Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba za Kamati hizi mbili ambazo zipo Mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda mahususi kwenye hoja iliyopo Mezani, ninaomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Mchengerwa yupo hapa. Tuna mradi wetu wa Soko la Kwasadala, humu ndani kama ni kurudia, nadhani nimeshasema zaidi ya mara 10. Sasa hivi wapo Arusha wamejifungia wanafanya marekebisho madogo, nisaidiwe kusukuma tuanze kujenga soko hili la Kwasadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni sambamba na soko la Mula na lenyewe walishatangaza mkandarasi amepatikana, lakini nimeambiwa kulikuwa na changamoto za kitaalamu, na lenyewe nisaidiwe kusukuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni yale maombi maalum niliyompelekea Mheshimiwa Waziri yanayohusu shule chakavu 77. Nashukuru ameanza na Nalutu na nyingine lakini naomba tusaidiwe sana ni hizi shule zimejengwa muda mrefu. Watoto wetu karne hii kukaa kwenye shule chakavu ndani ya Jimbo la Hai, jimbo la mjini, siyo heshima. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, atusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nimekuwa nikisema hapa kwamba ile mikopo ya 10% ya halmashauri tumefanya marekebisho ya sheria kuingiza kundi la vijana na kuongeza umri kutoka miaka 30 mpaka miaka 45. Naomba sana, kwa kuwa Mama anazo fedha za kutosha, safari hii hebu tufunge macho tuongeze na kundi la akina baba, nao wakopeshwe. Hii 45 ukiangalia umri uliobaki ni kidogo sana, tufungue na wanaume wote waweze kukopeshwa. Nilishasema tena hapa, wanaume wengi wanapata matatizo ya kisaikolojia kwa kukosa hili jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niingie moja kwa moja kwenye mchango wa Kamati yangu ya TAMISEMI. Mimi ni Mjumbe wa Kamati hii na ninamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu mjanja, anatusaidia tunaweza kutekeleza majukumu yetu vizuri. Nampongeza sana Mheshimiwa Mchengerwa pamoja na wasaidizi wake wote. Wameweza kutupa nafasi, tumetembea karibu mikoa yote Tanzania na Halmashauri zake. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mpo vizuri kwenye majimbo yenu, tumepita huko, kazi imefanyika, majengo yamejengwa, barabara zimejengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani wananchi huko wanasema kile ambacho kimefanyika kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, hivi hakuna namna nao wakaitwa mahali ili waseme Rais wao ni Dkt. Samia Suluhu Hassan? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi siku ya Ijumaa nilikuwa kwenye ziara pale Rundugai, clip ninayo, mwananchi mmoja akasema, Mheshimiwa Mbunge huna namna ya kushawishi nchi yote tukae sehemu moja na sisi tutoe azimio, tuseme Mama Samia, tumemaliza hiyo kazi? Kwa hiyo, nilitaka niwaambie, Watanzania wapo kule wanatusubiri tupeleke jina la Mama Samia, wakamalize shughuli yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa niwapongeze sana akinamama Wabunge mliopo humu. Huu moto mliouwasha humu ndani, niwape taarifa umehamia kule nje. Akina mama wanasema safari hii tumepata Mama mwenzetu, tunataka tuwafundishe Watanzania akina mama wanaweza. Kwa hiyo, na akina mama kule mtaani wanasema, “sisi tunatembea na Mama Samia Suluhu Hassan.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa taarifa yenu na sisi wababa tulishasema zamani, huyu ni mama yetu, hatuna wasiwasi, wababa tupo hapo nyuma yenu. Akina mama kuna msemo zamani ulikuwa unasema eti, akina mama hawapendani, lakini safari hii si tumeshauvunja! Akinamama wanapendana kuanzia huku Bungeni na kule nje na sababu tunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona treni hapo, tunapanda treni kama tupo Uturuki. Tunatoka Dar es Salaam, asubuhi tupo hapa. Tunaona Bwawa la Mwalimu Nyerere, Naibu Waziri Mkuu ametuambia hapa linakabidhiwa muda siyo mrefu, tunaona majengo kila mahali. Hivi Watanzania tunataka nini? Huyu mama tunataka tumpe nini? Huyu mama anatudai, na haki yake ni kura za kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo madogo. Makubwa yalishafanyika. Haya ninayotaka kueleza ni madogo tu na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI aelewe, ni madogo madogo, makubwa yameshafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunasubiri kwenda kumaliza kazi. TARURA amesema Makamu Mwenyekiti wetu mchangiaji wa kwanza, sisi tunamwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, kazi kubwa ilishafanyika, aachilie fedha kwenye eneo hili, kazi ikakamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu barabara zimechongwa za kutosha kwa kweli, lakini sasa kuna changamoto wakandarasi wameanza kukimbiza, hawapewi fedha, na sisi tunamsemea Mheshimiwa Waziri wetu wa TAMISEMI, anajitahidi sana. Niseme kwamba Wizara ya Fedha hebu ijitahidi itoe hizi fedha kazi ikafanyike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo lingine hapa, tulipata mafuriko, nami nikapata mafuriko kule kwangu. Daraja la Mkwarungo halipitiki, madaraja mengine kule Sonu, wananchi wanalalamika. Tunaomba fedha zile za TARURA ambazo ni shilingi bilioni 443 zilizopangwa ziende zote. Zimepelekwa shilingi bilioni 92 badala ya shilingi bilioni 443. Hizi fedha zilizobaki, au nimsindikize Mheshimiwa Mchengerwa twende wote pale Hazina tukakae hapo. Sasa naomba sana, tafadhalini sana, hizi fedha ziende. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mahsusi niseme pale kwetu Hai, ardhi imekuwa ni ndogo sana kiasi kwamba tunayoitegemea kiwango kikubwa ipo kwenye mashamba ya ushirika. Naomba Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, waitazameni Wilaya ya Hai wakijua haina ardhi kubwa, ardhi imekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yale maeneo ya ushirika yaliyopo pale ni kwa nini tusiyaweke kwenye Mfumo wa PPP, kama ambavyo tumefanya pale Karikoo? Tumefanya tathmini, evaluation ya ardhi, tukaithaminisha ile ardhi yetu, tukasema hii ardhi ni shilingi bilioni 13.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatafuta mwekezaji kwa Mfumo wa PPP. Tunamwambia njoo wewe na bilioni zako 13; za kwetu 13 za ardhi, za kwako 13 za uwekezaji, tunajenga hoteli. Pale mwisho wa siku kwenye turnover ya mapato tunagawana. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Wizara ya Kilimo kufanya utafiti, ni namna gani sasa Wilaya yetu ya Hai, yale maeneo madogo tunaweza tukayatumia, tukaweka mazao ambayo yanaweza kuongeza pato la Wananchi wa Jimbo la Hai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba jambo hili ni mtambuka. Migogoro ya ardhi, na huu ni utapeli mwingine umeingia. Nasemea kwenye Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ili Waziri alewe. Siku hizi limekuwa ni jambo la kawaida mtu kwenda Mahakamani, anachukua mmiliki ambaye ni fake anamweka. Yeye anasimama upande huu, wewe unashangaa unaletewa notice unaondolewa kwenye eneo lako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sisi ni wahanga kwenye eneo hili. Nina watu wengi sana ambao wamenyang’anywa nyumba zao kwa namna hiyo. Watu ambao wamezeeka, wagonjwa, yatima, wajane na ambao wanaishi nje ya Tanzania, imekuwa ni utamaduni wa kawaida jamaa anaenda pale anatengeneza, anaangalia huyu mtu yupo Bunge, safari hii ana miezi mitatu yupo pale Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachokifanya ni nini? Anatengeneza mmiliki hewa, anaenda naye Mahakamani, kesi inakimbizwa haraka haraka, wewe unashaanga unaletewa notice ya kuondoka nyumbani. Hili jambo linaumiza Watanzania wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hizi zinazohusika zikae chini, ikiwemo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Ardhi na Katiba na Sheria, mtazame jambo hili. Wazee wengi wanakufa kwa kihoro kwa kuondolewa kwenye nyumba zao na matapeli walioko kwenye simu, siyo hao; wamehamia kwenye ardhi. Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nasema NeST siyo tatizo, tatizo ni watumiaji wapewe elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)