Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Wizara ya Katiba na Sheria. Kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Wabunge wenzangu na Watanzania kwa ujumla, nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa inayofanyika nchini kwa sekta mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee, kwa jinsi ambavyo sekta ya Mahakama imepata maboresho makubwa kama ambavyo huko nyuma tulivyotoka na hivi sasa kuna mambo mengi sana yamefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kwa namna ya pekee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro na Naibu Waziri pamoja na timu nzima ya Mahakama kwa kazi kubwa inayofanyika nchini, pia kwa jinsi ambavyo utendaji wa Mahakama umeimarika na sekta hii imetoa matumaini makubwa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee, pia kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbulu na Wilaya ya Mbulu kwa ujumla, naishukuru Serikali kwa ujenzi wa Mahakama hasa Waziri Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, nimekwenda ofisini kwake mara kadhaa na hata ndani ya Bunge hili, na katika hoja mbalimbali za kudai ujenzi wa Mahakama mpya katika Wilaya ya Mbulu na hata alipoona ile picha ya Mahakama, alisema, “wala hatutakwenda Mbulu, wacha tutafute fedha tukajenge.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo imeanza, sasa ina karibu mwaka japo inasuasua, ni kazi nzuri kwa sababu Mahakama ilikuwa barabarani na ilikuwa haina hata sehemu ya kutosha kwa wasikilizaji kwenda Mahakamani na kusikiliza kesi za wenza wao na jinsi ambavyo zinaendeshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba walau fedha zipatikane kwa ajili ya kuleta msukumo zaidi kwenye ujenzi wa ile Mahakama, na kama Mheshimiwa Waziri alivyoahidi hivi karibuni, alisema tutakwenda Mbulu kutembelea hiyo Mahakama, lakini nadhani kama hatutapata fedha, hata tukienda Mbulu haitasaidia. Zile fedha zitolewe, mkandarasi yule aendelee kujenga ile Mahakama, kazi ilishaanza, inaendelea vizuri, hapa katikati kidogo imesimama kwa muda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kupongeza Samia Legal Aid Campaign, hii imetoa chachu kubwa kwa Watanzania kama Wabunge wenzangu walivyozungumza, lakini pia imetoa taswira ya kiu kubwa na ushauri wangu kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sibishani na Wabunge wenzangu, naomba kama itawezekana pengine ipate mzunguko wa mara mbili kwa mwaka katika nusu mwaka walau na nusu nyingine ili iweze kufika kwa wananchi zaidi, lakini pia kuona yale yaliyofikiwa kama yanatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli imekuwa kiu kubwa, kwani walipokuja Mbulu Mjini, hasa tulipozindua pale Manyara na baadaye ilipokuja Mbulu Mjini na Wilaya nzima ya Mbulu ilifanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali iangalie muundo wa mashtaka ama wa malalamiko yaliyo kwenye ule muundo yachujwe badala ya kwamba, wakija wale Maafisa kutoa ile huduma ya kuwasikiliza, basi walau kuwe na mchujo wa hoja zinazoenda pale kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi. Kwa sababu nyingine zilikuwa zinaenda wala hazikuhitaji zile level ama kwa zile ngazi ambazo wamekwenda wale wananchi na ikawa ni kama vile muda hautoshi na idadi ya watu ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee, naomba pia Serikali itoe fedha. Nilipozungumza na Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama, ni kwamba kidogo ilikuwa inasuasua kwa sababu ya upatikanaji wa fedha, na bajeti ya ujenzi kama tulivyosomewa na Waziri ilikuwa ni kiasi kidogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ijitahidi ili hii miradi ambayo tulitarajia ikamilike kwa mwaka ule wa fedha uliotengwa, basi ikamilike kwa wakati na Wizara ipate fedha za miradi na fedha za uendeshaji, kwa sababu kadri ambavyo fedha za miradi zinakwama, ndivyo inaenda kufumua bajeti ya mwaka mwingine unaokuja; na kwa sababu hiyo, bajeti zetu zinaakisi mafanikio kidogo kwa ajili ya zile fedha za mwaka wa kwanza zinakuja kuvuruga bajeti ya mwaka unakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Serikali ni kwamba tujitahidi kuona namna ya kupata fedha hizi na namna ya utekelezaji wake na usimamizi ulio mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mbulu ni Wilaya kongwe iliyoanzishwa na wakoloni. Kuna Tarafa zilikuwa na Mahakama za Mwanzo, sasa hivi kumebaki magofu, lakini pia huduma wananchi wanafuata pale Mjini na kwenye Tarafa kama za Haydom, Dongobesh na Tarafa ya Nambis ambayo ilikuwa na Mahakama mbili za wakoloni, ambazo hadi sasa ni magofu takribani miaka mingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kama inawezakana badala ya kujenga ngazi za kata, hebu Serikali itazame muundo wetu utoke kwenye ngazi ya mikoa, baadaye ngazi za wilaya, baadaye ngazi ya Mahakama za Mwanzo kwenye tarafa zetu nchini na hatimaye tunakwenda kwenye kata za kimkakati kulingana na jiografia ilivyo ili wananchi waweze kuhudumiwa katika huduma hii ya kupata haki za kisheria kwa karibu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakumbuka tulipitisha utaratibu wa kuwa na wasaidizi wa kisheria na wakaajiriwa nadhani kwa sehemu kidogo kutokana na uwezo wa Serikali. Nilikuwa nashauri kwamba wasaidizi wale wa kisheria wangeajiriwa kwenye ngazi za Halmashauri ili kusaidia kesi nyingi zinazotokea baina ya wananchi kwenye vijiji vyao, kwa kata zao, kwa mali zao pamoja na watu binafsi kusaidia maeneo hayo ambayo yatasaidia kwenye maeneo ya wananchi, lakini kwenye maeneo ya wale watu ambao...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Issaay, ni kengele ya pili. Ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)