Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara yetu hii muhimu ya Katiba na Sheria. Kabla sijachangia mengine ambayo ninawiwa sana, niendelee tu kuipongeza Wizara kwa jitihada inayofanya kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri. Pia nampongeza Mwanasheria Mkuu wetu kwa sababu amekuwa akiendelea kufanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya tofauti kabisa, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mama yetu kipenzi kwa namna ambavyo ameweza kuanzisha kampeni mbalimbali za utoaji wa huduma za haki kwa jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia, nilitamani nami nianzie kwenye kipengele cha Legal Aid Campaign ambapo tumeona kabisa Serikali yetu Tukufu ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wamekuja na kampeni ya utoaji wa msaada wa kisheria kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kabisa kwamba wananchi wengi wana changamoto ya upataji wa haki. Wanakuwa hawajui mambo gani ni haki zao na pia ni wapi watapata hizo haki zao na ni akina nani wana wajibu wa kuwapatia hizo haki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa elimu hii ambayo inaendelea kutembea kwenye jamii yetu, sisi tunaishukuru Wizara, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na tunampongeza kwa kweli kwa moyo huo wa kizalendo na kibinadamu na kama tunavyoona kaulimbiu ya CCM mwaka huu ni Kazi na Utu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kitendo cha kuanzisha kampeni kama hizi, inadhihirisha kabisa kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ana utu kwa kiwango gani, na anatamani kuona nchi yake inaongozwa kwa kuwa na upendo na utu kwa kiwango gani? Kuhusu hilo, naomba wanifikishie salamu zangu kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mikoa karibu 25 ambayo wameshafika mpaka sasa hivi. Wanaenda wanatoa huduma, wanahama, wanaenda maeneo mengine wanatoa huduma, lakini kwa takwimu walizotuonesha hapa, inaonesha ni wananchi karibu 2,698,908 wameshawafikia. Hii idadi siyo ndogo, na siyo ya kuipuuza. Kwa hiyo, tunawapongeza sana kwa kuweza kuwafikia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu katika hili, ni kwamba wakati wa utekelezaji wa zoezi hili, tumeona kuna baadhi ya changamoto ambazo zinajitokeza. Mfano, ushirikishaji kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na vyama vya kisiasa ulikuwa mdogo. Sasa natamani wanapoendelea na zoezi hili, kwa sababu ninaamini wamepita na wataendelea kupita, wanapokuwa wanafanya mazoezi haya, viongozi wa kisiasa kama Wabunge, Madiwani wahamasishwe, wawe sehemu ya kushiriki hizo kampeni zinazokuwa zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mungu, kwenye Mkoa wangu wa Songwe nadhani nilikuwa ni Mbunge pekee niliyeshiriki siku ile. Siyo kwamba barua hazikutolewa kwa Wabunge na huenda wakati mwingine hiki kitu kwa Wabunge unakuta hakifahamiki kwa uzuri, kwa hiyo, nayo inakuwa ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika zoezi lile sikuwaona Madiwani mkoa ule wakishirikishwa wote. Kwa hiyo, hili nalo niliona kuna gap la ushirikishwaji wa Madiwani kwenye utekelezaji wa zoezi hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani may be wanapoenda kwenye wilaya watawashirikisha wale Madiwani, lakini bado nilivyofuatilia niligundua kwamba kwenye ngazi ya wilaya na zile kata walizoenda Madiwani hawakushiriki zoezi hili kikamilifu na tunajua Madiwani ndiyo watu wanaoishi na wananchi na ndiyo watu wanashinda na wananchi kila siku ambao wanaweza at least hata kuwafafanulia wananchi kwa habari ya mambo haya yanayofundishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukasema unamfundisha mwananchi habari ya haki wakati kiongozi wake anakuwa hafahamu hiyo haki inapatikanaje na inatolewa na nani? Wakati gani anaweza akaipata? Kwa hiyo, hilo nilitamani kuomba Wizara iweze kulichukua na wakati mwingine waweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina ombi lingine la ziada kwamba wanapokuwa wanatekeleza hizi kampeni, wajaribu kugatua, yaani itoke kwenye ngazi ya Kitaifa iende kwenye ngazi ya mikoa na wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukaniambia kwamba kampeni iwe inafanyika kwa rotation wakati hili ni zoezi endelevu. Upotevu wa haki za watu ni tendo endelevu. Mtu atakosa haki yake leo, lakini unakuta hata wanaopoteza haki wakati huo unakuta elimu hiyo ilikuwa inatolewa, wengine hawakuwa na access ya hiyo elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natamani zoezi hili la elimu au hii Legal Aid Campaign ishushwe kwenye ngazi ya wilaya na tena itengewe bajeti ya kutosha ambayo itawawezesha wale watoa huduma hizo kwa wananchi waweze kupata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kabisa