Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi kuwa mchangiaji wa mwisho wa upande wa Wabunge jioni ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, Naibu Waziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Ndugu Maswi kwa kazi nzuri wanayoifanya pamoja na watendaji wote pamoja na Prof. Elisante Ole Gabriel kwa kazi nzuri aliyofanya katika Mhimili wa Mahakama, lakini pia pamoja na Mhimili wote, Jaji Mkuu, kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kuchangia bajeti hii, kwani kwa miaka mitano ya Bunge sijawahi kuichangia bajeti hii, lakini safari hii nimewiwa kuchangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha Mhimili wa Mahakama unafanya kazi yake nzuri ya kuwa mamlaka ya mwisho ya utoaji haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Serikali ya Awamu ya Sita Kamati yetu ya Bajeti imeshuhudia Mfuko wa Mahakama ukitendewa haki na kupatiwa bajeti ya kutosha ambayo imeimarisha miundombinu ya Mahakama ikiwemo jengo la pekee ambalo limepatikana awamu hii baada ya miaka 104 pamoja na maboresho ya Mahakama mbalimbali katika mikoa na wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa ujenzi wa Mahakama za Mwanzo zinazoendelea Mkoa wetu wa Pwani ikiwemo Mahakama ya Msata ambayo ipo Wilaya ya Bagamoyo, Mahakama ya Kimanzichana ambayo ipo Wilaya ya Mkuranga na Mahakama ya Bungu ambayo iko Wilaya ya Kibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu Serikali iendelee kutenga fedha kwa sababu mahitaji ya ukarabati wa Mahakama za Mwanzo ni mkubwa, ikiwemo Mahakama zilizochakaa. Kwa mfano, Mahakama ya Kiwanga ipo Chalinze, Mahakama ya Mwambao, tuna Mahakama pia kule Miono, zote zinahitaji ukarabati mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nimesimama kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Pwani kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna programu hii ya Mama Samia Legal Aid ilivyofanya vizuri, ilifika Mkoa wetu wa Pwani na wanawake wengi walijitokeza, lakini kipekee kwa namna ambavyo kampeni hii imefikia zaidi ya wananchi 2,600,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii pia imenzisha madawati katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 ambayo wananchi zaidi ya 6,000,000 wamefikiwa na huduma mbalimbali za kisheria, na tumeona migogoro ya ardhi ikitatuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita UWT tulikuwa na semina, nimshukuru Waziri Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, pamoja na Katibu Mkuu Ndugu Maswi kwa namna walivyotupitisha kwenye mafanikio makubwa, pia kwa namna ya kipekee wanavyoshirikiana na Umoja wa Wanawake wa Tanzania kwa kuwa tumeunda Kamati ya Katiba na Sheria, nasi tunaunga mkono Mama Samia Legal Aid na tumeshafanya utoaji wa msaada wa kisheria katika Mkoa wa Dodoma na Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Naibu Waziri, Mwenyekiti wetu, Wakili Msomi Mheshimiwa Zainab Katimba, kwa kufanya vizuri. Hii UWT ndiyo ambayo kupitia uongozi wa hayati Mama Sofia Kawawa ndiyo ilianzisha Shirika la SUWATA ambalo lilikuwa linatoa huduma za sheria, lakini hili Shirika hata kuhamasisha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, pia ilishiriki katika kuhakikisha Sheria ya Kazi ya mwaka 1975 inaweka kipengele cha likizo ya uzazi kwa makundi yote ya wanawake bila kuzingatia hali ya ndoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachofanyika sasa Umoja wa Wanawake Tanzania chini ya Mama Chatanda ni mwendelezo wa UWT ya Marehemu Mama Sofia Kawawa na Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani. Ndiyo maana tunaona kwa mara ya kwanza Serikali hii inapoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu mwanamke, kwa kuzingatia kwamba wahanga wakubwa wa changamoto za upatikanaji wa sheria ni wanawake ameanzisha hii programu ya Mama Samia Legal Aid, tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waliofikiwa na programu hii zaidi ya 9,000,000 kwa namna moja au nyingine, 2,600,000 wale wa madawati ya kisheria kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa zinamshukuru, na ni miongoni mwa watu ambao watampigia kura za kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, naipongeza Serikali kwa kuendelea kulinda Katiba yetu, kuendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025. Sisi tunasema tayari maboresho yamefanyika ya kuwezesha mazingira ya kufanyika kwa uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria tatu tulizopitisha hapa Bungeni ambapo watu wengi walishiriki ikiwemo taasisi zetu za kidini, ikiwemo wadau mbalimbali wa siasa, wameshiriki kuanzia kutoa maoni wakati wa kikosi kazi pia walikuja hapa Bungeni wakati wa kusikiliza maoni yao kwenye Kamati. Kwa hiyo, tunaamini mazingira haya yaliyotengenezwa, yatauwezesha uchaguzi kufanyika kuwa huru na wa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwapongeza Serikali na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa maboresho haya, na niwatakie heri Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa maandalizi yanayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja hii na kuwapongeza wote. Ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)