Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwa taarifa zote mbili. Kwanza, niseme ninaunga mkono taarifa zote za Kamati, kwa maana Kamati ya TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), pamoja na Kamati ya Elimu, Utamaduni, na Michezo. Naunga mkono taarifa zote zilizowasilishwa na Wenyeviti, maoni pamoja na mapendekezo yote ambayo yamewasilishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu ya TAMISEMI imepata ridhaa ya kutembelea maeneo mbalimbali nchini, kukagua miradi ya maendeleo, hususan maeneo ambayo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amepeleka fedha za miradi ya maendeleo. Bila shaka Wabunge wataungana nami kwamba, maeneo mengi Mheshimiwa Rais amepeleka fedha nyingi za miradi ya maendeleo, na kazi kubwa inafanyika kwenye kila eneo ndani ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, hatuna budi sisi kama Kamati kuendelea kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleao na kutimiza yale maono, pamoja na wasaidizi wake wa maeneo hayo kwa namna ambavyo wanaendelea kusimamia hizi fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pia shukrani na pongezi kwa Mheshimiwa Waziri mwenyewe, Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na Naibu Mawaziri, kwa ushirikiano na namna ambavyo wanaendelea kusimamia dhamira na maono ya Mheshimiwa Rais, kuhakikisha fedha hizi zinakwenda kuwahudumia wananchi maskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nisipowashukuru pia Makatibu Wakuu wa Wizara pamoja na Naibu Makatibu Wakuu. Pia, hata halmashauri ambazo Wakurugenzi wameendelea kusimamia fedha hizi kuhakikisha kwamba zinakwenda kutimiza yale malengo ambayo Mheshimiwa Rais amedhamiria kuwahudumia wananchi wanyonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, yapo mambo kadhaa sisi kama Kamati tumeshauri, na tungetamani Serikali iweze kuyatilia mkazo ili kuweza kukidhi haja na maono ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, tumeona fedha zinazokwenda kutekeleza miradi kwa upande wa TARURA. Fedha hizi hazitoshi na haziendi. Suala hili la TARURA lina sura mbili. Kwanza lina sura ya fedha yenyewe ya bajeti ambayo imetengwa na Wizara, zaidi ya shilingi bilioni 883 ambayo waliomba watu wa TARURA ili kutimiza wajibu wao katika kutekeleza maeneo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, lina sura ya pili ya fedha ya dharura, ambayo iliombwa ndani ya Bunge hili, zaidi ya shilingi milioni 326, kwenda kutimiza na kutengeneza barabara zilizokuwa zimeharibiwa na mvua upande wa El-Nino.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masikitiko ya Kamati, na ndiyo maana tumesema kwenye maoni na mapendekezo yetu, ni kwamba, hata ukiangalia la kwanza hili la fedha za bajeti, shilingi bilioni 883, mpaka kufikia Desemba, kwa maana ya Julai – Desemba, imekwenda 10% mpaka 11% peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika shilingi bilioni 883 wamepeleka shilingi bilioni 92 peke yake! Maana yake unaweza ukaona kwamba maeneo mengi wakandarasi wameendelea kudai, na kiukweli TARURA imeshindwa kutimiza wajibu wake, kwa sababu fedha za utekelezaji wa miradi haziendi kulingana na tulivyopitisha bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tulipitisha fedha hapa. TARURA walikuja wakaomba zaidi ya shilingi bilioni 326 kwa ajili ya miradi ya dharura, na dharura hii sisi Wabunge wote ni mashahidi, ilisababishwa na Mvua za El-Nino pamoja na Hidaya. Sasa, hii ni dharura, na tulitakiwa tuichukulie kama dharura, lakini unaweza ukaona, katika shilingi bilioni 326, fedha ambayo imekwenda ni shilingi bilioni 83 peke yake. Hawa watu hawawezi wakaendana na kasi hiyo ya udharura wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukubaliane kwamba jambo ambalo lina udharura lazima tulichukulie kwa udharura wake, kwa kuona ule muhimu wenyewe. Huwezi ukawa na dharura ukai-treat kwa mwaka mzima. Tunakwenda mwaka huu, na mvua zinaenda kunyesha awamu ya pili, hatujapeleka fedha hizi ambazo TARURA waliomba, zaidi ya shilingi bilioni 326. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wetu kama Kamati ni nini? La kwanza, ndiyo maana tumependekeza Mheshimiwa Waziri, hasa Waziri wa Fedha, wapeleke kwanza fedha zilizopo kwenye bajeti, zaidi ya shilingi bilioni 883, ili watu wa TARURA waende kutimiza wajibu wao kwenye maeneo mengi, kwenye barabara ambazo zinaharibika, na waweze kulipa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunapendekeza pia hii fedha ya dharura shilingi bilioni 326, haina haja ya kusubiri mpaka mvua zianze kunyesha awamu nyingine ya pili. Wapewe fedha hizi ili waende wakatimize kazi ya udharura. Shilingi bilioni 84 haiwezi kutosha, na ndiyo maana tukapendekeza kwamba, pamoja na hilo, ipo fedha ya World Bank kupitia DMDP, na tukasema fedha ile ilikuwa ni ya dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA wameomba zaidi ya shilingi bilioni 256, wakiwa wanaamini wakipewa fedha hizi, wakiunganisha na ile shilingi bilioni 83 angalau watakuwa na shilingi bilioni 340. Inaweza kusaidia na kutekeleza ilani kwenye maeneo mengi ya barabara za vijijini ambazo zimeharibiwa na mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha alione hili. Tunashukuru ametoa shilingi bilioni 83, lakini haitoishi. Tunaomba atoe fedha kupitia hii Miradi ya DMDP, hii shilingi bilioni 256. Wizara ilione hili; kama bado liko kwao, wapo kwenye mchakato wa manunuzi, waliharakishe ili angalau hawa watu wa TARURA wapate hii fedha shilingi bilioni 256, waende wakatekeleze wajibu wao katika maeneo mengi ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusiana na DART pamoja na UDART. Hapa kuna Wakala ambaye ni DART, lakini kuna mtoa huduma ambaye ni UDART. Hawa watu waliingia mkataba wa pamoja wa namna ya UDART kumlipa DART kwenye Access Fee ya barabara ambayo wanaitumia kutoa huduma ya mabasi. Kinachoshangaza, pamoja na makubaliano ya kimkataba, pamoja na sisi kama Bunge kupitisha bajeti iliyoletwa na Wizara hapa ndani, kwamba UDART watamlipa DART na fedha ile ni sehemu ya bajeti ya Wizara iliyoleta, leo hii tunaingia kwenye mgogoro ambao hauna sababu kwa taasisi mbili za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani leo UDART wanasema hawawezi wakalipa fedha kwa DART, kwa sababu ambazo hazina msingi wowote. Ndiyo maana tumeshauri kwamba, kwa kuwa tulipitisha hapa, na Sheria ya Bajeti ikalinda bajeti ile tuliyopitisha ndani ya Bunge, tunawaomba watu wa UDART waendele kulipa fedha kwa mujibu wa utaratibu wa sheria tuliyopitisha ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha aingilie kati. Asiruhusu huu mkanganyiko ukaenda kwa sababu hii ni sheria na tuliipitisha ndani ya Bunge. Hatuna sababu ya kuingiza mkanganyiko wowote, hasa kwenye taasisi mbili ambazo ni za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kwa sababu ya muda ni NeST. Tunakubaliana hapa, tulipitisha sheria wenyewe ndani ya Bunge mwaka 2023 mwezi wa 10. Sheria ambayo waliileta watu wa PPRA kupitia Wizara ya Fedha. Hatuna shaka juu ya utekelezaji, kwa sababu kiukweli inakwenda kusimamia utaratibu mzuri sana wa uratibu wa fedha zinazotumika kwenye maeneo ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria bila kuendelea kutoa elimu haitusaidii sana. Nichukue nafasi kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, aliona umuhimu huo akaunganisha semina ya Waheshimiwa Wabunge, Wakurugenzi, pamoja na watu wa PPRA, lakini bado tunaamini, kwa kuwa sisi tulipitisha sheria, PPRA wakaenda wakatengeneza kanuni na mwongozo, waende kwenye halmashauri zote na kwenye taasisi zinazotumia mfumo huu, watoe elimu ili angalau miradi ya maendeleo isiendele kusuasua. (Makofi)


Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa tuliyoiona kwenye miradi ya maendeleo, ni kwa sababu, ucheleweshaji mwingi ni kwa sababu ya mfumo. Wakurugenzi wanatangaza, hakuna wazabuni, na wakati mwingine hakuna mafundi. Unakuta maeneo mengine elimu ya kuutumia mfuko wenyewe kwa wale wanaotakiwa kutangaza, hasa walimu wa shule za msingi na sekondari, hauko stable. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba watu wa PPRA kupitia Wizara ya Fedha (watu wa Hazina), wakazunguke maeneo yote watoe elimu, na ikibidi panapobidi wapitie upya kanuni pamoja na mwongozo mliotoa. Kwa sababu haiwezekani, Mheshimiwa Rais anapeleka fedha nzuri sana kwenye maeneo hayo, miradi inachelewa kwa sababu ya mfumo tulioutengeneza sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezi kutusaidia sisi kama nchi, kwamba tumetengeneza mfumo mzuri, na Mheshimiwa Rais anapeleka fedha, halafu sababu inakuwa ni mfumo unaotuchelewesha, miradi inashindwa kuanza kwa kutimiza malengo na dhamira ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, watu wa PPRA warudi, waweze kuona namna ya kupitia ule mfumo, na watoe mwongozo na kanuni ili angalau hili jambo lisiweze kujirudia.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jafari Chege, kuna Taarifa.

TAARIFA

MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Chege. NeST bado ina tatizo kubwa sana kwani bado inadukuliwa. Kuna watu ambao wanadukua kiasi kwamba wengine wanaotaka ku-submit zile tender zao hawawezi. Kwa hiyo, mtandao huu bado una matatizo makubwa sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jafari, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo na ndiyo maana tumeendelea kusisitiza kama Kamati, na hata sasa hivi tunaendelea kusisitiza kama Wabunge. Hatuna shida na sheria tuliyoiunda sisi wenyewe, lakini shida ni elimu ambayo inatolewa na ndiyo inatusababishia miradi mingi ya maendeleo kukwama kutekelezwa kwenye maeneo haya ya halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya, niendelee kusema tena naunga mkono taarifa ya Kamati zote mbili. Ahsanteni sana, nashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)