Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza, kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, kwa kunijalia afya na kuweza kusimama hapa kuchangia katika hoja hizi mbili. Nitajikita zaidi kwenye hoja ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya TAMISEMI kwa wasilisho zuri, amewasilisha vizuri na hayo ni maoni ya Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kuhusiana na masuala ya kutoka katika mkoa Wangu, na hususan katika Jimbo la Tabora Mjini, ambako kazi kubwa na nzuri Mheshimiwa Rais ameifanya. Mimi nikiwa ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, nimeona kwa macho namna ambavyo fedha nyingi zimekwenda katika miundombinu ya shule, hospitali na zahanati, zimejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, haina mashaka yoyote ya kupongeza kazi nzuri na kubwa ambayo inafanywa na Mheshimiwa Rais kwa kupeleka fedha kwa wananchi na fedha ile ikawa na tija kwa sababu wanapata kile wanachokistahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ujenzi wa shule, hospitali na miundombinu mbalimbali katika nchi hii, changamoto hazikosekani na katika changamoto, sisi kazi yetu kubwa ni kuishauri na kuisimamia Serikali. Pale ambapo tunaona kuna upungufu tunaomba watusaidie, ili wale wananchi waweze kupata kile wanachostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kuhusiana na Kituo cha Afya cha Maili Tano, pale Tabora. Kituo hiki cha afya majengo yake siyo rafiki sana kwa sababu yalikuwa yanatumika na wale waliokuwa wanatengeneza barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapotaka kusema kituo cha afya, nami binafsi ninayetembea katika nchi kuangalia vituo vya afya vinavyojengwa, pale Kituo cha Afya cha Maili Tano bado hakijakamilika kuitwa kituo cha afya japokuwa kinatumika. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri naye yupo hapa, watusaidie kwenda kupeleka majengo yanayotakiwa ili kituo hiki cha afya kiweze kukamilika kuitwa kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, hakuna jengo la mochwari. Huwezi kuwa na kituo cha afya ambacho hakina jengo la mochwari. Hakuna jengo la mionzi wala hakuna jengo la wagonjwa wa nje, la OPD. Tunaomba sana Serikali iweze kupeleka majengo haya ili kituo hiki cha afya kiweze kukamilika na wananchi hawa waweze kukitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashukuru sana, tulikuwa na ukosefu wa jenereta, Serikali imeahidi kupeleka jenereta ndani ya mwezi huu. Nafikiri kuanzia tarehe 15, au 16 Februari, 2025, jenereta litakuwa limefika katika kituo cha afya pale. Wananchi wataendelea kupata huduma ambazo zinatakiwa kwa sababu ya changamoto ya kukatikakatika kwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatuna jengo la kufulia. Naomba sana majengo hayo yaweze kukamilika, kama ambavyo Serikali imekuwa ikiahidi ili wananchi wale wa Tabora, kile kituo cha afya ambacho kinahudumia wakazi wengi wa maeneo ya kata zilizoko karibu, waweze kupata huduma bora na stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ujenzi wa hizi shule za BOOST na SEQUIP, bado sisi katika Halmashauri yetu ya Tabora Mjini tuna changamoto ya shule chakavu, hususan za msingi. Tumekuwa na shule chakavu nyingi sana, na kauli ya Serikali wakati wote tunapokuwa tunahoji na kuuliza, wamekuwa wakitoa kauli ya kwamba, Halmashauri zifanye kazi ya kukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo Halmashauri zinazoweza kufanya hayo, lakini kuna Halmashauri, hususan sisi wenye Mikoa ya pembezoni, ukimwambia mtu akarabati shule zaidi ya 14 zilizochakaa, ambazo zimejengwa tangu wakati wa mkoloni, hawatutendei haki. Naiomba sana Serikali, pamoja na kazi nzuri inayofanyika ya ujenzi wa shule mpya, hizi shule chakavu nazo zikafanyiwe ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema na ninazungumza tena, shule zimechakaa kiasi kwamba zikija kudondoka maafa yatakuwa ni makubwa kuliko hata tunavyodhani. Nikikwambia katika Jimbo la Tabora Mjini tu, kuna shule karibia 14 zimechakaa kweli kweli na zinahitaji ukarabati wa hali ya juu ili hata unapoweka majengo mapya, basi yaendane angalau na hali halisi ya maeneo husika, ili yaweze kupendeza na kuendana na hali halisi ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna shule ambazo zina watoto wengi sana, wengi mno! Kuna shule moja pale Tabora Mjini inaitwa Majengo, ina jumla ya watoto 2,525. Katika shule hii wananchi wamejitahidi, kuna maboma ambayo wamejenga pale zaidi ya matano. Unaiambia Serikali ya Halmashauri iweze kusaidia kumalizia hayo maboma, tunapata wapi hizo fedha? Kwa kipato gani ambacho Halmashauri zetu za pembezoni wanakipata? Kwa hiyo, lazima ifike mahali waangalie na mapato.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa, Mheshimiwa Subira. Taarifa Mheshimiwa Kingu.

TAARIFA

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na mchango mzuri kabisa wa kizalendo wa Mbunge huyu, Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, nampa taarifa kwamba, Shule ya Msingi ya Puma, Jimbo la Singida Magharibi, ina wanafunzi zaidi ya 2,000 mpaka inasababisha watoto kusoma kwa shift. Sasa kwa kuwa Waziri wetu mchapa kazi yupo hapa, najua atakapokuja kutoa hitimisho atazikumbuka shule hizi zinazotajwa na Mheshimiwa Mwaifunga na hii ya Puma. (Makofi)

MWENYEKITI: Unaipokea hiyo taarifa, Mheshimiwa Hawa Mwaifunga?

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake kwa sababu ni changamoto kubwa sana kuwa na shule yenye watoto wengi, halafu madarasa hayatoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hizi shule tano hapa katika Manispaa ya Tabora, zina changamoto kubwa sana. Naiomba Serikali itusaidie; kwanza, iende ikaongeze madarasa; na pili, yale maboma ambayo yameanzishwa na wazazi katika maeneo hayo, wayamalizie, ili watato wetu waweze kusoma kwa raha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Waziri wa TAMISEMI yupo hapa, anaelewa hiki ambacho nakizungumza. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, pamoja na kazi nzuri na kubwa anayoifanya, lakini watoto hawa wa Jimbo la Tabora Mjini wanahitaji kupata elimu bora, na elimu bora ni pamoja na majengo ambayo wanasomea. Kama ambavyo Mheshimiwa Rais anapambana kujenga majengo mengine mapya, haya ya zamani yafanyiwe ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba pia, katika ujenzi wa hizi shule mpya ambazo zinajengwa, ziangalie uwiano na wingi wa watu kulingana na Sensa ya Mwaka 2022. Unakuta kuna maeneo mengine shule zinapelekwa, lakini uhitaji ni mdogo kuliko kwenye maeneo mengine. Maeneo mengine watu ni wengi sana, watoto ni wengi sana na wengine mikoa yetu watu tunazaa sana. Kwa hiyo, unakuta population ya watoto ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema leo katika Mkoa huu upeleke shule tano, huu upeleke shule tano, wengine unatuumiza kuliko wengine, wanakuwa wanapata zaidi kuliko tunavyopata sisi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)