Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Vilevile, nichukue nafasi hii kumpongeza kwa uongozi wake mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nichukue nafasi hii kumpongeza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na kumshukuru Mheshimiwa Jaji Mkuu, Spika wa Bunge, na wewe mwenyewe; Mawaziri, Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na uongozi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia kwa baadhi ya Wabunge ambao walitoa maoni yao. Nianze na Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, ambaye alizungumzia suala la majadiliano ya mikataba kuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwa yakini kabisa, kwa asilimia kubwa ya mikataba, ambayo Taifa hili tunajadili inachukua muda ambao ni muafaka na wa kawaida ndani ya misingi ile ya majadiliano. Ni kweli, ipo mikataba michache ambayo imechukua muda mrefu kama alivyotaja, lakini niseme kwamba, mikataba mikubwa na ya kimkakati kwa kawaida inachukua muda mrefu kwa sababu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ile complexity ya regime ya mambo ambayo mnayajadili; unazungumzia technical issues, business case yenyewe, legal regime, investment regime, tax regime, liability regime, security regime na mambo mengine, including pecuniary issues. Kwa hiyo basi, ni kawaida sana majadiliano ya mikataba mikubwa kama hii kuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mifano ya mikataba ambayo pia imechukua muda mrefu duniani. Kwanza ni Gabčíkovo-Nagymaros Project; huu ni Mradi wa Kujenga Bwawa la Umeme ambapo majadiliano kati ya Hungary na Czechoslovakia yalichukua miaka 20 kwa sababu ya complexity ya maeneo hayo ambayo nimeyataja. Ilikuwa ni kuanzia mwaka 1950 mpaka 1977 walipomaliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, majadiliano kati ya Marekani na Canada juu ya ujenzi wa bwawa la umeme katika Mto Columbia yalichukua miaka 49. Kwa nini? Kwa sababu ya complexity ya issue na kila upande unataka kuvutia kwenye maslahi yake kuangalia maeneo yote yale ambayo nimeyataja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za Ulaya, majadiliano ya matumizi ya River Rhine, kule Ulaya, round ya kwanza yalitumia miaka 17 mpaka walipokuja ku-conclude. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi, ni kawaida, hasa katika miradi mikubwamikubwa kama hii yenye complexities of regime, ambapo kila upande unataka kuhakikisha kwamba, wakimaliza wanatoka na mkataba mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mkataba wa LNG halikadhalika na Mkataba wa Liganga na Mchuchuma ina-involve complexities of regime. Tunataka kuangalia mambo mengi. Tunataka itakapokamilika iwe mikataba ambayo ina maslahi kwa Taifa hili, lakini kwa upande mwingine nao wanataka uwe na maslahi kwao. Ni kawaida sana kwa mikataba hii kuchukua muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao, na hapa nasikitika sana, hasa ninaposikia kauli za baadhi ya wanasheria wengine wakisema kwamba, suala hili ni uvunjwaji wa Katiba na Sheria, inasikitisha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu ni kwamba, tuache kufanya hivyo kwa sababu, sisi katika Sekta ya Sheria tulisema Taifa hili linasonga mbele na ku-support ukuaji wa uchumi. Tuliamua kwa makusudi kama Taifa, tu-embrace technology na sisi katika Sekta ya Sheria tutafanya hivyo, tuta-embrace TEHAMA. Kwa hiyo, ku-embrace TEHAMA, ni jambo la muhimu na ni la msingi kwa maendeleo ya Taifa lolote. Hata katika Sekta ya Sheria, tulisema hatutakaa nyuma katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, katika Sheria ya Usimamizi wa Haki na Matumizi ya Sheria (Judicature and Application of Laws Act, Sura ya 358) ukipitia Kifungu cha Nne tuliamua kwa makusudi kabisa, kama Taifa, kutengeneza kanuni za usikilizwaji wa mashauri kielektroniki nje ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni suala la Kisheria na asitokee mtu akasema kwamba, suala hili siyo la kisheria, huo ni uongo na upotoshaji. Ni suala la kisheria; na kwa nini tulifanya hivyo? Kwa sababu yapo mazingira mbalimbali ambayo, kama Taifa, tuliyabaini na tuliona kwamba, tunapokwenda huko mbele, lazima tuje na utaratibu ambao tunaweza ku-embrace TEHAMA katika utoaji wa haki katika usimamizi wa haki na