wahanga wa haki hizi ni wanawake na watoto na makundi maalum ambayo yako katika hali hatarishi ya kunyanyasika au kufanyiwa ndivyo sivyo. Tunafahamu kabisa wanawake wengi wanadhulumiwa mali, wanafanyiwa vitendo vya ukatili na hata sehemu ambayo wana haki na hilo jambo, wanafanyiwa vitendo vya ukatili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafahamu watoto wetu wanafanyiwa matendo ya ukatili mengi, japo siku hizi kuna kampeni za kuibua kero za wanaume ambao nao wanafanyiwa ukatili. Hata hivyo, bado kesi zinaonekana wanawake wengi na watoto wengi na watu wenye mahitaji maalum ndiyo wanaofanyiwa ukatili mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa na ombi. Kwa kuwa wahitaji ni wengi, naomba huduma hizi washushe hadi ngazi ya wilaya ili tunavyoendelea mbele, basi ziendelee kushushwa hadi ngazi ya kata, kama ambavyo huduma nyingine za ugani zimeweza kushushwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwenye habari ya mambo ya ukatili wa kijinsia, nina ombi moja. Mkoa wangu wa Songwe katika Wilaya yetu ya Momba Mji wa Tunduma ukatili umekuwa ukiongezeka siku hadi siku. Sisi kama viongozi wa eneo lile tunaumia, na tunaumia sana kwa sababu tunaona kama watu wetu wananyanyasika, na ufuatiliaji wa mashauri kwa wale watu wanaokuwa wanafanya vitendo hivyo vya ukatili tunaona kama hayachukuliwi kwa uzito huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naiomba Serikali yangu, kwamba Mji wa Tunduma kulingana na wingi wa malori ambayo yako pale, vitendo vya ukatili vimeongezeka kwa kiasi kikubwa ikiwezekana waweke kambi maalum ya kuhakikisha wanafanya utatuzi wa changamoto zinazopatikana eneo lile. Pia, waje na mbinu mbadala za kuwasaidia wananchi wa eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kituo cha polisi cha pale hakina uwezo mzuri, ukiangalia Mahakama, hatuna majengo mazuri kwa Wilaya ya Momba. Hilo pia nilikuwa natamani Wizara kama Wizara, Mji wa Tunduma, Halmashauri ya Momba waitazame kwa jicho la tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia baada ya kuongea hayo nilitamani niwaombe, suala la kuwapa dhamana watu wanaowabaka watoto wetu wadogo likose dhamana, kwa sababu haiwezekani mtu anabaka halafu mtu huyo huyo anaenda kupewa dhamana. Hivi mtu anambaka mtoto, wewe huwezi ukaona kwamba hilo ni kama kosa la uuaji? Anawezaje kuthubutu? Kwa hiyo, nilitamani suala la kukatili watoto sheria yake itungwe na wakose dhamana. Tunaumia sana kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kuongea na Waziri, baba yetu Mheshimiwa Ndumbaro aweze kutusaidia. Aliniahidi Wilaya ya Ileje kutupatia Mahakama mbili. Jana nilimwuliza swali la msingi kuhusiana hatua za ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Ileje inaendeleaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba Wilaya ya Ileje hata ujenzi haujaanza. Kwa hiyo, namwomba Waziri atakapokuwa anafanya finalization aje anipe kauli ya kwamba ni lini anapeleka fedha za kuanza ujenzi wa Mahakama ya Wilaya kwenye Wilaya ya Ileje?

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani Wilaya ya Ileje na ukongwe wake mpaka leo haina Mahakama hata moja. Huduma za Mahakama zinatolewa kwenye majengo ya upangishaji tena majengo ya CCM yaliyochoka. Kwa hiyo, namwomba Waziri atusaidie, Wilaya ya Ileje tunahitaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama. Basi aanze hata na hizo wilaya nyingine, kwenye tarafa nyingine atafanya wakati mwingine kama ikishindikana kupata fedha zote. Ahadi ni deni, leo nimekuja kumdai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, natamani kuongelea kipengele cha haki za binadamu. Sisi wengine ni waumini wa haki, yaani ukitaka kukosana nami, onesha unamnyima mtu mwingine haki au unaninyima haki yangu. Hapo naweza nikavua viatu na nikakubali kupambana na wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mama wa wafungwa. Nilishajitolea kuwa msemaji wa wafungwa wasiokuwa na wasemaji. Humu ndani hatuna mwakilishi wa wafungwa hata mmoja. Wafungwa wanateseka. Sheria inatambua haki za binadamu, pamoja na mfungwa, kwani naye pia ni binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani mfungwa makazi yake yanakuwa ni sawasawa na eneo ambalo hata wewe ukisema tu ukasimame au ukae, huwezi. Imagine rumande mtu anakunya kwenye ndoo, wewe unawezaje? Kwa hiyo, niseme, maliwato ya wafungwa yaboreshwe. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante. (Makofi)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, wafungwa wapewe na magodoro. Kama hawawezi, wawaruhusu wayalete, wenye uwezo na wana ndugu na jamaa wanaweza kuleta magodoro yao ya kulalia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)