Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Moshi Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Katiba na Sheria. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na timu nzima.
MWENYEKITI: Samahani Mheshimiwa Mchangiaji. Sekunde chache tafadhali.
Hapa Naibu Spika (Mhe. Mussa A. Zungu) Alikalia Kiti
NAIBU SPIKA: Endelea.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nilikuwa naendelea kutoa pongezi kwa timu nzima za Mahakama, Mabaraza ya Ardhi, pamoja na timu zote ambazo zinahusika katika mlolongo mzima wa kutoa haki. Tunaelewa kwamba wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana kutokana na uelewa wa watu na mazingira ambayo tunakabiliana nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumpongeza kwanza, Mheshimiwa Rais kwa Samia Legal Aid, ilishafika Moshi Mjini na kwa kweli hata kwetu ilileta matumaini makubwa sana kwa watu, na watu walitamani ikae muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba, tuweze kuhakikisha tunapata fedha zaidi kwa ajili ya kuendesha zile kampeni ili ziweze kukaa kwa muda mrefu zaidi. Pia, tuzishushe chini zaidi zifike maeneo ya chini kwa wananchi mpaka kwenye ngazi za mtaa. Kwa hiyo, napongeza sana. Imefika mikoa 25, watu milioni mbili, na inaonyesha taswira halisi ya kiu ya watu ambao hawajapata haki kwa kupitia mifumo ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni jambo ambalo tunapenda ku-encourage liwepo kwa sababu limeweza kutoa haki kwa wale ambao wamekosa haki kwa mifumo ya kawaida kutokana na changamoto mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niangazie eneo la ardhi. Nadhani katika maeneo kwenye Mkoa wetu wa Kilimanjaro na hata pale Moshi ambapo tuna changamoto za kisheria, ni eneo la ardhi. Sasa, naomba sana tuangalie namna mbadala. Baraza la Ardhi limeleta mafanikio, lakini bado lina changamoto ambazo zinaikabili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri tungetafuta chombo ambacho kinaweza kuwa mobile, badala ya watu kufuata, kwa sababu ardhi siyo mobile, tuwe tuna chombo ambacho kinaweza kwenda kule kwenye kata, kwenye mitaa, na kwenye vijiji ili kishirikishe wale wananchi, haki ingeweza kupatikana kirahisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata kama sijui tutafuta kitu gani, kitu ambacho kitajumuisha mamlaka zote zinazohusika na ardhi, lakini kiweze kwenda kule kwenye matatizo. Kwa sababu, hao watu wanaokuja huku saa nyingine mimi nafahamu hata kwenye taasisi hizi za kifedha, kuna sheria inasema, kama ni mwanafamilia unaweka labda hati kwa ajili ya collateral, lazima uende na mke. Sasa, hakuna mechanism sahihi ya kuonyesha kwamba huyu ni mke wa mhusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta watu kwenye familia mtu anachukua hati, anaenda kwenye taasisi za fedha, anaenda na mtu ambaye anasema ni mwenza, lakini siyo mwenza. Tukienda kule chini ambako wako pale na majirani wanajua, hii haki haswa kwenye ardhi inaweza ikapatikana kirahisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuliangazia ni eneo la wosia. Hakuna Mbunge ambaye katika matatizo yanayofika kwenye ofisi yake, matatizo ya mirathi hayapo. Sasa, mimi nadhani tumeona hapa kwamba talaka sasa zimefikia 16%; hilo ni tatizo; lakini hivi vitu vinaenda kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, 16% kwenye eneo la talaka maana yake tayari kuna tatizo kwenye hii taasisi ya ndoa. Najua, kuanzia kwenye ngazi za maendeleo ya jamii au ustawi wa jamii, focus kubwa siyo kuachanisha watu, lakini ni kutatua changamoto ambazo wanazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kwa hizi asilimia tunazokwendanazo, moja, tunakwenda kutengeneza Taifa la watu ambao hasa wale watoto (tuache hawa ambao wameachana) ambao wanaachwa hapo Katikati, wanakuwa tayari wanapata shida kubwa sana ya malezi hasa kwenye malezi haya ya kawaida ya kifamilia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, tuangalie namna ambavyo katika mifumo yetu ni namna gani zaidi tunaweza kupata suluhisho badala ya kwenda kwenye kuachanisha hawa watu kwa maslahi makubwa ya wale watoto. Zaidi ya hayo, ikibidi lazima hao watu waachane, basi ni namna gani watashiriki kwa ulazima kuwalea wale watoto pamoja?
