani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kwa dakika moja, ipo initiative kubwa inafanywa na Wizara inayohusiana na utoaji wa msaada wa kisheria. Mimi nipo kwenye legal field, kama kuna jambo gumu linalowafika Watanzania, ni namna ya kufikia haki yao ya kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa watu wanafanya jambo kubwa sana, lakini changamoto kubwa ninayoiona ni muda wanaopata katika maeneo wanayokwenda kutoa msaada wa kisheria. Changamoto ya pili, ni uwezo wa kifedha kwenye mfuko wa Samia Legal Aid Campaign. Hii kampeni imebeba jina kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kada ya kisheria ni moja kati ya kada ambazo ni ngumu kidogo kwenye nchi hii. Nashauri kwamba ili kuleta ufanisi na tija kwenye nchi hii, mfuko huu upewe fedha maalum, na utengewe bajeti ya kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao, nakushukuru. (Makofi)