Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti hii ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema, amenipa kibali cha kuchangia mchango huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo alituletea msaada wa kisheria kule Mkoa wa Mbeya. Wananchi walio wengi sana hasa wanawake wa Mkoa wa Mbeya walikuwa wanashindwa sana kupata fedha kwa ajili ya kuendesha kesi Mahakamani ili wawalipe Wanasheria, lakini Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa msaada wa kisheria ili kila mwananchi ambaye hana uwezo wa fedha kwa ajili ya kuendesha kesi zake, aweze kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amewaona wananchi wa Tanzania na hasa wananchi wa Mkoa wa Mbeya. Tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitamani kushauri jambo muhimu kwa jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais amejitoa kutoa msaada wa sheria. Pale kwetu Mbeya wananchi zaidi ya 200,000 wamepata msaada wa kisheria, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuishauri Wizara hii waandae makala maalum ambayo inaonesha namna ambavyo Mheshimiwa Rais amejitolea kusaidia msaada wa kisheria kwa wananchi mbalimbali. Kwenye Makala hiyo kiandikwe kichwa cha habari ambacho kinamsema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, maana hili lisije likapita bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niingie kuishauri Serikali kwa upande wa NIDA. Wananchi walio wengi walijitokeza kujiandikisha ili waweze kupata vitambulisho vya NIDA. Naomba kushauri, kasi ya kutoa vitambulisho vya NIDA iongezeke, kwa maana kipindi wananchi wamejitokeza kwa wingi wapo wananchi ambao mpaka sasa hivi hawajapata vitambulisho vya NIDA ila wana namba za utambulisho kwamba wao ni raia wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana ndugu zangu ambao wanahusika na mambo ya NIDA, wafanye utaratibu wa kutoa vitambulisho vimfikie kila mwananchi aliyejiandikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo lingine la kushauri hapa. Huko magerezani kuna wafungwa. Hao wafungwa ni binadamu kama binadamu wengine. Nashauri Serikali, kipindi cha uchaguzi, wafungwa hao nao wawe na haki ya kupiga kura kuwachagua viongozi ambao wanaona kwamba wanawafaa katika nchi yao ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, kuna wahalifu ambao wanahukumiwa miaka miwili, mitatu. Naomba niishauri Serikali, hao wananchi ambao wamefungwa kifungo hicho cha miaka miwili mpaka mitatu, basi wasikae bure gerezani. Wapewe kazi ya kufanya; walime mashamba, ili wakitoka huko wawe wamejifunza kitu kikubwa. Maana nchi yetu ni kubwa sana, ina mashamba maeneo mengi, hiyo itasaidia kuondoa uhalifu kwenye Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa pongezi ambazo Wabunge wamechangia hapa wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa namna ambavyo wanatuasa wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwamba tuhakikishe tunamrudisha Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana Naibu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, aliongea hapa, kwamba, “wananchi wa Mbeya, ninawashauri sana msiache kumrudisha Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Bungeni.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea shukrani nyingi sana, lakini pia tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge. Wananchi wa Mbeya Jiji niliwapongeza na ninawapongeza sana kwamba mlimchagua Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, pia mlimpa baraka ambayo wananchi waliendelea kumwombea Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson. Alipofika hapa akagombea nafasi ya Uspika, nawashukuru sana Kamati Kuu walipendekeza jina la Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, na lilipofika Bungeni, Wabunge wote tulimpa kura za kutosha akawa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru kipekee wananchi wa Mkoa wa Mbeya, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumpa kibali Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, kwenda kugombea nafasi kubwa ya kuwa Rais wa Mabunge Duniani. Tunashukuru wa support hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya, kwa heshima waliyopewa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na ushauri wa kila Mbunge mmoja mmoja aliyeshauri hapa, tumchague kwa heshima Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, ili arudi hapa. Tumeupokea na tunaufanyia kazi, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ni mpakwa mafuta wa Mungu, Mwenyezi Mungu amemnyooshea mkono. Siamini kwamba kuna mtu atajitokeza kupingana naye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaheshimu mamlaka, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, heshima kubwa aliyotupatia wananchi wa Mkoa wa Mbeya, tumeipokea kwa dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakushukuru sana kipekee hata wewe namna unavyoongoza Bunge hili Tukufu, Mwenyezi Mungu asikupungukie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushauri upande mwingine kuhusu Mahakama. Kuna wakati fulani Mheshimiwa Hakimu ama Mheshimiwa Jaji anavyotoa hukumu, wale ambao walikuwa wana kesi pale, nakala za hukumu hawapewi kwa wakati. Hilo limekuwa ni changamoto kubwa sana kwa sababu wananchi wengi sana wanasumbuka kupata nakala za hukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri sana kwa upande huu, pale ambapo Mheshimiwa Jaji au Mheshimiwa Hakimu anapotoa hukumu, si anasoma, basi pale pale ziwe zimeshaandaliwa nakala za hukumu ili wale ambao walikuwa wanahukumiana kesi wawe wanakabidhiwa nakala zao pale pale kwa sababu hii imekuwa ni changamoto na kero kubwa sana. Wananchi wanasumbuka kufuatilia nakala za hukumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa kuendesha kesi, mfano kesi za mauaji, katika suala la namna ya upelelezi, wanasema ndani ya miaka 10 ndipo ambapo kesi zinakuwa zinaanza ama kuendeshwa. Wananchi walitamani sana angalau basi wafanye kwa miaka mitano ndipo mambo mengine yaendelee. Hilo lingekuwa jambo jema sana ambapo wananchi ingewapunguzia shida mbalimbali wanazozipata ndugu zao wanapokuwa magerezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kushauri kwamba Mahakama za Mwanzo zimesahaulika sana katika kufanyiwa ukarabati, hasa zile Mahakama kongwe. Naomba mtupie jicho hapo na Mheshimiwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama yuko vizuri sana, namwelewa vizuri sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo.

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja. Ahsanteni kwa kunisikiliza. (Makofi)