Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Jonas William Mbunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kufanya maboresho makubwa kwenye Wizara hii ya Nishati upande wa Mahakama, kwenye miundombinu na kwenye shughuli zote za utendaji kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria kwa kufanya kazi nzuri ya kuleta taarifa katika Bunge hili Tukufu, na pia kwa kufanya kazi nzuri sana ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake kwenye upande wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ninachukua nafasi hii kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Jumanne Sagini, Naibu Waziri. Pia nampongeza Eliakim Chacha Maswi, Katibu Mkuu, Dkt. Franklin Rwezimula, Naibu Katibu Mkuu, na bila kumsahau Profesa Elisante Ole-Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, pamoja na wafanyakazi wote. Nawapongeza sana kwa sababu utendaji wa kazi wa Mahakama zetu sasa hivi ni tofauti kabisa na ile miaka ya nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka ya nyuma kulikuwa na malalamiko makubwa sana ya upatikanaji wa haki kwa wananchi, lakini sasa hivi mambo yanakwenda vizuri. Kwa hiyo, lazima nichukue nafasi hii kuwapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza naipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha nyingi zaidi, sijapata figure kamili na sahihi, lakini ninajua ni fedha nyingi ambazo zimetumika kujenga jengo la Mahakama Kuu ambalo ni jengo la kisasa na limeweka mpaka akiba ya Supreme Court ambayo haipo kwenye Katiba yetu. Kwa hiyo, tunajua kama kutakuwa na mabadiliko, tayari nafasi hiyo itakuwa accommodated kwenye jengo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naipongeza Wizara hii pamoja na Mheshimiwa Rais, kwa kutoa fedha kuanza kujenga Mahakama Jumuishi katika mikoa yetu. Kwa nafasi hii, naipongeza sana Wizara kwa sababu tayari kuna fedha nyingine zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama hiyo katika Mkoa wa Ruvuma na shughuli zimeanza kuendelea pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, niendelee kupongeza kwenye upande wa miundombinu, Serikali imetoa fedha nyingi kuendelea kujenga Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo. Ni Mahakama za kisasa na ni nzuri ambazo zinajengwa sasa hivi, pia katika kuendelea kuboresha mifumo ya utoaji haki kwenye upande wa Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali, imeweka miundombinu ya kisasa ya TEHAMA, na kama alivyoongea Mheshimiwa Kandege kwa sababu nami nipo kwenye Kamati ya Bajeti, kwa taarifa iliyopo sasa hivi, Majaji wanapotoa hukumu wakimaliza neno la mwisho na hukumu inatolewa. Kwa hiyo, ni mfumo mzuri na utasaidia sana katika utoaji haki kwa haraka kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuunda Tume ya kutayarisha Sera ya Haki Jinai na mikakati ya namna ya kutekeleza sera hiyo. Haya yote ni katika maboresho ambayo yamefanyika ili kuhakikisha kwamba haki inatolewa na wananchi wetu wanapata haki katika mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa utoaji haki Mheshimiwa Rais alianzisha msaada wa kisheria wa Mama Samia Legal Aid. Hiyo imesaidia sana kwa wananchi wetu kwa sababu watu wengi hasa wale wanaoishi vijiji hawajui sheria, hawajui namna gani ya kuendesha kesi. Kwa hiyo, hii inawasaidia sana wale ambao hawana uwezo wa kulipa gharama za kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka, Serikali hii imetoa fedha nyingi kuhakikisha kwamba inatoa mafunzo ya Kikatiba kwenye Halmashauri zetu. Sasa hivi kulingana na taarifa ya Mheshimiwa Waziri takribani Halmashauri 50 …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jonas, kengele ya pili hiyo.

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, takribani Halmashauri 50 tayari zimepata elimu kwa ajili ya huduma za kisheria.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jonas, ni kengele ya pili.

MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)