Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuifanya siku ya leo iende vizuri mpaka tunafikia hatua hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu kwa namna ambavyo wanatuongoza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena wewe na Mheshimiwa Spika kwa kuliongoza Bunge letu vizuri kabisa. Tunamwombea Mheshimiwa Spika na tunakuombea Mheshimiwa Naibu Spika mpate mitano tena kule Mbeya na mitano tena pale Ilala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba, na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Mhagama pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, ndugu yangu Mheshimiwa Njeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru wapigakura wa Songea Mjini kwa namna ambavyo wananiunga mkono, na kwa namna ambavyo tunashirikiana nao. Tunaamini kwa umoja wetu 2025 tutafanikiwa kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru familia yangu ikiongozwa na mke wangu kipenzi Bi. Flora pamoja na watoto kwa kuendelea kuniunga mkono wakati natekeleza majukumu ya Kiserikali. Namshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Seriali kwa ushirikiano ambao anatupatia Wizara ya Katiba na Sheria, na kwa maelezo yake mazuri ambayo ameyatoa hivi punde. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu Waziri, Mheshimiwa Jumanne Sagini, Mbunge wa Butiama, naye namwombea kila la heri katika mwaka huu wa 2025. Namshukuru Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote kwa kufanikisha mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge 21, ambapo 19 wametoa michango yao kwa njia ya kuongea na wawili wametoa michango yao kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mhimili wa Mahakama kwa ushirikiano ambao wanatupatia, na leo hapa umewakilishwa vema na Mheshimiwa Profesa Elisante Ole Gabriel pamoja na Mheshimiwa Eva Nkya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Spika, ushauri wote ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa njia ya kuongea na kwa njia ya mdom,o tumeupokea. Tuahidi, Wizara hii ni Wizara sikivu, tutaenda kuufanyia kazi. Tutawapa majibu mengine kwa maandishi, lakini wataona utekelezaji wa mambo hayo kwa kadiri ambavyo siku zinakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu niongee mambo makubwa matatu. Jambo la kwanza ni kuhusu Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign). Kila Mheshimiwa Mbunge aliyesimama na kuchangia kwa maandishi amepongeza kwa dhati kampeni hii na umuhimu wake katika jamii katika kuleta haki, usawa, amani, na maendeleo. Tunazipokea pongezi hizo kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, na tutamfikishia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampeni hii ina misingi yake. Msingi wa kwanza ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan Ibara ya 13(1), ambayo inasema kuwa kila mtu ni sawa mbele ya sheria. Hivyo, kampeni hii inalenga kuwafanya Watanzania wote wanapokuwa mbele ya sheria wawe sawa, na ndicho ambacho tunakitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampeni hii inatokana na Sheria ya Bunge, Sheria Na.1 ya mwaka 2017, Sheria ya Utoaji wa Msaada wa Kisheria, sheria ambayo Bunge hili Tukufu liliitunga ili iwasaidie Watanzania. Utekelezaji wa kampeni hii ni utekelezaji sheria hiyo ya Bunge. Hivyo, Bunge hili nalo linastahili pongezi kwa kutunga sheria ambayo inawasaidia Watanzania hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampeni hii ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi hususan Ibara ya 120(b). Wakati Ilani hii inaandikwa, Mheshimiwa Dkt. Bashiru alikuwa ndiye Katibu Mkuu. Ibara ile ambayo uliiandika kipindi kile ndiyo tunaitekeleza sasa katika kuhakikisha kwamba tunawapa wananchi haki yao stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mpango huu ni maelekezo mahsusi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Januari, 2023 Waziri wa Katiba na Sheria aliniita, akaniambia tunataka tutekeleze ilani, tunataka tutekeleze Katiba, tunataka tutekeleze sheria ili tuwafikie Watanzania wengi waweze kupata haki. Wizara ikatekeleza na leo ndiyo matunda haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeyasema haya kwa sababu ni lazima tujue kwamba kampeni hii ina misingi thabiti kabisa. Kwa misingi hiyo, kampeni hii haiwezi kufa kwa sababu imejikita kwenye misingi ambayo ipo na ni endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara tumeweka mkakati. Mkakati wa kwanza, tayari kuna Maafisa Dawati katika halmashauri zote 184, ambao kazi yao ni kuendeleza utoaji wa msaada wa kisheria kipindi kile cha kampeni cha siku 10 zinapokuwa zimekwisha. Maafisa Dawati hawa wanafanya kazi nzuri kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tumeingia makubaliano na Chama cha Mawakili Tanzania, asasi za kiraia ambazo zinatoa