Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nampongeza sana Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro, Mbunge na Naibu wake Mheshimiwa Jumanne Abdallah Sagini, Mbunge na wataalamu wa Wizara na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hii kwa kazi nzuri wanazofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utahusu umuhimu wa msaada wa huduma za kisheria kwa wananchi kupitia kwenye kampeni ya Mama Samia Legal Aid.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inaendeshwa kwa kuzingatia utawala wa sheria na misingi ya haki za binadamu. Vyombo vya sheria nchini vina jukumu la kusimamia utoaji haki, hifadhi ya Katiba, kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na taasisi zake, kusimamia hifadhi za haki za binadamu na kuhakikisha sheria na taratibu za nchi zinafuatwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mhimili mkubwa wa utawala wa sheria ni Mahakama. Kazi kubwa ya Mahakama ni kuhakikisha usawa mbele ya sheria kwa watu wote. Katika kutoa haki, Mahakama hutumia mfumo wa wataalamu mbalimbali ambao hutafsiri sheria na kufikia mwafaka wa kutoa haki. Wataalamu hao ni pamoja na Waendesha Mashtaka, Mawakili/Wanasheria na Mahakimu au Majaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakili ni mtaalamu wa sheria anayepewa leseni ya kutoa ushauri wa kisheria na kuwakilisha wateja katika masuala mbalimbali ya kisheria. Wakili anaweza kuwa mtu ambaye amehitimu katika taaluma ya sheria, amefuzu mafunzo ya sheria na kisha kupokea leseni ya kufanya kazi ya uwakili. Kwa upande mwingine, mwanasheria ni mtu yeyote aliyesoma kozi ya sheria katika chuo kinachotambulika na kuhitimu na kufaulu na kupata Shahada ya Sheria (LLB).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi yetu, Mawakili na Wanasheria huchukua jukumu kuu katika mfumo wa sheria kwa kuwa na uwezo wa kufafanua sheria, kutoa ushauri wa kisheria. Mawakili huwakilisha wateja Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mawakili wa Serikali ni watumishi wa Serikali na jukumu lao kubwa ni kutetea maslahi ya Serikali. Vilevile Wakili wa Serikali humsaidia mwananchi yeyote ambaye ana kesi kubwa kama ya mauaji au uhaini ambazo hukumu zake ni kifo. Kwenye hizi kesi kubwa, Serikali inamwekea mshtakiwa wakili wa kumtetea na analipwa na Serikali yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawakili binafsi, wamejiajiri na huduma wanayotoa hulipiwa na mteja. Kwa mantiki hii, wananchi wengi binafsi wanaohitaji huduma za kisheria wanapata huduma kutoka kwa mawakili binafsi kwa malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mawakili binafsi wanalipwa, wananchi wanaohitaji huduma ya kisheria na wasioweza kumudu gharama za mawakili huishia kukosa huduma za kisheria. Kwa sasa hapa Tanzania, mwananchi wa kawaida akiwa na kesi inayohitaji wakili, huwa gharama za wakili ni kubwa sana na wengi hawazimudu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa kuwa Wakili au Mwanasheria wa Serikali hawajibiki kusaidia wananchi mwenye tatizo binafsi la kisheria, basi kimbilio la wananchi lina mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, liwe liwalo, kupata wakili au mwanasheria ni hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa haki za wananchi wasio na uwezo, zinalindwa na masuala ya kisheria yanashughulikiwa ipasavyo. Ni kwa mantiki hiyo nawiwa kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuanzisha programu ya kutoa msaada wa huduma za kisheria kwa wananchi bure kupitia Kampeni ya Mama Samia Legal Aid. Katika miaka ya awali, kampeni hii itafanyika kwa miaka mitatu ambapo itahitimishwa mwezi Februari, 2026 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar. Kampeni hii ni kielelezo kwamba Rais Samia anataka kumfikia kila Mtanzania anayehitaji huduma za kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, programu hii imekuwa ni ukombozi mkubwa, kwani huduma za kusaidiwa kisheria zimewafikia wananchi wasio na uwezo wa kulipia gharama za uwakili ili kupata huduma za kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni utekelezaji wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanasaidiwa katika matatizo yote ya kisheria bila malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, zoezi la kutoa msaada wa kisheria katika mikoa tofauti limefanyika kwa mafanikio, kwani maelfu ya wananchi wameshafikiwa na huduma, wanaume na wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Waziri, tumeambiwa kwamba tangu kuzinduliwa kwa kampeni hii, tarehe 27 Aprili, 2023, jumla ya mikoa 25 imefikiwa na Kampeni (Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Simiyu, Singida, Iringa, Mara, Songwe, Morogoro, Njombe, Katavi, Tabora, Geita, Kigoma, Mtwara, Kilimanjaro, Mwanza, Mbeya, Lindi, Rukwa, Pwani, Arusha, Tanga na Kagera) na upande wa Tanzania Bara Mkoa uliobaki ni Dar es Salaam ambapo kampeni itatekelezwa ifikapo Juni, 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri ametueleza kwamba katika utekelezaji wa kampeni hiyo, wananchi wamepatiwa huduma mbalimbali ikiwemo elimu kuhusu masuala ya haki na wajibu; umiliki na utatuzi wa migogoro ya ardhi; matunzo ya watoto; utatuzi wa migogoro ya ajira na mahusiano kazini; ukatili wa kijinsia; wosia, mirathi, ndoa na familia; usajili wa matukio muhimu ya binadamu; na haki za binadamu. Aidha, kupitia mada zinazotolewa, wananchi wamepata fursa ya kuuliza maswali kuhusu masuala ya kisheria na kupatiwa majibu papo kwa hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumejulishwa kwamba kupitia kampeni hiyo, jumla ya halmashauri 180, kata 1,907 na vijiji/mitaa 5,702 zilifikiwa na jumla ya wananchi 2,698,908; wanaume 1,347,325 na wanawake 1,351,583 walifikiwa na kupata elimu ya huduma za kisheria kupitia mikutano ya ana kwa ana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeambiwa kwamba kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, jumla ya migogoro 24,691 iliyodumu kwa muda mrefu ilipokelewa ambapo baadhi ilidumu kwa zaidi ya miaka kumi. Utatuzi wa migogoro hiyo umewezesha kuimarisha amani, utulivu na utengamano miongoni mwa wanajamii, kwani umeacha pande zilizokuwa na migogoro zimeelewana.

Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro iliyoshughulikiwa ilihusisha masuala ya ardhi, ndoa za utotoni, matunzo ya watoto, madai, ndoa, jinai, ukatili wa kijinsia, ardhi, ajira na mengineyo. Aidha, jumla ya migogoro 5,704 ilitatuliwa na kuhitimishwa kwa njia mbadala kati ya migogoro 23,399 ya muda mrefu iliyopokelewa. Utatuzi wa migogoro 18,987 unaendelea katika ngazi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru sana Serikali, kwani kampeni ya Mama Samia Legal Aid imejikita katika kutoa elimu ya kisheria kwa wananchi hasa katika masuala ya ukatili wa kijinsia, migogoro ya ardhi, mirathi na usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala na masuala yanayohusiana na haki za binadamu kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kuu la kampeni hiyo inayotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria ni kulinda na kukuza upatikanaji wa haki kwa wote kupitia huduma ya msaada wa kisheria nchini huku ikitarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wote, bila kujali hali zao za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufanikisha programu hii, utekelezaji wa kampeni umefanyika kwa kushirikiana na Wizara na Taasisi za Serikali, Asasi za Kiraia, Wanazuoni na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, matokeo ya muda mrefu wa kampeni hii ni kuchangia katika kuboresha upatikanaji wa haki kwa watu wasiojiweza, hususan wanawake, watoto na watu maskini walio katika mazingira magumu. Vilevile itachangia kuimarisha amani na utulivu hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, inategemewa kwamba jambo hili jema litaimarisha mfumo wa utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika ngazi za Serikali Kuu hadi Serikali za Mitaa na hatimaye itapunguza idadi ya migogoro na matukio yanayotokana na ukosefu wa uelewa wa sheria na kuimarisha uwajibikaji na uwezo wa taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali kwenye kutoa huduma za msaada wa kisheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maoni yangu, kampeni ya Mama Samia Legal Aid ni fursa pekee iliyotolewa kuwakomboa wanyonge wanaopitia dhuluma mbalimbali kwa kutoelewa sheria hapa nchini. Kwa kiwango kikubwa hili jambo linafanikishwa kupitia kwa wasomi wetu ambao ni Wanasheria na Mawakili wa Serikali na wale waliojiunga kwenye hili jambo jema na la heri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampeni hizi zitatoa msaada wa kisheria kwa raia wa Tanzania wa kipato cha chini. Huduma hizi zitachangia kwenye kurudisha haki na utulivu kwa raia na familia maskini hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kazi iliyofanyika, nichukue nafasi hii kuwapongeza watekelezaji wa Programu ya Mama Samia Legal Aid. Mpaka sasa wamefanikiwa kutatua matatizo mengi kwenye maeneo waliyopita. Pia wameandaa ushahidi na kukabidhi kwa mamlaka zinazohusika katika kutoa haki ili waathirika waweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kampeni hizi zisiishie mwezi Februari, 2026 bali ziwe ni kitu cha kudumu na endelevu. Kwa kufanya hivyo, Rais Samia atakuwa ameacha alama kubwa katika kipindi cha utawala wake, kwani programu hii imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kwa kutatua migogoro mbalimbali ya kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia kampeni hizo, Watanzania wamepata nafasi ya kusikilizwa na Mawakili waliobobea huku migogoro mingi ikipatiwa ufumbuzi wa papo hapo, na mingine ikipelekwa kwenye vyombo vya kutoa haki. Hivyo basi, inatakiwa kampeni hii iwe endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo yangu hapo juu, naunga mkono hoja.