Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nianze kutumia fursa hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuwa na afya njema iliyotuwezesha kukutana mchana huu kujadili hoja ya Mheshimiwa Waziri Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu na kunifanya niendelea kuwa msaidizi wake katika nafasi ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, ninashukuru taasisi zilizo chini ya Wizara na Mhimili wa Mahakama kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, na pia kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia, Mheshimiwa Waziri pamoja na mimi kama Naibu Waziri. Nawashukuru viongozi wengine wa Kitaifa, akiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa miongozo yao inayotuwezesha kutimiza majukumu yetu kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Wabunge, kama alivyozungumza Waziri wangu katika kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi nzuri anayoifanya, kuliongoza Bunge lako Tukufu. Aidha, nikupongeze wewe binafsi kwa mwongozo wako mzuri katika kumsaidia Spika kutekeleza majukumu yake. Nami niungane na waliosema kuwaomba wananchi wa Majimbo haya mawili ya Mbeya Mjini pamoja na Ilala kuhakikisha wanawapa kura nyingi za kishindo na mweze kurejea na kuendelea kuliongoza Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyowashukuru Waziri wa Katiba na Sheria alipokuwa akiwasilisha bajeti yake, napenda kutumia fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati, Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Florent Kyombo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya uongozi wa Mheshimiwa Oran Manase Njeza, kwa ushauri na miongozo yao iliyoiwezesha Sekta ya Katiba na Sheria kutimiza majukumu yao vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Katiba na Sheria, kwa namna anavyotuongoza sisi wasaidizi wake na management ya watumishi wengine wa Wizara katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Katiba na Sheria na taasisi zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nawashukuru Management ya Wizara, Taasisi za Wizara pamoja na Mhimili wa Mahakama kwa kutupatia ushirikiano mkubwa, kutuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uridhie niwashukuru wananchi na wapigakura wa Jimbo la Butiama kwa ushirikiano wanaonipa mimi Mbunge wao, hasa ninapotekeleza majukumu mengine ya Kitaifa, hususan kwa nafasi ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria. Pia nawashukuru viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya wilaya na mkoa kwa uongozi wao ulioniwezesha kutimiza wajibu wangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee, naishukuru familia yangu, hususan mke wangu kipenzi Bi. Mariam Sagini, watoto wangu ambao leo wamewakilishwa na Bi. Leila, Mama yangu Mzazi Zena Sagini kwa ushirikiano na dua wanazoniombea ninapotekeleza majukumu ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Ubunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba nitumie fursa hii kutoa maelezo kwa baadhi ya hoja za Waheshimiwa Wabunge, hususan kwenye sekta ya Mhimili wa Mahakama. Kwanza, niwashukuru Wabunge wote kwa pongezi kubwa walizozitoa kwa Mhimili wa Mahakama kwa mageuzi makubwa na uboreshaji wa miundombinu inayosaidia kutoa haki kwa wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, tunakiri, ni kweli, jengo lile lililojengwa ni kubwa, la kisasa na hakuna mfano wake Afrika na tumeambiwa ni jengo namba sita. Pongezi kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Jaji Mkuu na Mhimili wote wa Mahakama kwa ubunifu na kuja na jengo lililo bora sana. Nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa fedha zilizowezesha ujenzi huo kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, yameelezwa mambo mbalimbali hapa, hususan upungufu wa watumishi katika Sekta ya Mahakama. Ni kweli kwamba, upungufu huo upo, lakini tunaishukuru Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa vibali vya ajira kila mwaka, ili kuipunguzia Sekta ya Sheria upungufu wa wafanyakazi. Kwa mfano, mwaka uliopita, 2024 Mahakama ilipewa kibali cha kuajiri watumishi 522 na mwaka huu wameruhusiwa kuajiri watumishi 1,044. Kwa mwelekeo huo, tutaendelea kutatua tatizo la upungufu wa watumishi wa Sekta ya Mahakama hadi pale tutakapolimaliza kabisa, hususan kutegemea bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, limezungumzwa suala la uchakavu wa miundombinu ya Mahakama, hususan Mahakama za Mwanzo na baadhi ya Mahakama za Wilaya kwamba, zilijengwa wakati wa kipindi cha mkoloni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua changamoto hii. Ni kwa msingi huo Mahakama iliweza kuandaa mpango wa maboresho ya Sekta ya Mahakama ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ya Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani, Mahakama za Hakimu Mkazi Ngazi ya Mkoa, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, imeshauriwa hapo kwamba, kwa kuwa, kata zetu ni nyingi na tunazo tarafa ambazo zinakadiriwa kufikia karibu 1,000 ni muhimu tungewekeza kwenye ujenzi wa Mahakama ngazi ya tarafa badala ya kwenda kwenye kata ambazo hatujafika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Wizara, tunachukua ushauri huo kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba, tarafa zetu zote zinafikiwa na Mhakama, halafu baada ya hapo ndiyo twende kwenye ngazi ya kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme mpango tunaoendeleanao sasa hivi, ni kuimarisha Mahakama ngazi ya Mahakama Kuu, Mahakama Jumuishi Ngazi ya Mkoa, na tunakwenda kwenye Mahakama za Wilaya na tunaendelea na hizi Mahakama 72 tulizoanzanazo katika awamu hii tunayoendelea nayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama itaendelea kutekeleza mpango wake wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, kama ilivyoombwa na Wabunge wa majimbo mbalimbali. Tunafahamu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mbeya ameongea juu ya Mahakama ya Ileje. Nimhakikishie Mbunge kwamba, mpango wa kuijenga Mahakama ya Wilaya ya Ileje upo na utendelea kutekelezwa na Mahakama kadiri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumepata maoni ya maandishi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, Mahakama yake ya Wilaya ya Kiteto pia ipo kwenye mpango huo, itatekelezwa sanjari na mpango mwingine wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ombi la kuanzisha Mahakama, Ngazi ya Wilaya ya Mlimba, ni kweli, Mahakama inao mfumo unaozingatia utawala wa Serikali Kuu. Kwa hiyo, kwa vile hakujaanzishwa Wilaya ya Mlimba, inakuwa vigumu sana kwa Mahakama kuanzisha Wilaya katika Jimbo la Mlimba, lakini tunamhakikishia, pale itakapofika Mlimba kuwa na sifa za kuanzisha Wilaya kwa taratibu za TAMISEMI, Mahakama pia itajipanga kupeleka Mahakama ya Wilaya katika ngazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, umetolewa ushauri mwingi kuhusu uimarishaji wa utoaji wa haki kwenye Mahakama zetu, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba, ushauri wote utachukuliwa na kufanyiwa kazi kwa sababu, ni dhamira ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha kwamba wananchi wanapata haki, na ndiyo maana mtaona Mheshimiwa Waziri atazungumzia habari ya utoaji wa msaada wa kisheria wa Mama Samia Legal Aid Campaign. Ni dhamira yake kuona kwamba, Watanzania wanapata haki, hivyo, Mahakama itaendelea kuimarishwa ili kuona haki hiyo inawafikia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo ninaunga mkono hoja, nashukuru sana. (Makofi)