msaada wa kisheria, vyuo vikuu, na wadau wengine mbalimbali ili kuufanya mpango huu kuwa endelevu, na utakuwa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Juni mwaka huu wakati tunafanya kwa Mkoa wa Dar es Salaam, tutafanya mambo makubwa mawili. Moja, ni kuhitimisha round ya kwanza. Round ya pili ni kufungua awamu ya pili ambayo itaanza mara baada ya kuhitimisha Mkoa wa Dar es Salaam, itafanya uendelevu wa mkoa huu. Tutapita tena kila sehemu kuhakikisha kwamba tunatekeleza hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Waheshimiwa Wabunge ya kwamba tuwe na Mfuko wa Msaada wa Kisheria (Lega Aid Fund) tumeipokea, tutakwenda kuichakata kama Serikali, na kwa kuwa tuko kwenye mpango wa kukamilisha Sera ya Msaada wa Kisheria, hilo nalo tutalipa uzito kupitia jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo ningependa kulisema, Waheshimiwa Wabunge wamechangia sana kuhusiana na umuhimu wa kuzingatia Katiba, umuhimu wa kufanya uchaguzi, na kujibu hoja ambazo zimetolewa, zinazosema, no reform no election.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu niseme kidogo kuhusiana na Reforms. Mwaka 1958 na 1959 nchi yetu ilifanya Uchaguzi Mkuu ambao ulijikita kwenye ubaguzi wa rangi. Vyama vya siasa vilitakiwa vichague mgombea mmoja Mwafrika, mgombea mwingine Muasia au Mhindi na mgombea mwingine Mzungu kutoka Ulaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1962 tulifanya reforms tukayaondoa haya, tukaleta uchaguzi ambao hauzingatii ubaguzi wa rangi. Tukaendelea na uchaguzi huo chini ya mfumo wa chama Kimoja, tukiwa na Rais mmoja mgombea.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulipofika mwaka 1995 – 2024 tumefanya mabadiliko. Tunafahamu, baada ya vyama vingi tuliondoa habari ya chama kimoja tukaleta vyama vingi. Tukaondoa mgombea mmoja kwenye nafasi ya Urais tukaleta wagombea wengi. Huko nyuma tulikuwa na wagombea wawili tu kwenye Ubunge, sasa tuna wagombea wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara ya mwisho mimi Songea Mjini tumegombea, ndani ya chama tu tulikuwa 31. Haya ni mabadiliko ambayo yamefanyika ndani ya mfumo wetu wa kisheria na wa Kikatiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu niseme, kati ya mwaka 1995 mpaka mwaka 2004 tulikuwa na sheria mbili za uchaguzi; Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya mwaka 1985 na Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1979. Tunavyoongea leo sheria hizo hazipo tena kwa sababu tumefanya mabadiliko, kuanzia mwaka 2004 kuja sasa tumefanya mabadiliko.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, tumefanya mabadiliko makubwa 15 ambayo napenda sana tuyasikilize tuweze kuyaongea vizuri, ili ambao wanataka kutuvuruga waache kutuvuruga. Badiliko la kwanza, tumefuta Sheria ya Uchaguzi ya Taifa ya Mwaka 1985 na kazi hiyo ya kufuta ilifanywa na Bunge hili Tukufu, linastahili pongezi zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumefuta Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 1979. Kazi hiyo nzuri imefanywa na Bunge hili Tukufu. Bunge hili linastahili maua yake. Mabadiliko mengine ni kutunga sheria mpya ya uchaguzi wa Rais, Wabunge, na Madiwani. Siyo kufanya mabadiliko, tumetunga sheria mpya, na mnafahamu sheria hii tuliitunga mwaka jana; Februari 2024 katika Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mjadala mrefu na kushirikisha pande zote, tukapata sheria yenye vifungu 168, ikielezea kila jambo linalohusu uchaguzi, kila mchakato, na watu wote walishirikishwa. Kama reforms kubwa tumezifanya Februari, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tujiulize, kutoka Februari, 2024 mpaka leo tunataka reform gani tena? Sheria hii ni mpya, haijawahi hata kutumika. Kwa hiyo, mabadiliko haya yamefanywa na chombo chenye mamlaka, ni Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumetunga sheria kwa mara ya kwanza, Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Mwaka 2024. Tume ya Uchaguzi ilitajwa kwenye Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ilikuwa haijatajwa na sheria mahsusi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya kwanza tumefanya reforms hizi kubwa Februari, 2024. Sasa Tume iko vizuri, ina sheria yake. Uhuru ambao umetamkwa kwenye Katiba, umefafanuliwa vizuri sana kwenye sheria hii. Ukitaka kuusoma uhuru wa Tume, siyo kwa jina tu, kwa kila kipengele; nenda kasome sheria hii utaielewa na utaitilia maanani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumetunga Kanuni za Maadili ya Uchaguzi wa Rais na Madiwani za Mwaka 2025. Vyama vyote vimesaini kanuni hizo, isipokuwa Chama cha CHADEMA. CHADEMA waliamua kutokusaini kwa utashi wao; wala hawakuzuiwa na mtu yeyote, na huwezi kumlazimisha mtu kusaini. Hizi ndizo reforms ambazo tumeziweka sasa. Kanuni za Uchaguzi