Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niwe mchangiaji katika Wizara hii muhimu. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema kwa kunijaalia afya na kuweza kusimama leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mheshimiwa...
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, namwita Mwenyekiti kunipokea kwa dakika chache, endelea tu Mheshimiwa Kandege.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mwenyekiti anakuja, hatua ya pili ilikuwa nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri sana ambayo ameifanya katika maboresho na kuhakikisha kwamba haki inatolewa kwa wakati. Hili jambo linawezekana katika nchi chache Afrika na Tanzania tukiwa vinara. (Makofi)
Hapa Mwenyekiti (Mhe. Joseph K. Mhagama) Alikalia Kiti
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti. Nimepata fursa ya kuongea na Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Mheshimiwa Waziri, na Naibu Waziri. Kwa hiyo, tulipata fursa ya kupata mengi juu ya maboresho makubwa ambayo yamefanyika kuhusiana na suala zima la utoaji haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata historia moja nzuri sana ambayo Mtendaji Mkuu wa Mahakama alituambia sisi Wajumbe wa Kamati kwamba, kuna kipindi ambapo ilikuwa inatakiwa ushahidi utolewe na mtu ambaye yuko Marekani. Sasa akawa anaomba kwamba itabidi asubiriwe kipindi ambacho atapata likizo, maana anafanya kazi Marekani. Pia, ajikusanye atafute tiketi ili aje Tanzania, na suala lenyewe lilikuwa linahusu mambo ya sheria za ndoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa akaambiwa kwa advancement na kazi nzuri ambayo imefanywa Tanzania na maboresho ambayo yamefanywa chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huna sababu ya kupoteza muda wako kutafuta tiketi wala kutafuta likizo eti kuja kutoa ushahidi wako. Tanzania hii, akaambiwa tunachotaka kwako wewe utuambie muda wako, lini utakuwa uko tayari. Tunahitaji hardly saa mbili maximum, ukiwa Marekani huko huko sisi tutapata ushahidi wako. Hakuamini, lakini hicho ndicho kilitokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, akawa anatoa ushahidi na yeye mwenyewe anajiona, na akauliza maswali mpaka akaridhika. Alidhani kwamba labda haya yanawezekana Marekani, lakini hayo yanawezekana kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hongera sana Mheshimiwa Rais katika kuhakikisha kwamba haki inapatikana kama nchi ambazo zimeendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi na maboresho makubwa ambayo yamefanyika, naomba niongelee ndani ya Wilaya ya Kalambo na Jimbo la Kalambo. Naomba niendelee kumshukuru Mheshimiwa Rais, Waziri, Naibu Waziri, na Mtendaji Mkuu wa Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji Mdogo wa Matai ni miongoni mwa miji ambayo imepangwa kisasa. Kwa hiyo, pale ambapo Serikali inaleta majengo, nataka yalingane na hadhi ya jinsi ambayo tunapanga mji wetu. Nashukuru, ujenzi wa Mahakama ya kisasa wa thamani ya shilingi bilioni 1.5 unaendelea na mkandarasi yuko site. Naishukuru sana Serikali kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya Kalambo tuna jumla ya tarafa tano, tuna jumla ya Mahakama za Mwanzo tano, lakini cha ajabu Tarafa ya Mambwenkoswe haina Mahakama ya Mwanzo hata moja, na hii ni tarafa ambayo iko mbali sana. Tafsiri yake ni kwamba, wananchi ambao wangependa haki yao ipatikane kwa wakati, wanakosa kupata haki yao ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya utayari, tayari wameshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo. Nami natamani Mahakama ya Mwanzo ingejengwa jana. Kwa hiyo, naomba, na nilipata fursa ya kuteta na Mheshimiwa Waziri, akasema, kwa mujibu wa sera hii tarafa inastahili kujengewa Mahakama yake ya Mwanzo ili vijiji hivi 16 ambavyo wananchi wanataka kupata haki zao kwa muda muafaka, waweze kupata haki bila kutembea umbali mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, katika Mahakama zetu tano, Mahakama mbili zina hali nzuri ikiwemo Mahakama iliyopo Sopa na Mahakama iliyopo Msanzi. Mahakama inayojengwa Kasanga iko kwenye hatua nzuri, naipongeza Serikali. Kazi ambayo naiomba Serikali, pamoja na kuhakikisha kwamba tunaenda kujenga Mahakama ambayo haipo katika Tarafa Mwambenkoswe, lakini haipendezi pale ambapo ukienda kutazama Mahakama iliyopo Kijiji cha Mwimbi Tarafa ya Mwimbi ilijengwa kipindi cha mkoloni. Pia, Mahakama ya Mwanzo iliyoko Tarafa ya Mwashe na Kijiji cha Mwashe nayo ilijengwa kipindi hicho hicho cha mkoloni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati mwafaka sasa maboresho yafanyike. Pia, ikiwezekana, kwa sababu wakati mwingine ukarabati unakuwa ni gharama zaidi, ni bora ukaanzishwa ujenzi mpya ili tuendane na hali ya sasa ya majengo, kwani wananchi wa Kalambo wanapenda vitu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo eneo lingine ambalo naomba nichangie. Nalo ni kazi nzuri ambayo inafanyika kuhakikisha kwamba haki inatolewa, lakini haki ikicheleweshwa au mtu akilazimika kutafuta haki kwa kutembea umbali mrefu, jambo hili halina afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kalambo hatuna Baraza la Ardhi la Wilaya. Kwa hiyo, mashauri yote ambayo yanahitajika yapate ufafanuzi na ufumbuzi kupitia Baraza la Ardhi yanaishia ngazi ya kata. Yakishaishia ngazi ya kata, pale ambapo rufaa inatakiwa ifuatwe kwa maana ya kwenda Wilayani, kwa sababu Kalambo hakuna Baraza la Ardhi la Wilaya, wananchi wa Kalambo wanalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kutafuta haki yao Sumbawanga Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake ni nini? Mwananchi huyo lazima ajipange, maana huwezi ukahudhuria siku hiyo hiyo. Lazima atafute sehemu ya kufikia, lazima atumie nauli, lazima ajipange kwa chakula. Kwa hiyo, inafikia wakati mwingine mwananchi anaona kuliko kupata adha hii, wanaamua kumalizana kwa namna ambayo haki inakuwa haitendeki. Kwa malengo mazuri ya Wizara hii, sidhani kama mngependa jambo hili litokee. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limekuwa likiongelewa muda mrefu. Sijajua ni kwa nini hatupati ufumbuzi kuhakikisha kwamba Mabaraza ya Ardhi yanafanya kazi kama ambavyo Mahakama zinafanya kazi. Kuna kipindi mchakato ulionekana karibu unakamilika, lakini kuna habari ya kurudi nyuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, wakati hiyo michakato inaendelea, basi kama hakuna gharama kubwa sana mtutengenezee utaratibu ili wananchi wa Kalambo wakati wanasubiri utaratibu mwingine, Baraza la Ardhi la Wilaya lianzishwe, maana sisi ni Wilaya ambayo iko fully fledged. Hakuna sababu ya kwenda kulazimisha kukaa kwa ndugu ambaye sio ndugu yako eti kwa sababu umeenda kufuata haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru sana, nimemwona Waziri anatikisa kichwa kwamba wananchi wa Tarafa ya Mwambenkoswe, watafikiriwa. Kwa hiyo, atakapokuja kuhitimisha atasema namna gani tunaanza kwenda kujenga Mahakama ya Mwanzo katika Tarafa ya Mwambenkoswe ambayo haina Mahakama hata moja ya Mwanzo. Vijiji 16, kata tatu tunasubiri kauli kutoka kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)