matumizi ya Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika kanuni zile za mwaka 2021 nilizozisema, Kanuni za Usikilizwaji wa Mashauri Kielektroniki nje ya Mahakama (Judicature and Application of Laws Remote Proceedings and Electronic Recordings), Kifungu cha Nne, nitakisoma na nitajaribu kukitafsiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema kwamba, “The court may on its own motion or an application by a party allow proceedings to be conducted remotely on its own motion.” Maana yake ni kwamba, Mahakama ita-assess mazingira yaliyopo siku hiyo na kuona kwamba, tulisikilizeje shauri hili, hasa kama kuna mazingira katika mitandao na social medias zinarushwa habari za ajabuajabu na nyingine ni za kutisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama jukumu lake siyo tu mashauri, lakini kuhakikisha na huko wananchi wengine waendelee na shughuli zao; shughuli za kiuchumi ziendelee. Siyo shauri linasikilizwa na kila kitu kimefungwa, barabara zimefungwa, haiwezekani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mahakama iki-assess mazingira, inaweza ikaamua na ni kwa mujibu wa sheria na kifungu kile kimeweka utaratibu na methods za namna ya kusikiliza shauri kwa njia ya mtandao nje ya Mahakama na Kifungu cha Tano sasa kinaweka zile procedures.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia kilichotokea tarehe 24, procedures zile zilikuwa properly followed. Sasa huyu mtu anayetokea anasema kwamba, kuna uvunjifu wa sheria. Sheria zipi? Sheria si ndiyo hii!
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ndiyo Sheria na mimi ninayezungumza hapa ndiye Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kwa hiyo, watu waache upotoshaji. Unaweza kuwa na malengo yako, lakini siyo kwa kupotosha na kusema kwamba sheria za nchi zinavunjwa, hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilisema nitumie fursa hii kulizungumzia hili jambo kwamba, suala hili ni kwa mujibu wa Sheria na hata siku nyingine yoyote Mahakama ita-assess tu mazingira na kuona isikilize wazi au isikilize kwa njia ya kimtandao nje ya Mahakama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawasihi sana wananchi na wanasheria wenzangu wanaojaribu kupotosha, waache kufanya hivyo kwa sababu, kufanya hivyo kunasababisha taharuki na kuwafanya wananchi waone kwamba, Serikali yao inaendesha mambo nje ya sheria, jambo ambalo siyo kweli. Mahakama haiwezi ikaamka tu asubuhi ikasema wanasikiliza kwa njia ya mtandao, hapana. Ni kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nichukue nafasi hii kumpongeza mchangiaji, Mheshimiwa Salome Makamba, kwa uchangiaji mzuri na wa kiufundi na amechangia ndani ya sheria. Amechambua vizuri kuanzia Katiba, Sheria na mpaka ilivyoteremka kwenye Kanuni za Maadili. Kwa hiyo, nampongeza sana; Wanasheria wa namna hii tunawapongeza sana wanapokuwa wanachangia vitu ndani ya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, tunakushukuru kwa michango yako. Niseme tu kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali siyo tu kusubiri bajeti, kuna vitu vingi tunaweza kuvifanya kwa mazingira tuliyonayo na tutaendelea kutoa ushauri wa kisheria. Kwa mfano tu, kwa mwaka huu tunaomaliza tumetenga kiasi cha kutosha sana katika mafunzo, lakini kuna mafunzo mengine tunayafanya wenyewe bila kuhitaji fedha na jambo hilo tutaendelea kulifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue nafasi hii tena kumpongeza Waziri wetu kwa uongozi wake mzuri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wote katika Sekta ya Sheria. Namshukuru Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwandishi Mkuu wa Sheria kwa kazi nzuri wanayoifanya na wanavyonisaidia. Naishukuru sana Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria na Wabunge wote ambao tumekuwa tukifanya kazi pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Wabunge wote ambao wamechangia leo kwa michango yao mizuri ambayo inalenga kuboresha sekta ya sheria kwa ujumla. Niwaombe Wabunge watuunge mkono kupitisha bajeti hii ili tuweze kwenda kuyatekeleza yale yote yaliyoelezwa na Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria katika hotuba yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima na taadhima, naunga mkono hoja. (Makofi)