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu kwenye nchi zilizoendelea ni kawaida kabisa watu kuachana, lakini malezi ya watoto wana-share. Hapa kwetu watu wanaachana, lakini malezi ya watoto hata kama wana-share, lakini wanawachanganya wale watoto kwa sababu huyu anamwambia yule ni mbaya, akienda kwa huyu anamwambia yule ni mbaya, psychologically tunawaharibu wale watoto. Kwa hiyo, nadhani kuna haja ya kuliangalia hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi hapo kwenye wosia. Watu wengi hasa kwenye jamii zetu wanaogopa kuandika wosia kwa sababu wanaona mara moja tu kwamba nikianza kuandika wosia najiandaa kufa, au ili niandike wosia mpaka niwe nimezeeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, badala ya kwenda kwenye wosia moja kwa moja, mimi nadhani ni vizuri katika kila kitu ambacho watu wanamiliki kama inavyokuwa kwenye benki kuna Next of Kin, waandike. Kama ni kwenye ardhi awe ameandika pale. Hati ya ardhi, kama ni wazazi waende wakubaliane mume na mke kwamba Next of Kin wa hii ardhi yetu tukiwa hatupo ni nani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama wana watoto, automatically haki ya watoto ilindwe, wale ambao ni chini ya miaka 18, lakini kama ni zaidi ya miaka 18 wawe na nafasi ya kuandika na wawe wana-review kama tunavyofanya kwenye kulipa Land Rent.
Mheshimiwa Naibu Spika, wanapoenda kulipa Land Rent waandike Next of Kin, kwamba wakiwa hawapo ni nani aweze kuchukua hiyo kama ni property, kama ni Bank Account, kuyapunguza haya. Kwa sababu ingetokea hata wale ambao ni wasimamizi wa mirathi wamekuwa pia sio watu waaminifu, kitu kinachosababisha matatizo makubwa kwenye jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye eneo ambalo nimeona tunakazania sana kuwa na sheria ambazo zitawabana watu wa shisha na watu wa betting. Nadhani hapo kuna maeneo mawili ya kuongezea. Pamoja na shisha na betting, kuna pombe kali zisizokuwa na viwango vinavyotakiwa. Hii trend ya shisha, actually inaenda kwa watu wenye uwezo kidogo, wa kishua ambao ni wachache, lakini hizi pombe kali ambazo hazina viwango, zinakwenda kwa wale watu wa chini kabisa ambao ni wengi. Kwa hiyo, hizi sheria zi-upgrade. Hiyo shisha, betting, na pombe kali zisizokuwa na viwango, nayo tuangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine tunaangalia suala lingine ambalo kwetu linaweza kuwa na tija. Tunaangalia haya masuala matatu niliyoyataja kama masuala makubwa ambayo yana matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nilisema, waendesha bodaboda na bajaji hawana leseni. Leseni ni chanzo cha mapato kwa Serikali. Wao hawa-qualify kwa sababu leseni ya kawaida ya daraja la chini nilisema tena ni karibu shilingi 340,000 kupata, kwa sababu unaanzia driving school, lakini wako barabarani hawana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusipitishe sheria ambayo wale ambao tayari wako barabarani, wana pikipiki na bajaji hawana leseni, tutoe fee ndogo kama ni shilingi 50,000 wafanyiwe test tu na Polisi? Anajua sheria za barabarani, anajua kuendesha, apewe leseni. Badala ya kusema kwamba lazima twende driving school au twende huku na wanakufa bila kuwa na hii driving license. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwamba, kila sheria duniani ina exception. Sasa hatuwezi kuacha watu wanaendesha pikipiki na bajaji, wanakufa kwenye ajali hawawezi kupata insurance, hata ile ya third party kwa sababu hana leseni. Hiyo leseni ni chanzo cha mapato, halafu sisi hatuoni kwamba hilo ni tatizo. Kwa hiyo, naomba sana tuliangalie kama jambo ambalo tunaweza kulifanya kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mabadiliko ya sheria ambayo yanapigiwa kelele. Nafikiri ni vizuri na sisi tusimame na tuliangalie hili kwa upana. Kwa nini kikundi cha watu kinaweza kikasema hili ni tatizo wakati wanajamii wenyewe hawajaona kwamba ni tatizo? Wewe unasimama unasema bwana, sisi tunataka Katiba mpya. Kabla hujaipata hiyo Katiba mpya unasema tunataka reform za election; kabla hujaipata unaleta kitu kingine. Basis yao ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tuwe na sheria ambazo ili mtu alete hoja, aibebe kama hoja ya Kitaifa, lazima iwe imesimamiwa na idadi ya watu kwenye kila kata, kwenye kila wilaya na kila mkoa, na wakishafika idadi fulani ndiyo inakuwa National Agenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anabeba ajenda yake anasema bwana sisi tatizo letu sasa ni Katiba mpya. Sisi tatizo letu sasa hivi sijui ni sheria za uchaguzi. Ni nani anamtuma? Ili iwe National Agenda iweze kupigiwa kelele ni lazima kuwe na idadi ya watu katika kila kata, mtaa na wilaya, wanao-demand. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kuwa tuna watu ambao kwa sababu kuna social media watakuja waseme sasa hivi tatizo ni hili. Watarudi kesho waseme tatizo ni hili, halafu walete ajenda ambazo zinaichanganya nchi yetu. Kwa hiyo, naomba sana tutafute namna ya kuweka sheria ambayo italazimisha kuwe na idadi ya watu ambao watasema hiki kitu ndiyo kiwe ni National Agenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uhalifu wa mitandao. Sina uhakika kama sheria zetu zina uwezo kiasi gani kupambana na uhalifu wa mitandao? Tuunde timu chini ya watu ambao watajaribu kufanya tathmini ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tarimo, ni kengele ya pili.
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)