Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naomba kuungana na Watanzania wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza vyema miaka minne kwa kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. Pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri iliyotukuka ya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa Mgombea Mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa uzoefu na weledi wake, kama ilivyo kwa Watanzania walio wengi, nina imani kubwa kwa Mheshimiwa Nchimbi na kumtakia afya njema na kila la heri kwenye mchakato ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Doto Mashaka Biteko, Mbunge, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kutekeleza majukumu ya kumsaidia Waziri Mkuu, ikiwa na pamoja na jukumu la kuendelea kuisimamia ipasavyo sekta ya nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi na Spika na pia uongozi wote wa Bunge kwa uongozi mahiri na wenye ubunifu wa hali ya juu katika kuongoza mhimili wa Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Mbunge na Waziri wa Katiba na Sheria kwa hotuba nzuri iliyojaa ubunifu mkubwa na imedhihirisha utayari wa Taifa letu katika ya ushindani wa Kimataifa (National competitiveness). Bajeti hii ambayo ni ya mwisho, inaenda sambamba na Dhima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026 ambayo ni Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi chake akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, tathmini zinathibitisha mafanikio makubwa ya utekelezaji na usimamizi wa Mpango wa Kwanza na wa Pili na kupelekea Taifa letu la Tanzania kufanya vizuri mno katika mazingira ya kuboresha huduma ya kutoa haki kwa wananchi, na Tanzania inaongoza katika nyanja nyingi ukilinganisha na nchi nyingi duniani na hata Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Ofisi ya Mahakama imefanikiwa katika kuboresha mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ikiwemo mfumo wa usimamizi wa mashauri na kupelekea kuongeza tija katika utatuzi wa mashauri, yakiwemo yaliyodumu kwa kipindi kirefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Mahakama imeendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya mahakama katika ngazi mbalimbali nchini ikiwemo jengo la Makao Makuu Dodoma ambalo ni la kwanza Afrika na la sita duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza Serikali iweke mkakati wa kuboresha ufanisi kwa taasisi zote zinazofanya kazi na Mahakama, zikiwemo Polisi, Mwendesha Mashtaka na hata Mawakili ili utoaji wa huduma uendane na ufanisi uliojengeka na Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yake, Ofisi ya Mahakama inaendelea kukabiliwa na upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali na uchakavu wa majengo ya Mahakama za ngazi zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoshauriwa kwenye taarifa ya Kamati ya Bajeti, kuna haja kwa Ofisi ya Mahakama kuongeza watumishi katika Mahakama zote nchini ili kuongeza tija na ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napendekeza Serikali kuhakikisha inatenga fedha za kutosha za maendeleo ili kuendeleza ujenzi na ukarabati Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya, Mahakama Kuu pamoja na nyumba za Majaji ili kuboresha na kusogeza huduma hii muhimu kwa wananchi. Mkazo wa elimu ulenge kujenga uwezo wa masuala ya mikataba ya Kimataifa na hasa negotiations skills za Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Mbeya bado ina changamoto za uhaba wa Mahakama za Mwanzo na inapelekea wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma ya Mahakama ya Mwanzo. Mji Mdogo wa Mbalizi wenye idadi ya watu zaidi ya 100,000 ina Mahakama ya Mwanzo ambayo ni ndogo sana na chakavu ambayo ni hatarishi kwa usalama na afya ya watumishi na hata wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa Serikali kuanza ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo katika eneo la Utengule Usongwe ambalo limetolewa na wananchi. Pia, naomba kuwepo na kipaumbele cha ujenzi wa Mahakama za Mwanzo angalau mbili kwa kila Tarafa za Usongwe, Isangati na Tembela.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.