Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia. Naomba nikupongeze kwa kazi nzuri unazozifanya. Umefanya kazi nzuri sana, na ninawaomba wananchi wa Ilala wakurudishe tena, kwani tunakupenda sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nampongeza Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia, amefanya kazi nzuri sana, na ninaendelea kusisitiza kuwaomba wananchi wa Mbeya waturudishie Mheshimiwa Dkt. Tulia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Naibu, wamefanya kazi nzuri sana. Nampongeza Mheshimiwa Rais, kwa jengo zuri kubwa la Mahakama Kuu hapa Dodoma, ni jengo zuri sana la kwanza katika East Africa na Afrika ya Kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha kampeni ya msaada wa kisheria kwa wananchi. Kampeni hiyo imesaidia sana wananchi wetu hasa akina mama, walikuwa wanadhulumiwa ardhi, haki zao walikuwa hawajui wakimbilie wakazipate wapi? Mambo ya mirathi, sasa hivi wananchi, hasa akina mama wanajua sehemu ya kwenda kupata haki. Kwa hiyo, kampeni hizi zimesaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, lakini kampeni hizi zinakomea Wilayani, kwa hiyo, naiomba Serikali kampeni hizi za msaada wa sheria zishuke kwenye kata. Pia naiomba Serikali kampeni hizi ziwe ni endelevu kwa vile zimesaidia wananchi sana, na wananchi wengi wanakimbilia kupata msaada. Hongera sana Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kusogeza Mahakama karibu na wananchi, imepunguza usumbufu. Wananchi wengi walikuwa wanapata taabu kwenda sehemu ‘A’ kwenda kupata haki zao. Naipongeza sana Serikali kwa Mkoa wetu wa Simiyu kwa kujengewa Mahakama katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu nne. Kwa mfano, Wilaya ya Busega imejengwa Mahakama nzuri sana ya kisasa, Wilaya ya Bariadi imejengwa Mahakama nzuri sana ya kisasa, Wilaya ya Maswa imejengwa Mahakama nzuri sana ya kisasa na Wilaya ya Itilima imejengwa Mahakama nzuri ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninalo ombi kwa Wilaya ya Meatu. Mahakama ya Wilaya ya Meatu, majengo yamechakaa sana. Naomba Wilaya ya Meatu tujengewe Mahakama mpya. Maendeleo yana wivu, Wilaya ya Meatu wakiona Wilaya zote kwa Mkoa wa Simiyu; tuna Wilaya tano ambazo tumejengewa Mahakama mpya, wananchi wa Meatu wanakuwa na wivu kwa sababu majengo yao yamechakaa sana. Kwa hiyo, tunaomba kujengewa Mahakama mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Mahakama kwa kuweka mifumo ya kisasa ya uendeshaji wa Mahakama na kusaidia sana utoaji wa haki kwa wananchi. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana alizozifanya kwa miaka minne. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi nzuri sana, lazima apewe maua yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kura atakazozipata haijawahi kutokea, kwa vile amefanya kazi nzuri sana. Nampongeza sana, na Mwenyezi Mungu ambariki Rais wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama yetu atembee kifua mbele, sisi watoto wake tupo, atashinda kwa kishindo. Tutatafuta kura kona kwa kona, uvungu kwa uvungu, kitanda kwa kitanda lazima kieleweke kwa Mheshimiwa Rais. Mtu mzima hatishiwi nyau, Mheshimiwa Rais hatatishwa na kitu chochote, ushindi lazima tushinde, lazima tuongoze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu gani kinachowafanya wapige kelele na kumtukana Mheshimiwa Rais? Hatutakubali, hatupo tayari kusikiliza matusi wanayomtukana na tukayavumilia. Lazima tutawajibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yangu ya kuchangia ni hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)