Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza, nianze kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote, kwa kweli wametuwakilisha vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kuona kwamba, sasa ipo haja ya kuongeza mafao au marupurupu kwa walimu. Alilizungumza hilo juzi tu kwenye mkutano, walimu wameshaanza kuandaa maua yake. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais ameona kwamba, kweli walimu ni watumishi ambao wanatakiwa wapate mishahara ya juu kuliko watumishi wote katika nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kusema hayo, nawaomba wale wanaohusika waanze kuchakata, kufikiria. Kwa sababu Mheshimiwa Rais amesema sasa wao, Utumishi, Wizara ya Fedha, waanze kufikiria ni namna gani wataongeza ili Mheshimiwa Rais atakapowaita wawe na majibu, wasianze tena kurudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, nirudi kwa pongezi nyingine. Ni juzi tu kuna watoto walitekwa, wale wanafunzi wadogo, wakapatikana. Nampongeza sana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza kwa kufanya kazi ile ya kishujaa kuwaokoa wale watoto. Ingawa kuna watu wengine wameanza kubeza, eti kwa nini waliwaua wale majambazi? Wangewapiga miguuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi wale majambazi wangerudi ndani mara moja na kufyeka wale watoto, hao Polisi si tungewafukuza kazi. Kwa hiyo, tuwapongeze, lakini tusibeze, tusilete mambo ya siasa. Wale watoto wameokolewa na wazazi wao wamefurahi. Namwomba sana huyo Kamanda wa Mkoa wa Mwanza aungane na makamanda wangine wakawatoe watoto wote, vijana wote waliotekwa ili wawapeleke kwa wazazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa hili la kwetu la VETA. Kuna VETA 64 mpya, mimi namwomba sana Waziri wa Fedha, mpaka sasa, hizi VETA zinatakiwa ziwe zimeshamalizika, lakini hivi ninavyoongea zinasuasua. Tulishawaambia wananchi huko, watoto wamejiandaa waende VETA, lakini bado hazijafikia kumalizika kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, naomba unisikilize, VETA hizi 64 zinatakiwa ziishe. Sasa mimi ninaongea hapa jambo la msingi, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu naona hapo sijui vipi? Naomba unisikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha na Wizara ya Elimu hakikisheni hizi VETA zinakwisha. Wakati mwingine nashangaa, eti tunasema kuna VETA ya mfano. Kwa hiyo, hizi VETA nyingine ni za namna gani? Tunapojenga VETA sasa hivi zote ziwe VETA bora, kama ile tuliyoenda kuiona Kagera, VETA ya mfano, sasa hizi nyingine ni VETA za namna gani? Kwa hiyo, tunapofanya hiyo kazi, VETA zote ziwe na uniformity, zote zifanane ili kutoa elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, la VETA naona mmenielewa. Hilo la VETA limeeleweka, kwamba zijengwe kwa ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, nije kwenye suala la madeni. Kuna viongozi wa vyuo vikuu wengine wamestaafu, wengine bado wapo kazini, fedha zao zote zimekaguliwa, lakini bado hawajalipwa mpaka leo. Mpaka nashangaa, jamani kuna tatizo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, hebu aende pale Utumishi akutane na Katibu Mkuu Utumishi, na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha. Siwafundishi kazi, lakini naomba hebu wakutane wamalize madeni haya ya hawa viongozi wa vyuo vikuu. Nilisema wakati fulani, hawa viongozi wa vyuo vikuu hawana kelele, na hawajui hata kulalamika, lakini tusichukue hicho kuwa ndiyo kigezo. Hebu tuwape stahili zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nije kwa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kuna watumishi walifanya kazi kipindi cha Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, walivyomaliza kufanya hiyo kazi walikuwa na kitu kinaitwa HS (HandShake). Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alisaini, hao ni wale Wakuu wa Wilaya. Sasa mpaka leo wale Wakuu wa Wilaya bado wanangojea zile fedha zao ambazo waliahidiwa au zilishasainiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne. Hivi ni tabu gani inayofanya wasilipwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili nalo ni lake. Nilimwambia siku moja hapo vizuri, kwa upole, lakini leo nalisema kwa sauti. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, yaani mpaka wale watumishi wakajipa majina, wanajiita nyamakazi. Wanafanya kazi Wakuu wa Wilaya, hebu ile handshake yao muwape kwa sababu Mheshimiwa Rais alishaipitisha. Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia, analijua hilo, wala hana shida, ninyi hapo katikati kwa nini mnambwelambwela? Naomba mwasaidie hao Wakuu wa Wilaya ili waweze kutulia kule, waweze hata kufanya shughuli nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua ukishamaliza, ukitoka hapa, kama huna shughuli nyingine ya kufanya, ukapewa ule mzigo wako, kidogo unaweza ukafanya kitu, lakini sasa hivi wapo kule nje masikini ya Mungu, wengine wala hata hawajui wafanye nini? Hebu Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Utumishi na Waziri wa Fedha, hakikisheni sasa hili suala la handshake ya Wakuu wa Wilaya linafika mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa kunipa muda. (Makofi)