za Mwaka 2025 ni reforms kubwa ambazo ziko hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Sheria ya Uchaguzi ambayo tuliitunga, kuna mambo ya msingi ambayo napenda pia kuyaongea. Moja, suala la kupita bila kupingwa limeondolewa kabisa. Hili ndilo lililokuwa lalamiko kubwa sana, mpaka watu walikwenda Mahakamani, Mahakama ikatoa hukumu. Hukumu ya Mahakama ile imetekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii tunajifunza hapa kwamba, kumbe tukitaka mabadiliko, twende Bungeni ama twende Mahakamani, siyo kulazimisha watu kuingia mtaani na barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na malalamiko kuhusu Wakurugenzi kusimamia uchaguzi. Suala hili limeshapatiwa tiba. Sasa hivi uchaguzi utasimamiwa na Maafisa Waandamizi ambao watateuliwa na Tume na kwa njia ya ushindani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeanzisha Kamati ya Usaili ya kupata viongozi wa juu wa Tume ili kupata umoja. Kamati hii inaongozwa na Majaji Wakuu wa Tanzania na wa Zanzibar. Pia, inaongozwa na Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, pamoja na mtu mwingine ambaye atateuliwa kutengeneza column ya watu watano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hapa, duniani kote namna ya kufanya uteuzi katika nafasi nyeti kama hizi ni ama ateuliwe na Rais ama ateuliwe na Bunge, halafu Rais aidhinishe, au ateuliwe na chombo huru na Rais aweze kuidhinisha. Sasa Tume hii ya Uchaguzi tungeileta humu Bungeni tuiteue sisi, haki isingetendeka, kwa sababu sisi tungekuwa tunaandaa Majaji wa kuamua shughuli yetu wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, chombo hicho ndicho mwafaka, ndicho chombo huru kabisa na kimezingatia viwango vya Kimataifa vya kuhakikisha kwamba Tume ya Uchaguzi inakuwa huru kama jina lake ambavyo limesema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uteuzi wa Mwenyekiti na Mkurugenzi pamoja na viongozi wengine wa juu utatangazwa. Watu wataomba, na watashindanishwa kwenye usaili. Wale watakaofuzu ndio watakaopendekezwa kwa Mheshimiwa Rais kwa ajili ya uteuzi. Jambo hili halijawahi kufanyika toka nchi hii imepata Uhuru. Reforms hizi tunazozifanya sisi hapa, sasa tuwaulize ndugu zetu, wanataka reforms gani zaidi ya hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, reforms zimekwenda mpaka Magereza. Sasa wafungwa nao wanaruhusiwa kupiga kura. Hii inakwenda sambamba Kifungu cha 10 pamoja na Jedwali la Tatu linalotupa maelezo haya. Pia, kura ya Rais inaweza ikapigwa popote pale, siyo katika kituo ambacho umejiandikisha. Haya ni mageuzi makubwa sana ambayo yamefanyika. Makosa ya unyanyasaji wa kijinsia yameingizwa na yamepewa msimamo mkubwa ili uchaguzi wetu siyo tu uwe huru, bali pia utende haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatujaishia hapo, suala la pingamizi limefafanuliwa vizuri. Wale wasioweza kulielewa wakasome Kifungu cha 26 pamoja na Kifungu cha 53, vinaelezea kuhusu pingamizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria niseme kwamba tumefanya reforms nyingi kuanzia mwaka 1961 mpaka leo. Tumekuwa na sheria nane, na tumekuwa na kanuni sita. Tumeshafuta sheria mbili na tumefanya mabadiliko (amendments) ya sheria sita. Hizo ni reforms kubwa kuliko zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natamka hapa kama Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria; dhamana ya kusema kuna uchaguzi au hakuna uchaguzi kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kwa mujibu wa Sheria Na. 1 na Na. 2 za mwaka 2024, ni Tume ya Uchaguzi ya Taifa na siyo mtu mwingine yeyote yule. Mtu mwingine atakayesema hivyo anajivisha joho ambalo sio lake. Tuwaombe Watanzania wampuuze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo ningependa kulisema ni umuhimu wa bajeti hii ambayo tumeipitisha safari hii. Bajeti hii sisi tunaita bajeti ya haki, kwa sababu ni bajeti ambayo inatampa haki Mtanzania, bajeti ambayo itatoa shibe kwa Watanzania wenye njaa na kiu ya haki; watapata haki katika kila eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni bajeti ambayo italeta mwanga na inaondoa giza la dhuluma ya haki kwa Watanzania wanyonge katika kona zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; bajeti ambayo itafuta chozi la mnyonge aliyekosa haki kwa muda mrefu sana; na bajeti ambayo ni mtetezi wa wananchi wanyonge, hasa wenye migogoro sugu na ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yetu Waheshimiwa Wabunge waweze kutuunga mkono ili kupitia bajeti hii tupeleke haki kwa Watanzania wanyonge ambao wanahitaji zaidi wapate haki hiyo, ambayo itawapa usawa, ambayo itawapa amani na hatimaye itawapa maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tena sana wewe kwa namna ambavyo umetuongoza kwa siku ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)