Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi pia nashukuru sana kwa kweli kwa kupata fursa ili niweze kuchangia Wizara yetu ya TAMISEMI pamoja na Wizara ya Michezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo machache sana. Jambo la kwanza ni kuhusiana na ujenzi wa stendi ya Jiji la Arusha, na bahati nzuri, toka nimekuwa Mbunge nimeweza kuuliza maswali mara tatu yanayohusiana na ujenzi wa stendi hii. Swali la kwanza niliuliza tarehe 14/04/2021, nikauliza tena tarehe 04/09/2023 na tarehe 31/10/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, nilikuwa natamani nisome majibu ya Serikali kuhusiana na ujenzi wa stendi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa tarehe 14 mwezi wa Nne, 2021 majibu ya Serikali yalikuwa yanasema hivi, naomba niyanukuu kutokana na Hansard tuliyokuwa nayo:-
“Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Jiji la Arusha imetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 30 katika eneo la stendi mpya itakayojengwa, itazingatia pia mahitaji ya wafanyabiashara wadogo kama machinga, stendi ya taxi, pikipiki, bajaji, ofisi za Polisi, Usalama Barabarani na maeneo ya huduma mbalimbali. Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inayoendelea sasa ni taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mhandisi mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu wa mradi huo. Mradi huo wa ujenzi wa stendi ya kisasa Jiji la Arusha utajumuishwa kwenye mradi wa uboreshaji miundombinu (Tanzania Cities Transforming Infrastructure and Competitiveness (TACTIC)) utakaotekelezwa kwenye halmashauri 45 za Majiji, Manispaa na Miji nchini ambapo Serikali inaendelea na majadiliano na Benki ya Dunia.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo yalikuwa ni majibu ya Serikali ya tarehe 14/04/2021 ambayo yalituahidi kwamba mradi huu unakwenda kutekelezwa. Nikauliza swali tena tarehe 04/09/2023 na Serikali yetu ikaweza kutupatia majibu. Majibu ya Serikali yalikuwa ni kama ifuatavyo, na ninaomba ninukuu pia.
“Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mradi wa kuboresha miundombinu katika Majiji, Manispaa na Miji (TACTIC) awamu ya pili itatekeleza ujenzi wa stendi kuu ya kisasa ya mabasi katika eneo la Bondeni City, masoko mawili pamoja na bustani moja ya mapumziko kwa lengo la kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani. Mheshimiwa Spika, kazi ya usanifu imekamilika na taratibu za ununuzi kwa ajili ya kumpata mzabuni zinatarajiwa kukamilika mwezi Desemba mwaka 2023. Baada ya taratibu hizo kukamilika, utekelezwaji wa ujenzi kwenye maeneo yaliyoainishwa utaanza.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani Desemba, 2023 taratibu zitakamilika na ujenzi wa stendi utaanza. Hata hivyo, kwenye swali la nyongeza pia Serikali iliweza kutujibu, naomba ninukuu pia.
“Mheshimiwa Spika, kwanza, lini tunatangaza tender hiyo, kama nilivyosema, tupo kwenye hatua za utaratibu wa manunuzi na siwezi kuwa certain sana kusema lini, lakini Serikali tunahakikisha tu kwamba by December mwaka huu, yaani mwaka 2023 tutakuwa tumekamilisha taratibu zote za manunuzi na mkandarasi kwenda site kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huu. Mheshimiwa Spika, pili...”
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hii ya pili niiache kwa sababu haihusiani na stendi. Nikaja tena nikauliza mara ya tatu tarehe 31/10/2024, naomba pia nisome majibu ya Serikali.
“Mheshimiwa Spika, Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilifanya 2023 ikamaliza, ikatuahidi, mkandarasi mpaka leo hajafika, lakini anatujibu tena hapa:-
“Mheshimiwa Spika, Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, na usanifu wa kimazingira katika eneo la Bondeni City, zabuni ya ujenzi wa stendi hii ikatangazwa tarehe 19/01/2024 (mwaka jana) kupitia mfumo wa NeST na hatua iliyofikiwa ni ya upembuzi (due diligence) kwa wakandarasi waliopendekezwa ili zabuni itolewe kwa mkandarasi atakayekidhi vigezo kwa utekelezaji. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa mpango uliopo tathmini ya mradi imefanyika na kukamilika Julai, 2024, hatua ya kusaini mkataba itafanyika na ujenzi unatarajiwa kuanza ifikapo Januari, 2025.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la nyongeza wakatujibu tena, naomba ninukuu: “Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna uhitaji mkubwa wa stendi ya kisasa katika Jiji la Arusha eneo la Bondeni City na tayari Serikali imeshatangaza zabuni na imeshapata mkandarasi ambao waliomba. Hatua iliyopo sasa ni ya kufanya uhakiki wa maana (due diligence). Naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwamba mpango wa Serikali ni kuanza ujenzi mapema iwezekanavyo Januari, 2025 na mkataba utasainiwa wakati wowote kati ya Novemba na Desemba mwaka huu 2024.” Majibu yapo mengi naomba niishie hapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niiulize Serikali, Desemba 2023 imepita, Januari 2025 imepita, leo tupo Februari, 2025. Ukienda pale Arusha eneo la Bondeni City ardhi ipo eka 30 na hati ipo. Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kafanya kazi kubwa ya kutuletea mradi wa TACTIC ili stendi iweze kujengwa katika eneo lile. Sasa hawa wataalamu wanaohusika na taratibu za manunuzi, kumpata mkandarasi ili aweze kwenda site, watuambie tatizo lao ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mchengerwa, Waziri wa TAMISEMI yupo hapa ambaye sisi hatuna mashaka na usimamizi wake, nataka tujue kwamba mbona katika halmashauri nyingine na majiji mengine tender zimetangazwa, wakandarasi wamepatikana; kuna changamoto gani kwenye Jiji la Arusha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mtu anakwamisha, analeta uzembe, kwa nini Serikali haichukui hatua, kwa sababu lile ni Jiji la Kimataifa? Mheshimiwa Rais, kafanya kazi kubwa, kaleta pale Royal Tour, utalii sasa hivi umerudi katika mahali pake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais, kafanya kazi kubwa, ameleta pale wageni, mikutano kila siku na mji umechangamka. Ni aibu kutokuwa na stendi ya kisasa. Kwa hiyo, naomba Serikali ituambie katika haya majibu matatu waliyonipatia hapa Bungeni, lipi ni jibu la Serikali ili niweze kulichukua niweze kuwapelekea wananchi wenzangu katika Jimbo la Arusha Mjini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)