Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naunga mkono hoja za Kamati zote mbili. Pili, namshukuru Mheshimiwa Rais na nina sababu ya kumshukuru. Wapo watu wanauliza maswali. Kwa nini, Wabunge tunashukuru sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuwa ninayo sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais. Naomba Wabunge wenzangu tunaposhukuru tutaje na mambo aliyoyafanya kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi hiki mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Mlimba na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimejengwa shule za sekondari tisa; mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Mlimba na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, zimejengwa shule za msingi 16 mpya bila michango ya wananchi; mimi nikiwa Mbunge wa Jimbo la Mlimba na Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, vituo vinne vya afya vimejengwa bila michango ya wananchi na vinatoa huduma, na hivi punde, tunatarajia kujenga pale na Kata ya Utengule. Sasa kwa nini, nisishukuru kwa mambo makubwa namna hii? Ninayo mengi ya kushukuru, lakini itoshe tu kushukuru hayo machache. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye changamoto. Bado kuna changamoto kubwa mbili kwenye Jimbo langu na wananchi wa Mlimba wamenisisitiza sana niliseme leo. Changamoto ya kwanza ni sekta ya miundombinu, hasa barabara za TANROADS na TARURA, bado wananchi wa Mlimba wameendelea kusisitiza jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la maji, hasa Mradi wa Mlimba. Ule mradi sasa umesimama na Waziri wa Maji, kama yupo, au Naibu Waziri wanisikie. Mheshimiwa Rais alikuwa na nia njema Kata ya Mlimba kuwatua akina mama ndoo kichwani. Mradi ule una thamani ya shilingi bilioni 7.4, sasa umesimama yapata miezi sita. Najua Mheshimiwa Waziri wa Maji anafanya kazi nzuri, nadhani katika hili ataenda kukamilisha vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni barabara. Hapa namshukuru Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na amekuwa balozi wa wakandarasi wa ndani. Wapo wakandarasi wanafanya vizuri, lakini wapo wakandarasi wanatuangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo nitatoa mfano, mimi Jimbo langu la Mlimba tuna barabara ya lami pale inayojengwa kuelekea Makao Makuu ya Halmashauri. Barabara hii ilisainiwa tarehe 22 Mei, 2023, Mkandarasi ni Mell Construction Company Limited.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi huyu alipaswa akamilishe kazi hii ya tarehe 23 Januari, 2024 lakini mpaka leo yapata miaka miwili mkandarasi huyu hajafanya kazi ile na hana sababu, hadai chochote Serikalini. Sasa huyu naomba ni-load formal complains kwa PPRA, nipeleke maombi yangu kwa njia ya mdomo kwa PPRA na CRB kama wananisikia huko walipo. Hatuna sababu ya kuendelea kuwa na wakandarasi wa namna hii, wanaokwamisha kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba Mheshimiwa Waziri katika hili pia kwa upande wako uchukue hatua mapema leo hii, ikiwezekana hata leo mkandarasi huyu asimamishwe ile kazi apewe mwingine na watu waendelee kupata huduma pale Mlimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninavyoenda kumalizia, nataka nitoe elimu kidogo kwenye sekta mbili; Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Ardhi hasa kwenye eneo mahususi la ardhi. Kwa kuwa, namfahamu Waziri wa Ardhi, sasa hivi kaka yangu Mheshimiwa Ndejembi ni transformative, ni kijana ambaye anataka mabadiliko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akiwa Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, akiwa anamsaidia Mheshimiwa Mama Jenista, nilishauri hapa kwa habari ya upungufu wa OPRAS. Ninaamini alimshauri vizuri Waziri wake, Serikali ikafanya mabadiliko, ikaachana na Mfumo wa OPRAS ikaja na PEPMIS na PIPMIS. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naamini leo ni Waziri kamili wa Ardhi na ni transformative, atakwenda kupokea haya ninayosema leo. Nampongeza yeye, Naibu wake, kaka yangu Mheshimiwa Pinda, Katibu Mkuu, pia na Kamishna Mathew, wanafanya kazi kubwa kwa Watanzania. Vilevile nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuwa naye ni transformative, katika hili atanisaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri bado kuna obwe kwenye usimamizi wa watumishi wa Sekta ya Ardhi. Nashauri watengeneze kanuni au waangalie marejeo kwa mujibu wa sheria. Leo hii, mfano Afisa Ardhi wa Mlimba anapewa kazi na Mkurugenzi wa Halmashauri kama ndio kiongozi wake wa karibu anayemsimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Kamishna anampa maelekezo. Kwa hiyo, ana mabosi wawili, anafuata lipi? Sasa kuna mkanganyiko hapa, lazima huu utatuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine, kama Taifa mpaka leo hatuna National Land Use Master Plan. Mpango kabambe wa matumizi bora ya ardhi wa Kitaifa na kwa kuwa Waziri wa Ardhi ameanza kufanya matukio ya Sera ya Ardhi ya Mwaka 1995, ninaamini atakwenda ku-accommodate ninachokisema leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa ni lazima National Land Use Master Plan (Mpango Kabambe wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi), ardhi yetu, hizi kilometa za mraba 645,000 zingepaswa kuwa kwenye National Land Use Master Plan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi ya jumla itengenezewe utaratibu wake, ardhi ya hifadhi itengenezewe utaratibu wake na ardhi ya vijiji itengenezewe utaratibu wake. Halafu kwenye Halmashauri huku, Halmashauri zote ziwe na document mbili; Land Use Master Plan, yaani Mpango Kabambe wa Matumizi Bora ya Ardhi na Infrastructure Master Plan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kazi ya Halmashauri, sasa hapa wanaingia Waziri wa TAMISEMI. Halmashauri zako nchini hazizidi 20 ambazo zina Land Use Master Plan. Ukienda Majiji yote ya Tanzania ukiacha Jiji la Dodoma, Arusha ni squatter city, Dar es Salaam squatter city, Mbeya na Tanga ni squatter city. Why, na katika hili hatutaweza kuondoa migogoro ya ardhi katika nchi hii, kwa nini? Kwa kuwa, hatuna hizo document za Land Use Master Plan na Infrastructure Master Plan, na inawezekana kwa kutumia mapato ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dodoma tulifanya hayo kwa mapato ya ndani. Dodoma imepangwa kwa eneo lote, ila imepimwa kwa 70% na ilifanyika kazi hiyo kwa miaka mitatu. Inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ushauri wangu, kazi ya Waziri wa Ardhi kama Waziri wa Kisekta ni kusimamia hiyo instrument ya Land Use Master Plan, halafu yeye anayokaa nayo kama ana remote control hapa, anamwangalia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Namtumbo pale, je anafuata kilichoelekezwa na Wizara kama Wizara ya Sekta? Hana sababu ya kusafiri sana. National Use Master Plan ndiyo mwarobaini wa migogoro ya ardhi nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)